Na Stella Aron, JamhuriMedia

Katika kuhakikisha kuwa wananchi wana afya bora, Serikali imeendelea kushirikiana na wadau mbalimbali kutoa huduma za afya kwa kuzingatia sera na miongozo iliyopo.

Sera ambayo imeendelea kutumika katika kuelekeza utoaji wa huduma za afya ilipitishwa mwaka 1990. Tangu sera hiyo ilipopitishwa,yamekuwepo mabadiliko mbalimbali ya kiuchumi na kijamii, mabadiliko ya sayansi na teknolojia.

Mwaka 1996 marekebisho ya sera yalipitishwa kwa lengo la kuanzisha mfumo mpya wa utoaji na uendeshaji wa huduma za afya ambapo ushiriki wa sekta binafsi katika utoaji
wa afya ulitambuliwa na kupewa msukumo.

CCBRT imekuwa mstari wa mbele kuunga mkono juhudi za Serikali katika kuwainua na kuleta maendeleo katika sekta ya afya nchini.

Hospitali ya CCBRT imekuwa ikitibu magonjwa mbalimbali kama ulemavu wa mguu kifundo, mdomo wazi, fistula na mtindio wa ubongo, pia inatoa huduma zote za afya za kibingwa na kibobezi zikiwemo kusafisha figo (dialysis), meno, masikio, pua, koo, macho na miwani .

Pia magonjwa ya akina mama,matibabu ya wajawazito,mfumo wa uzazi,mifupa,kliniki za watoto, magojwa ya ndani, fiziotherapia na magonjwa ya ngozi.

Shirika la Afya Ulimwenguni (WHO), inakadiriwa kuwa asilimia 80 ya kuharibika kwa macho kunaweza kuzuilika au kutibika kwa matibabu, pamoja na yale yanayosababishwa na mtoto wa jicho, maambukizo, glaucoma, makosa yasiyosahihishwa ya kinzani, visa kadhaa vya upofu.

MTAALAMU WA KUTENGENEZA JICHO BANDIA NCHINI

Rehema Semindu ni mtaalamu wa kutengeneza jicho bandia katika Hospitali ya CCBRT jijini Dar es Salaam,anasema kuwa utengenezaji wa jicho bandia unapatikana katika Hospitali ya CCBRT peke yake hapa nchini.

“CCBRT ni kituo pekee kinachotengeneza jicho bandia hapa Tanzania, mchakato wa kutengeneza kila jicho moja huchukua masaa matatu.

“Natengeneza jicho kwa kuhakikisha linalingana mtumiaji wa jicho hilo, pia natumia vifaa mbalimbali kama nyuzi nyekundu kuonyesha mishipa midogo midogo ili kuhakikisha jicho hilo halina utofauti na macho ya kawaida,” anasema.

NAMNA YA KUTENGENEZA

Akizungumzia namna anavyofanyakazi na kutengeneza jicho bandia,anasema kuwa kwanza mgonjwa anatakiwa kupimwa jicho shimo la jicho ambalo limetolewa.

“Baada ya kujua kinachofuata ni kuanza uumbaji wa jicho bandia kwa kutumia unga maalumu,kemikali maalumu ya kutengenezea hicho pamoja na kutengeneza mishipa ya damu ambapo nazo kuna nyuzi maalumu.

“Kabla ya kuingiza kwenye mashine kwanza naangalia jicho hilo ambalo ni la plastiki kama linafana na lenzie kisha hulipeleka kwenye mashine kwa ajili ya uumbaji.

“Uumbaji mzuri wa jicho ni masaa manne hivyo kwa siku naweza kutengeneza macho mawili hadi matatu tu,” anasema Rehema.

Anongeza kuwa zamani kulikuwa hakuna utaratibu huo hivyo wagonjwa walikuwa wakiwekewa macho bila vipimo na kusababisha mwonekano wa sura mbaya ama kutisha.

Anasema kuwa baada ya kumaliza uumbaji wa jicho humpachika mgonjwa sehemu ambapo jicho limetolewa ambapo kwanza mgonjwa hujiangalia kwenye kioo na akifurahi ndipo huanza kupewa maelekezo.

UTUNZAJI JICHO BANDIA

Kwanza mgonjwa anatakiwa kulala nalo kila siku kwa wiki moja na kisha kulitoa kwa ajili ya kuliosha na kisha kulirudishia mwenyewe akiwa nyumbani.

“Kwanza kabla ya kumpachika jicho bandia kwanza tunampa maelekezo ya namna ya utunzaji na jinsi ya kulipachika mwenyewe mara baada ya kuliosha ambapo hutakiwa kurudia hospitali kwa miezi sita kama ni mtoto na mtu mzima anatakiwa kurudi hospitali baada ya mwaka mmoja.

“Anaporudi hospitali kazi yetu ni kuangalia maendeleo yake na kisha kulisafisha kwa mashine lakini pia tunaangalia je mgonjwa amenenepa au amepungua au yupo vilevile.

“Kama kuna mabadiliko ya kunenena au kupunguza ni lazima kutakuwa na mabadiliko pia kwenye jicho hivyo vyote tunaangalia upya na kufanyikazi tena,” anasema.

Rehema anasema kuwa mgonjwa akinenepa au kupungua yeye mwenyewe ataona mabadikiko kwenye jicho hivyo anaweza kurudi hispitali na kubadilishiwa kutokana na kero atakazokuwa akizipata.

Anaongeza kuwa manunuzi ya vifaa hufanyika nchini Uingereza ambapo CCBRT hulazimika kununua vifaa hivyo kwa mwaka mara moja na gharama zake huwa si chini ya Paund milioni 10.

WAGONJWA WA MACHO WENGI NI WANAUME

Anasema kuwa wagonjwa wengi anaopachikwa jicho bandia ni wanaume ambapo vyanzo vyao asilimia kubwa huwa ni ajali, kupigana, kwenye migodi, wachomeleaji.

“Kwa asilimia kubwa wagonjwa ninaowapokea ni wanaume kwa sababu wamekuwa wakipata changamoto kwenye vyanzo vingi vikiwemo hivyo hivyo hivyo nashauri wafanyakazi kujikinga kwa kuvaa vifaa vya kuzibia macho wakati wa kufanyakazi ili kuepuka macho kuharibika,” anasema.

USHAURI

Hospitali ya CCBRT imekuwa msaada mkubwa kwa wagonjwa wa namna hivyo ambapo gharama za utengenezaji jicho bandia ni sh.100,000 ambapo gharama nyingine hucgangiwa na wahisani hivyo anaishauri jamii kuacha kujinyanyapaa na kushindwa kushiriki shughuli mbalimbali za kijamii kwa kuhofia kuchekwa.

“CCBRT imekuwa mkombozi kwa jamii kwani kwa muda mrefu wenye matatizo kama hayo wamekuwa wakitwa majina mbalimbali kama chongo, Ngurumo, kwa mzee kijicho na mengi mengi lakini sasa ufumbuzi umepatikana na majina hayo hakuna” anasema.

Pia ameshauri jamii kuwasaidia watoto wenye saratani ambao hutakiwa kutolewa jicho kwa kuwapa msaada wa matibabu ili waweze kufurahia wanapokwenda shule ama kucheza na wenzao bila kunyanyapaliwa.

By Jamhuri