Muungano wa kijeshi unaoongozwa na Saudi Arabia umeua raia 109 katika mashambulizi tofauti ya ndege katika kipindi cha siku 10, wakiwemo 54 katika soko lenye shughuli nyingi na 14 wa familia moja waliokuwa shambani.

Mratibu Mkaazi wa Umoja wa Mataifa nchini Yemen Jamie McGoldrick ameyaelezea mapigano yanayoendelea nchini humo kuwa yasiofaa na ya kuhuzunisha.

Ikitaja ripoti za awali kutoka ofisi ya haki za binadamu ya Umoja wa Mataifa, taarifa ya Mcgoldrick imesema mashambulizi hayo ya ndege yalililenga soko lenye watu wengi katika wilaya ndogo ya Al Hayma katika mkoa wa Taiz siku ya Jumanne, na kuuwa watu 54 na kuwajeruhi 32.

Katika siku hiyo hiyo, shambulizi la ndege kwenye shamba lililopo wilaya ya Attohayta katika mkoa wa Hodeidah liliuwa watu 14, na mashambulizi ya ndege kwingineko yakauwa raia wengine 41 na kuwajeruhi 43 katika kipindi cha siku 10.

Chini ya sheria ya kimataifa, pande zinazohasimiana laazima ziwaachilie raia pamoja na miundombinu ya kiraia. Umoja wa Mataifa hauna makaridio ya karibuni zaidi kuhusu idadi ya vifo nchini Yemen, baada ya kusema Agosti 2016, kwamba kwa mujibu wa vituo vya afya watu wasiopungua 10,000 wameuawa.

Umoja wa Mataifa unasema mgogoro wa Yemen ndiyo mbaya zaidi wa kibinadamu, ambapo watu wapatao milioni nane wako katika hatari ya kukubw ana janga la njaa, mripuko wa ugonjwa wa kipindupindu uliowaathiri watu milioni moja, na mporomoko wa uchumi katika nchi ambayo tayari ilikuwa moja ya mataifa maskini zaidi katika ulimwengu wa Kiarabu

Please follow and like us:
Pin Share