Mratibu Ofisi ya CPT Taifa, Mariam Kessy, kwenye kongamano la kumbukizi ya miaka 20 ya kifo cha Mwalimu Nyerere aliwasilisha mada kuhusu familia. Yafuatayo ni baadhi ya yale aliyozungumza. 

Familia kama msingi wa taifa na jamii, kila mmoja anakotoka na anakoishi ni vizuri kuzungumzia familia. Kila tunachofanya lazima kilenge familia.

Tunaposema taifa letu ni maskini, maadili katika taifa letu yameporomoka,  – tunazungumzia familia zinazounda jamii au taifa letu.

Maendeleo hatupaswi kuyatazama katika vitu tu na kusahau mambo mengine. Mtazamo au falsafa ya Mwalimu Nyerere aliyojifunza kutoka familia halisi alimoishi – familia ya Kiafrika, utamaduni na mifumo yake ndivyo vilivyomwongoza kuweka dira ya kulijenga taifa hili katika misingi iliyosimikwa juu ya tunu za upendo, umoja na mshikamano.

Maisha halisi ya familia ndiyo yaliyompa mwanga katika kuweka dira hii. Dira hiyo ilimsaidia pia katika kuliunganisha taifa letu lenye makabila mengi na lenye dini tofauti tofauti. Ni jambo ambalo alilipigania sana na mpaka leo tunajivunia na tunatakiwa kumuenzi. Maisha ya Mwalimu Nyerere ndani ya familia ndiyo msingi uliomwongoza kuzijali familia katika kutengeneza sera. Alipigania sana huduma za jamii kwa wote. Haya yote alilenga kuijali familia.

Kutoka katika mafundisho ya kidini na historia yetu ya wanadamu na historia yetu ya Tanzania, familia huanzishwa kwa ndoa na sheria za nchi zinatambua hilo na kuweka taratibu za ufungaji ndoa; na kuweka aina ya ndoa – ndoa ya wake wengi na ndoa ya mke mmoja.

Pia tunazo aina mbili za familia – familia ndogo ya mke, mume na watoto; na familia pana inayohusisha ndugu wengi.

Familia inatambulika kama ndiyo taasisi muhimu ya kijamii na kitovu cha shughuli za kijamii. Ni kitengo cha jamii kinachoundwa na nasaba ya wazazi na watoto; au ndugu wenye nasaba.

Familia bora huwa kitovu cha maendeleo, furaha na kwa jumla ustawi wa maisha; familia ni mahali ambako watoto hujifunza umoja na upendo miongoni mwao.

Familia zina wajibu wa kuhakikisha ziko salama, zina afya njema, elimu, zinahudumia wazee, zinaimarika kiroho na zinakuwa na upendo.

Familia yenye umoja inakuwa na upendo wa Mungu, na ni alama ya Utatu Mtakatifu; na kwa hakika upendo wa Mungu kwa ubinadamu huonekana.

Ingawa dhana ya familia inaweza kuonekana kuwa rahisi, matendo ya binadamu yameifanya kuwa ngumu zaidi.

Suala la familia linapewa kipaumbele. Kuna Siku ya Familia Duniani (Mei 15) na Kanisa pia lina Siku ya Familia. Familia si jambo dogo, bali ni jambo linalostahili kuheshimiwa na jamii na watu duniani kote.

Familia ni msingi, ndipo mtu huzaliwa, hutunzwa, hulelewa na kufundishwa tunu za kimaadili na kiroho ambazo ndiyo msingi wa maisha ya mtu. Kama mtu ana msingi imara kimaadili na kiroho atafaulu mambo mengi maishani mwake. Lakini kama anakosa tunu hizi pengine hata akiwa na kisomo kiasi gani anaweza asifanikiwe.

Sisi kama wazazi tunaelewa maana ya familia na majukumu yake ambayo ni dhamana kubwa sana ambayo tumekabidhiwa na Mwenyezi Mungu. Hii ni dhamana inayotuongoza katika kujenga mustakabali mzima wa jamii na taifa.

Kutimiza majukumu ya familia ni lazima wote kushirikiana bila kumwachia mdau mmoja peke yake. Tunapojibidisha kujenga familia imara tunakuwa tunajenga taifa bora, tunajenga jamii bora; na kinyume chake ni hasara kwetu wenyewe. Ikiwa tutakuwa na familia dhaifu, familia maskini, familia isiyokuwa na maadili, tutapata madhara mengi.

Changamoto katika familia: Mabadiliko ya sasa ya maisha yasitufanye tuache mambo mema ya asili. Katika nyakati hizi kuna miundo tofauti ya familia.

Siku hizi kuna familia za aina tofauti. Kuna familia zinazohusisha familia iliyotokana na ndoa ya mke na mume; familia inayohusisha wana ndugu kama babu na bibi, shangazi, wajomba, binamu na kadhalika; familia za watu wazima watatu au zaidi pamoja na watoto. Familia za namna hii hutokana na talaka, au pia ndoa za mitala.

Aina nyingine ya familia ni ile ya waliotalakiana kuolewa sehemu nyingine na hivyo kukuta wakijumuisha pamoja watoto waliotokana na ndoa nyingine za awali. Hawa wanapokuwa pamoja huunda familia mpya. Aina nyingine ni familia zilizotokana na kuasili watoto, hivyo kuwa ni wanafamilia kisheria.

Familia nyingine hujumuisha watu wazima wanaokuwa walezi kwa mtoto au watoto ambao si wa kuwazaa.

Kimsingi, familia huundwa na ndoa ambayo wanaooana, kwa hiari yao hukubaliana kuishi pamoja.

Sheria ya Ndoa ya mwaka 1971 inatambua aina mbili za ndoa: ndoa ya mke mmoja na ndoa ya mitala (wake wengi). Inatambua na kuruhusu aina tatu za kufunga ndoa ambazo ni ndoa za asili (kienyeji), ndoa kwa imani za kidini na ndoa zinazofungwa kwa utaratibu wa kiserikali.

Hata hivyo, changamoto zinazosababishwa na mfumo wa kisasa wa maisha zinafanya familia kuwa kitu muhimu zaidi.

Kuna faida nyingi zinazotokana na familia imara. Miongoni mwa faida hizo ni kuwa na uhakika wa mahitaji muhimu kama ya chakula, maji, malazi na mavazi. Familia iliyo imara kimaadili watoto wake huishi vizuri na hupata huduma kama elimu kwa namna iliyo nzuri.

3030 Total Views 2 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!