Umri usiwe kikwazo cha kutimiza ndoto

 

Kuwa na umri fulani si kigezo kuwa huwezi kutimiza ndoto zako. Umri ni namba tu.

Bila kujali kama wewe ni mzee au mdogo kiasi gani, bado unaweza kutimiza ndoto zako. Bado unayo nafasi ya kufanya mambo makubwa. Umri usiwe kikwazo cha wewe kutotimiza ndoto zako.

Kuna watu wakianza kufikiria kuanza kutimiza ndoto zao wanaona bado ni wadogo na wanaona hawawezi kufanya chochote kutimiza ndoto zao.

Kuna wengine wakiona wamefikia umri fulani tayari wanaona kufanya mambo fulani ili watimize ndoto zao haiwezekani. Mpendwa msomaji, umri kuwa kikwazo cha kutotimiza ndoto zako ni suala zima la fikra.

Ukianza kufikiria kuwa jambo fulani haliwezekani, akili inakubali kutowezekana na mwili unakuwa hauna nguvu sana pale akili inapotumika inabidi utii tu.

“Ukifikiri unaweza, hauwezi, upo sahihi,” alisema Henry Ford. Maisha yako ya leo yanatokana na jinsi ulivyowahi kufikiri na unavyofikiri. Ukibadili namna yako ya kufikiri, utabadili maisha yako.

Tukimtazama Yusufu aliyebeba kichwa cha “Nina Ndoto”. Huyu alianza kuwa na ndoto toka akiwa na umri wa miaka 17. Huu ni umri ambao vijana wengi wanaona bado hauruhusu kuanza kutimiza ndoto zao.

Aliyeweka mfumo wa watu kutoanza kufuata ndoto zao wakiwa bado wanasoma sijui ni nani.

Ukiwauliza vijana wengi swali hili, “Utaanza kutimiza ndoto zako lini?” Wengi watakwambia, “Nikimaliza masomo yangu.”

Sikia rafiki yangu, ndoto haziangalii unasoma au una umri gani. Katika umri wowote unaweza kufanya jambo lolote kubwa.

Nikukumbushe kitu, facebook ilianza kutengenezwa katika chumba cha bweni la Chuo Cha Harvard alimokuwa akilala Mark Zuckerberg. Huyu alikuwa na umri wa miaka 19 alipoanzisha facebook.Leo hii kama facebook ingekuwa nchi, ingekuwa nchi ya kwanza duniani kwa kuwa na idadi ya watu wengi. Facebook inawatumiaji  bilioni 2.38 kwa mwezi, wakati nchi ya China yenye watu wengi inakadiriwa kuwa na watu bilioni 1.4

Nafikiri unaweza kuona jinsi watu wenye ndoto wanavyofanya mambo makubwa.

Bado unasema wewe ni mdogo? Unamfahamu Ryan Kaji? Ryan ni mtoto mwenye miaka 7, ambaye anamiliki chaneli ya Youtube yenye watazamaji zaidi ya milioni 19 inayoitwa ‘Ryan ToysReview’ ambayo ni chaneli ya watoto.

Katika chaneli hiyo, video mbalimbali huwekwa kila siku zikimuonesha mtoto huyo akicheza na wanasesere mbalimbali.

Kutokana na chaneli hiyo kupendwa sana na watoto wengi duniani, imekuwa ikimlipa mtoto huyo dola milioni 11 za Marekani kwa mwaka kutokana na matangazo ambayo huwekwa.

“Kama hutatui matatizo, basi wewe ni tatizo,” anasema mchungaji Sunday Adelaja. Alina Morse hakupenda kuwa tatizo, bali ni mtatuzi wa matatizo. Mtoto huyo akiwa na miaka 7 aligundua kwamba pipi huchangia sana kuharibu meno ya watoto wengi. Baada ya kuona hivyo alitengeneza pipi ambazo husafisha meno. Biashara hiyo imeweza kukua na kuwa na thamani ya dola milioni 2 za Marekani; miaka 6 baada ya kuanzishwa.

Siku moja nilikutana na Hadija Jabiry ambaye ni mwanzilishi na mkurugenzi wa kampuni ya GBRI inayojihusisha na kuuza matunda na mbogamboga nje ya nchi. Hadija ameajiri Vijana zaidi ya 200 katika shughuli zake, akiwa chini ya miaka 30. Ni Mtanzania anayefanya mambo makubwa.

Hadija alianza  ujasiriamali tangu akiwa anasoma Chuo Kikuu cha SAUT, Mwanza. Siku hiyo nilimuuliza, “Uliwezaje kumudu masomo ya darasani na mambo ya nje?”

Alinijibu hivi, “Kama huna hela utaweza, ukiona mtu anasema siwezi kufanya jambo fulani jua ana pesa.”

Kwa msingi huo naungana na Hadija nikisema kama unasema huwezi kutimiza ndoto zako jua kwamba umeridhika na hali ya maisha uliyonayo.

Kuna watu pia katika umri wa uzee wamefanya mambo makubwa. Harry Bernstein akiwa na umri wa miaka 96 aliandika kitabu chake cha kwanza kiitwacho ‘The invisible wall’ na baadaye aliandika vingine viwili. Anasema, “Miaka ya 90 ilikuwa miaka niliyofanya mambo makubwa.”

Je, bado umri ni kikwazo cha kutimiza ndoto zako?

Mandela alikuwa rais akiwa na miaka 70. Colonel Sanders alianzisha KFC akiwa na miaka 65 nabado ikawa biashara kubwa duniani.

1510 Total Views 2 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!