Na Stella Aron, JamhuriMedia

Mfumo dume ni kikwazo kimojawapo katika suala la ushiriki wa afya ya uzazi na kuchangia baadhi ya wanawake kutumia njia ya uzazi wa mpango kwa njia ya kificho na usiri.

Mecy Haule (46) (si jina lake halisi), mkulima wa tumbaku na mkazi wa Tabora, anasema kuwa ana miaka 14 ndani ya ndoa na ana watoto sita ambao wamepishana kuzaliwa kwa mwaka mmoja na nusu na wengine miaka 2.

Akizungumzia historia ya maisha yake, Mecy anasema kuwa baada ya kumaliza elimu ya msingi hakupata bahati ya kuaendelea na masomo hivyo alishirikiana na wazazi wake kwenye kilimo cha tumbaku na kulina asali.

Anasema kuwa aliendelea na shughuli ya kilimo kwa muda mrefu na alifanikiwa kununua shamba lake la hekari 2 ambalo alilima tumbaku na kahawa.

“Siku moja ambayo sitoweza kuisahau niliamka asubuhi na kwenda shambani kwangu ambako ni mbali kidogo na shambani kwa wazazi wangu.

“Nilipofika shambani niliweka chakula na maji yangu pembeni, kisha nikaanza kupalilia upande ambako nilikuwa nimepanda kahawa ghafla alitokea kijana ambaye sikuweza kumtambua kwa haraka akiwa ameshika panga.

“Aliniziba mdogo kisha akanipiga ngwala na kunibaka na sikuweza kupiga kelele kutokana na namna alivyonisokomeza nguo mdomoni.

“Niliwaeleza wazazi wangu kuhusiana na tukio hilo baba alilazimika kumsaka kijana huyo ambapo kila siku alikuwa akinisindikiza shambani kisha yeye hujificha pembeni akiwa na silaha.

“Hata hivyo baada ya muda niligundua kuwa ni mjamzito nikiwa na miaka 21 na nilimweleza mama ambaye alifanya jitihada kwa siri za kunipa dawa za kienyeji ili mimba itoke

“Nilitumia dawa za aina mbalimbali ambapo mimba hiyo ilitoka ingawa nilipatwa na changamoto kubwa baada ya damu nyingi kutoka na pia maumivu makali ya tumbo yaliyomsababisha mama kwenda hospitali akijifanya yeye ndiye anaumwa tumbo na alipokewa dawa aliniletea na baada ya wiki tatu nilianza kupata unafuu,” anasema Mecy.

Mecy anasema kuwa hivi sasa ameolewa na ana watoto sita na bado mumewe anahitaji watoto wafike 10 jambo ambalo limesababisha ugomvi ndani ya ndoa.

Anasema kuwa kwa upande wake idadi ya watoto aliopata wanatosha kwani alibeba ujauzito wa karibu karibu ambapo mtoto wa mwisho aliyezaliwa mwaka 2018 alinusurika kufa baada ya kushindwa kujifungua kutokana na kutokuwa na nguvu na pia kutokwa na damu nyingi.

“Nilinusurika kufa kwani sikuwa na nguvu hivyo nilipata bahati kwa kuwa gari ya wagonjwa ilikuwepo siku hiyo ambapo nilikimbizwa hospitali ya Mkoa wa Tabora pamoja nikiwa hoi.

“Nilifikishwa hospitalini na kufanyiwa upasuaji na mtoto alitoka akiwa mgonjwa hivyo nililazwa wiki tatu ambapo mume wangu alilazimika kuuza ng’ombe ili apate pesa ya kunitibia.

“Tangu siku hiyo sihitaji tena kwani pia niliumwa na niliishiwa na damu hivyo nimelazimika kutumia njia za uzazi wa mpango kwa siri kwani kwani mume wangu bado anahitaji watoto na nikimshirikisha suala la uzazi wa mpango inakuwa ugomvi mkubwa hadi taarifa zinafikishwa kwa mama mkwe kuwa nina mwanaume mwingine.

“Mwanzoni mwa mwaka huu aliniuliza mbona kimya muda mrefu nikamjibu hata mimi sijui ni kwanini hivyo nilimshauri twende hospitali tukapate ushauri sababu ya kutopata mimba lakini aliniambia kuwa hayo si masuala ya wanaume hivyo alinitaka mimi niende na majibu nimletee.

“Siku akifahamu kuwa nimejiunga kwenye huduma ya uzazi wa mpango baada ya kupata elimu kuwa nahatarisha maisha yangu lakini mume wangu anakataa masuala hayo kwa sababu kuwa yeye ana uwezo wa kuwale na kuwasomesha kutokana na ng’ombe wengi alionao” anasema.

Tanzania ni kati ya nchi zenye uwiano wa juu wa vifo vya wajawazito duniani (410 kwa kila watoto 100,000 wanaozaliwa wakiwa hai), na utoaji mimba usio salama ni moja kati ya sababu zinazoongoza.

Utoaji mimba usio salama unachangia hadi asilimia 19 ya vifo vya uzazi nchini Tanzania huku huduma ya afya kwa ajili ya kudhibiti matatizo ya utoaji mimba usio salama ukiigharimu serikali fedha nyingi.

