Serikali ya Zimbabwe imeeleza kuwa itampa aliyekuwa Rais wa nchi hiyo. Robert Mugabe nyumba ya kuishi, magari pamoja na ndege binafsi ya kusafiria ikiwa ni sehemu ya stahiki wanazopatiwa watumishi wa serikali waliostaafu.
Pamoja na hayo, pia atapewa watumishi 20, wakiwemo walinzi wake 6 watakaokuwa wanalipwa na serikali ya nchi hiyo, kwa mujibu wa gazeti la serikali la Herald.
Rais Mugabe mwenye umri wa miaka 93, aliyejiuzulu nafasi yake ya urais nchini Zimbabwe, ndiye kiongozi wa kwanza kutajwa kunufaika na mikakati hiyo mipya iliyotangazwa na Rais Emmerson Mnangagwa.
hakuna tarifa zilizotolewa kuhusu malipo, lakini katiba ya nchi hiyo inataja kuwa Rais Mstaafu atalipwa pensheni ambayo ni sawa na mshahara wa Rais aliyepo madarakani kwa wakati huo.
Mwezi uliopita, chombo kimoja cha habari nchini Zimbabwe kiliripoti kuwa Mugabe aliahidiwa fedha kiasi cha dola za kimarekani 10 milioni 9sawa na shilingi za kitanzania 22.3 bilioni) kama nyongeza ya kustaafu ikiwa ni moja ya vitu alivyoahidiwa ili ajiuzulu. Serikali ya Zimbabwe ilipinga vikali madai haya.
Kama sehemu ya stahiki zake, Rais Mugabe atapewa gari aina ya Mercedes Benz s500 pamoja na mengine mawili ambayo yatakuwa yakibadilishwa kila baada ya miaka mitano.
Mugabe na mkewe Grace watapewa pasi za kusafiria za kidiplomasia ambazo zitawaruhusu kusafiri safari nne za ndege au treni katika daraja la kwanza (first class) na safari nne za nje ya nchi kwa kutumia ndege binafsi.
Vilevile atapewa nyumba iliyokamilika katika eneo lolote atakalotaka ndani ya Mji Mkuu Harare. Nyumba hiyo italipiwa gharama zote na serikali.
Pia, atapata bima ya Afya yeye pamoja na mkewe na wengine wanaomtegemea.

Please follow and like us:
Pin Share