Na WAF – Tanga

Waziri wa Afya Ummy Mwalimu amewataka Watanzania kuacha matumizi holela ya dawa bila kufuata ushauri wa madaktari ili kuepuka usugu wa dawa dhidi ya vimelea ambapo husababisha dawa hizo kushindwa kuponya.

Waziri Ummy amesema hayo Mei 20, 2024 kwenye Semina ya kuwajengea uwezo wananchi wa Tanga Mjini kuhusu masuala ya Afya iliyofanyika katika Ukumbi wa Tanga Mji Mkoani Tanga.

“Tufuate ushauri wa Madaktari wanapo tuandikia na kutushauri dawa gani tunapaswa kutumia na kwa wakati gani ili kuepuka usugu wa dawa dhidi ya vimelea. amesema Waziri Ummy.

Aidha, Waziri Ummy amewakumbusha kina-mama wajawazito kuhudhuria kliniki mapema pindi wanapohisi kuwa na ujauzo ili kupunguza vifo vitokanavyo na uzazi.

Pia, Waziri Ummy amewasisitiza wajawazito kwenda kujifungulia katika vituo vya kutolea huduma za Afya ili kuepusha vifo vya watoto wachanga.

“Ili tuweze kupunguza vifo vya watoto wachanga lazima kuwa na matunzo kwa watoto wanaozaliwa na uzito upungufu kwakuwa kundi hili liko kwenye hatari zaidi ya kufa.” amesema Waziri Ummy.

Amesema, Serikali inaendelea kuweka mazingira rafiki ili kupatikana kwa huduma za watoto wachanga kutoka Hospitali 14 zilizokuwa na wodi maalum za watoto wachanga (NCU) mwaka 2018 hadi Hospitali 241 mwaka 2024.

Katika Semina hiyo pia kumetolewa mada mbalimbali zinazohusu masuala ya Afya ikiwemo mada ya elimu kuhusu mifumo ya Afya inavyofanya kazi kuanzia ngazi ya Taifa hadi kwenye Jamii.

Vilevile, wamejadili masuala ya Afya ya uzazi,mama na mtoto ambapo ushiriki wa wanaume katika afya y uzazi na wajibu wa jamii nzima katika kupunguza vifo vya watoto wachanga wanaozaliwa na uzito pungufu ilisisitizwa.      

By Jamhuri