Ripoti ya Hali ya Idadi ya Watu Duniani ya mwaka 2022, iliyotolewa na Shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulika na idadi ya watu na afya ya uzazi, (UNFPA) inasema karibu nusu ya mimba zote, ambazo ni jumla ya milioni 121 kila mwaka duniani kote, hazikutarajiwa.

Daktari bingwa wa magonjwa ya wanawake na uzazi kutoka Hospitali ya Mtakatifu Francis Ifakara, Elias Kweyamba anasema kuwa kuna sababu mbalimbali ambazo huchangia wanawake kushiriki kwenye uaviaji licha ya kujua kwamba anahatarisha maisha yake.

Anasema kuwa bado Serikali ina kazi ya kuelimisha jamii kuhusiana na uzazi wa mpango na kuzuia mimba zisizotarajiwa kwa kuelimisha jamii na pia ni vyema kukawa na upatikanaji wa huduma baada ya mimba kuharibika ili kupunguza vifo vya uzazi.

Dk Kweyamba anasema kuwa mila na desturi zimekuwa sababu ya baadhi ya wanawake kufanya uaviaji hivyo bado elimu ya afya ya uzazi wa mpango kwa wanaume na wanawake inahitajika kwani wapo wanaobeba mimba kutokana na shinikizo la wenza wao bila ya kujua madhara na mwisho hushiriki katika uaviaji mimba usio salama.

“Suala kuzuia mimba na kupanga uzazi wengi wanadhani ni jukumu la mwanamke lakini ukweli kwamba wanaume nao wana njia za kupanga uzazi na wakizitumia kwa usahihi, zinaweza kuleta matokeo chanya na kupunguza uaviaji mimba.

“Umefika wakati kwa wanaume kujua kuwa matumizi ya njia za uzazi wa mpango si jukumu la mwanamke pekee bali linabebwa na usawa wa kijinsia,” anasema.

Anasema kuwa kuna faida nyingi kama wanaume endapo watashiriki kikamilifu katika kupanga uzazi ndani ya familia kwani itasaidia kuepuka mimba zisizotarajiwa lakini pia kupata muda wa mwanamke kupumnzika na kujishughulisha na kazi nyingine za maendeleo.

Hata hivyo Dk Kweyamba anasema kuwa wanawake wanaofariki kutokana na uaviaji mimba hutokana na kukosa huduma muhimu mara baada ya mimba kuharibika kutokana na kufanya uaviaji mimba kwa njia zisizo sahihi na kwa kificho.

Anasema kuwa huduma ambayo mwanamke anatakiwa kuipata kitaalamu inaitwa Comprehensive Post Abortion – (cPAC) ambayo kwa Kiswahili inatambulika kama “Huduma Baada ya Mimba Kuharibika”, hii hutolewa kwa ajili ya kulinda usalama wa afya ya mwathirika wa tukio, wataalamu wa afya wanasema huduma huu ni muhimu sana kwa mwathirika.

Baadhi ya huduma za cPAC ambazo mwanamke anatakiwa kuzipata ndani ya muda mfupi tangu kuharibika kwa mimba au kutolewa ni kusafishwa kizazi (usafi wa kizazi), kupewa ushauri wa kisaikolojia, kupewa elimu ya afya ya uzazi, kukupewa dawa maalum, kupewa au kuongezewa maji, damu.

Pia anapokwenda hospitali hupata huduma ya kuchunguzwa Saratani ya Matiti, Kkchunguzwa magonjwa wa zinaa kama vile H.I.V au gono, kuchunguzwa magonjwa ya kuambukiza
Kupewa ushauri wa afya ya kizazi na saikolojia, huduma ya kuchunguzwa saratani ya shingo ya kizazi.

MIKAKATI YA SERIKALI

Serikali imeainisha mikakati na juhudi zinazofanywa katika kukabiliana na changamoto dhidi ya utoaji mimba usio salama.

Naibu Waziri wa Afya Dk Godwin Mollel anataja mikakati hiyo kuwa ni pamoja na kutoa elimu juu ya afya ya uzazi kwa watoto wa kike ambao wapo chini ya umri wa kuzaa.

Dk Mollel aliyasema bungeni Dodoma wakati akijibu swali la Mbunge wa viti maalumu Judith Kapinga.

Anasema kuwa Wizara kupitia vitengo vyake imeendelea kutoa elimu kwa klabu za vijana na vijana balehe kutojihusisha na ngono zembe ili kuepuka mimba zisizotarajiwa ambazo hupelekea kuongezeka vitendo vya utoaji mimba usio salama.

Katika swali lake, mbunge huyo alitaka kujua hatua zinazochukuliwa na serikali kukabiliana na utoaji mimba usio salama.

Akijibu swali hilo, Dk Mollel anasema Wizara inaendelea kusimamia utoaji wa huduma za uzazi wa mpango katika vituo vya huduma bila malipo ili kuwawezesha wanawake na wanaume kuzuia mimba zisizotarajiwa.

Naibu waziri huyo alitoa wito kwa jamii kuhakikisha mimba zote zinapatikana kwa mpango ili kuondokana na changamoto ya utoaji mimba usio salama unaoweza kuathiri afya za wajawazito.

Pia, aliwataka wajawazito kuhudhuria kliniki za uzazi wa mpango ili waweze kupatiwa elimu ya afya ya uzazi ikiwemo jinsi ya kuepukana na mimba zisizotarajiwa ili kuondokana na uavyaji wa mimba usio salama.

By Jamhuri