Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia

Madaktari bingwa wa Saratani watakiwa kutoa mapendekezo na mikakati ya namna bora ya wagonjwa kuzifikia huduma sambamba na kupunguza rufaa zinazo epukika kwenda nje ya nchi kupata matibabu.

Pia wametakiwa wataamu wa Saratani kujikita katika kufanya tafiti za kisayansi zitazowezesha nchi kuwa na teknolojia na ubunifu utakaosaidia utoaji wa huduma hususani za saratani.

Prof. Pascal Ruggajo ambaye ni Mkurugenzi wa Huduma za Tiba wa Wizara ya Afya, ametoa rai hiyo kwa niaba ya Waziri wa Afya katika Kongamano la pili la kisayansi la Magonjwa ya Saratani linalofanyika Jijini Dar es salaam.

Amefafanua kuwa tunahitaji sasa majibu ya changamoto zetu yatokane na sisi wenyewe “For Local Problems”, sisemi kuwa tuachane na matokeo ya tafiti zinazofanyika kwingineko Duniani.

“Takwimu zinaonyesha kwamba wagonjwa wapya wa saratani elfu 40 hugundulika kila mwaka huku vifo vinavyohusishwa na saratani vikifikia elfu 27 kila mwaka hivyo ni dhahili tunahitaji kutafakari kwa kina na kuweka mikakati ya pamoja kama taifa” ameeleza Prof. Ruggajo

Ameongeza kuwa wakati wa tatizo la UVIKO-19 kila taifa lilijaribu kutumia rasilimali za ndani kuokoa watu wake hivyo ni muda umefika sasa wa tupate majibu ya kisayansi yatakayowezesha kuunda nyenzo na matumizi ya dawa ikiwemo tiba asili za mwafrika ambazo zinaonyesha kutoa matumaini katika matibabu ya saratani.

Aidha Prof. Ruggajo ameagiza kuwa bodi za kujadili wagonjwa wa saratani “Tumor Board” ziimarishwe na maamuzi ya bodi hizo yaheshimiwe kwa kuwa matibabu ya Saratani yanahusisha kada zaidi ya moja

Kwa Upande wake rais wa chama cha Madaktari wa Saratani Tanzania (TOS) Dkt. Jerry Ndumbalo amesema kuwa mkutano wa pili wa wataalamu wa Saratani unalenga kuwaleta pamoja wataalamu mbalimbali wanaohusika kutibu saratani kutoka sehemu mbalimbali duniani ili kujadili jinsi ya kugundua saratani, kutibu kwa teknolojia mpya na kukinga.

“Mkutano huu umebeba kaulimbiu isemayo kuziba pengo katika utoaji wa huduma za saratani inayolenga kubainisha maeneo yenye upungufu katika utoaji wa huduma na kuyatafutia ufumbuzi” amesema Dkt. Ndumbalo

By Jamhuri