Ukraine imesalia na siku zisizozidi 30 za mapigano dhidi ya Urusi kabla ya hali ya hewa kuzuia mashambulizi yake, afisa wa ngazi ya juu wa jeshi la Marekani anasema.

Akiongea na BBC Jumapili kupitia kipindi cha Laura Kuenssberg, Jenerali Mark Milley alisema hali ya baridi itafanya iwe vigumu zaidi kwa Ukraine kutekeleza mashambulizi.

Alikiri mashambulizi hayo yalikwenda polepole zaidi kuliko ilivyotarajiwa. Lakini alisema: “Bado kuna mapigano makali yanayoendelea. “Waukraine bado wanasonga mbele na wamekuwa na maendeleo thabiti.”

Jenerali Milley alisema ni mapema mno kusema kama mashambulizi ya kukabiliana na mashambulizi ya Urusi yameshindwa, lakini akasema Ukraine “inaendelea kwa kasi ya utulivu katika mstari wa mbele wa Urusi”.

“Bado kuna muda wa kutosha, labda takriban siku 30 hadi 45 kabla ya hali ya hewa mbaya kuanza, kwa hivyo Waukraine hawajamaliza. “Kuna vita ambavyo havijafanyika… hawajamaliza sehemu ya mapigano ya kile wanachojaribu kutimiza.”