Ulemavu wa fikra umejificha. Wakati mwingine ni vigumu kuutambua au kwa vile ulemavu huu una nguvu na unaweza kutupumbaza wote, ni jambo ambalo linachukua tafakuri na kujiuliza maswali yasiyokuwa na majibu. Mfano, sisi Waafrika kuwa na majina ya Kizungu na Kiarabu au sisi Waafrika kutukuza vizazi vya nchi za nje kuliko kutukuza vizazi vya babu zetu. Au kutukuza na kujivunia lugha za kigeni zaidi ya lugha zetu sisi. Kiongozi wa serikali kujigamba na kutamba kumiliki magari ya kifahari badala ya kutangaza jitihada zake za kuchangia maendeleo ya watu wake.

Ulemavu wa fikra, uwe wazi au ujifiche kwa kiasi fulani, ni kizingiti cha maendeleo ya binadamu. Sote tunajua pasipo shaka kwamba ili tupate maendeleo ni muhimu kabisa kupambana na ulemavu wa fikra. Ingawa kuna vitu vingi vya kuzingatia katika maendeleo ya taifa lolote duniani, kuna mambo ambayo ni muhimu sana na hayaepukiki. Mambo haya ni elimu, siasa, vijana na uchumi. Nchi ambazo zimezingatia mambo haya na kuyashughulikia kwa umakini mkubwa, zimepiga hatua kubwa ya maendeleo. Na zile zilizopuuza, ziko nyuma kimaendeleo.

Kwa kifupi, huu ndiyo mchakato wa kupambana na ulemavu wa fikra. Elimu ni mkombozi wa ulemavu wa fikra. Na si elimu tu, bali elimu bora. Elimu ambayo imefundishwa kwa kutumia lugha yetu na kuelezea mazingira yetu ya siku kwa siku.

Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inasema hivi kuhusu elimu: “Serikali itafanya jitihada kuhakikisha kwamba watu wote wanapata fursa sawa ya kutosha kuwawezesha kupata elimu na mafunzo ya ufundi ngazi zote za shule na vyuo vingine vya mafunzo.” (Katiba, ibara ya 11(3) ).

Serikali iliyo madarakani na zile zilizopita zimejitahidi kiasi fulani kufuata katiba kuhusu elimu. Tatizo linalojitokeza ni mfumo na ubora wa elimu inayotolewa. Baada ya uhuru elimu iliendelea kutolewa kwa kufuata mfumo wa kikoloni. Wakati wa ukoloni watu walielimishwa kuwatumikia wakoloni. Ilikuwa inaandaliwa nguvu kazi. Hawakuwa na haja ya kuandaa watafiti, wagunduzi na watu wa kuliendeleza taifa letu. Mitaala iliyotengenezwa ilikuwa ikilenga kumfundisha mtu katika mtindo wa kukariri tu. Au kufanya kazi kama roboti.

Ili taifa liendelee, linahitaji wavumbuzi, watafiti, watu wenye fikra pevu ambao wanazama kwenye fikra na kuchambua mambo mbalimbali. Taifa linahitaji wanafalsafa, wenye kuleta mawazo mapya na kuyachambua kwenye jamii. Na wafanye hivyo kwa uhuru na kwa kujiamini, wafanye hivyo bila shinikizo au mahaba ya chama chochote cha siasa. Wawe huru kufikiri bila kushinikizwa na mtu yeyote au taasisi yoyote yenye madaraka  au nguvu za fedha.

Ni bahati mbaya kwamba mpaka leo hii mitaala yetu yote bado ni kama ile ya wakati wa wakoloni! Mfumo bado ni ule ule wa kumfundisha mtu kukariri. Kinachohitajika kwa sasa hivi ni kutengeneza mitaala mipya ambayo italenga katika kutoa elimu ya kumkomboa mtu kifikra, mtu akawa na uwezo wa kuhoji na kufanya utafiti hadi kuelekea uvumbuzi wa vitu mbalimbali na kuchangia kukua haraka kwa uchumi na maendeleo ya taifa letu la Tanzania.

Tunahitaji mfumo wa elimu utakaowaandaa vijana kuwa wanasiasa bora, ambao badala ya kuvitanguliza vyama vyao ya saisa, wanalitanguliza taifa lao. Vijana ambao watashiriki kutengeneza sera za vyama vyao zenye kulenga kuleta maendeleo  ya taifa zima.

Siasa za kujenga uzalendo na mshikamano wa taifa zima. Vijana ni kiungo muhimu cha kizazi na kizazi, ili taifa liendelee na kustawi, ni muhimu liwe na kiungo kizuri kati ya  kizazi na kizazi. Kiungo hiki ni vijana wetu, ambao bila kuwaandaa vizuri, bila kuwapatia elimu ya kuwakomboa na kuwapatia fikra pevu, tutaacha nyuma yetu taifa ambalo liko hoi bin taabani.

Kutokana na mabadiliko ya kisayansi na kiteknolojia yanayojitokeza hivi sasa, kijana ndiye mwenye nafasi kubwa ya kujifunza na kuweza kuonyesha ujuzi wake katika taifa, hivyo kuleta maendeleo nchini na uvumbuzi katika nyanja mbali mbali. Mambo ya kujiuliza ni kwamba, je, kijana huyu ana nafasi gani ya kupata ujuzi, kuuendeleza na kuutumia? Mitaala yetu ya shule za msingi na sekondari inasaidiaje kumwandaa kijana kupambana na hali ya sasa hivi?

Tunapomsikia kiongozi kijana akibeza aina fulani ya magari na kuyaita ya wanyonge, wakati serikali anayoitumikia inajinadi kuwa ni serikali ya wanyonge, inatia shaka juu ya elimu yetu. Inawezekana vipi kiongozi wa wanyonge akabeza maisha ya wanyonge?

Kiongozi wa wanyonge, anashabikia magari ya kifahari ambayo kwa vyovyote vile yanahitaji fedha nyingi za kigeni, fedha ambazo zingeweza kujenga shule, hospitali na barabara? Katika hali ambayo kila kiongozi anatangaza umaskini wa  taifa letu, wakati ambao kila kiongozi analalamikia bajeti ndogo ya kuiendesha serikali, inawezakana kweli, kiongozi akabeza usafiri ambao unatumia mafuta kidogo? Usafiri ambao bei yake si kubwa sana?

Huyu ni kiongozi msaliti au ni kiongozi aliyeteleza. Na je, kiongozi msaliti hana dawa yake? Au kiongozi aliyeteleza hana dawa yake? Mtu anayejitambua akiteleza anafanya nini? Mtu anayejitambua akijiingiza kwenye usaliti anafanya nini? Kuwajibika ni somo ambalo liko kwenye mfumo wa elimu yetu? Hayo yote ni muhimu katika kujenga taifa imara na lenye maendeleo. Huwezi kuhubiri kunywa maji wakati wewe unakunywa mvinyo. Na ndege wa bawa moja huruka pamoja.

Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda, anasema kwamba gari la IST ni gari la wanyonge. Je, yeye ni kiongozi wa watu gani? Ni Watanzania wangapi wanaweza kununua hilo gari la wanyonge? Kipato cha Mtanzania kimesimama wapi? Kiongozi na kwa maana hii mkuu wa mkoa ambaye amekuwa akijitambulisha kama mtetezi wa wanyonge ni lazima alifahamu hili. Haiwezekani Watanzania kwa uchumi wa leo wakanunua magari ya kifahari kama anavyofikiri. Na yeye kwa mshahara wake wa serikali ya wanyonge hawezi kuwa na gari la kifahari. Akiwa nalo, ni lazima ahojiwe. Na la msingi hapa ni kusisitiza umuhimu wa elimu kama mkombozi wa fikra.

Kuna hatari kubwa ya kuwa na taifa dhaifu lenye hali mbaya katika nyanja zote; yaani kiuchumi, kisiasa na kijamii endapo kijana wa sasa hakuandaliwa ipasavyo kushika nafasi za kusimamia masuala hayo. Aidha, kijana huyu anapaswa kuandaliwa kwa kupewa elimu bora itakayombadilisha fikra na mtazamo wake kimaisha ili kumwezesha kupambana na changamoto muhimu za kimaisha kikanda na kidunia. Haya yote yanafanikiwa endapo tu kijana ataandaliwa kupata elimu.

Ili kuboresha uchumi wetu, kuna haja kubwa ya kuiboresha kwanza elimu yetu na kuwaandaa vijana wetu waweze kuukabili ulimwengu huu unaobadilika kila siku ya Mungu. Jambo hili linahitaji msimamo wa kitaifa. Ni lazima liwe jambo ambalo litaheshimiwa na wanasiasa wote. Vyama vyote vinavyotengeneza sera na kujiandaa kuingia madarakani ni lazima vizingatie kitu hiki. Bila elimu bora, bila kuwaandaa vijana vizuri ni vigumu kujikwamua kiuchumi na ni vigumu kujikwamua kifikra. Elimu ipewe kipaumbele na yeyote aliye na nia njema na taifa letu la Tanzania.

By Jamhuri