Wiki iliyopita niliandika makala yenye kichwa “Imani yako inaakisi fedha zako.” Kama ilivyo ada nimepokea mirejesho mingi kwa barua pepe, simu za miito na ujumbe mfupi. Wasomaji wamekuwa na mitazamo tofauti – wengine wakinipongeza na wengine wakionesha dukuduku.

Pia wapo  wachache wamepinga uthubutu wangu wa kuchambua fedha katika sura wanayodai nahamasisha watu kutafuta fedha. Bila shaka hawa ni wale wanaoamini “fedha si nzuri kwa sababu inaharibu tabia za watu.”

 

Nilivutiwa sana na mchango wa msomaji mmoja kutoka Arusha aliyeniandikia barua pepe ifuatayo:

 

“Bw. Sanga nakupongeza sana kwa makala zako. Unaandika ujasiriamali na mambo ya kujitambua in a unique style kiasi kwamba kila ninaposoma makala zako napata ladha na impact kubwa mno. Kwenye makala yako ya leo umeeleza vizuri mno kuhusu imani za fedha.

 

“Loo! Makala hii imenisaidia na kuniokoa mno kwa sababu nimekuwa na kawaida ya kushiriki gossiping kuhusu wenye fedha. Mfano hili la kuamini kuwa kuna makabila yanafanikiwa kwa sababu ya wizi ama ushirikina nimekuwa ninaamini pasipo kujua kuwa ninaathiriwa na imani hizo.”

 

“Hata hivyo Bw. Sanga ninaomba unisaidie nawezaje kuzalisha fedha za kunitosha? Kwa sababu mimi ni mwajiriwa lakini kadiri siku zinavyoenda ninaona majukumu yanaongezeka na mshahara naona hautatui mahitaji yangu vizuri, maisha ni magumu, nikitafiti naona biashara karibia zote zimeshafanyika. Je, nitafanya kitu gani ama namna gani ili niweze kuzalisha fedha? Narudia tena kukupongeza na ninaamini utanisaidia katika hili.” Mwisho wa kunukuu.

 

Katika makala haya leo ninajibu swali la msomaji huyu aliyeniuliza, “Nawezaje kuzalisha fedha za kunitosha?” Hata hivyo, kabla sijaeleza namna gani mtu unaweza kuzalisha fedha za kukutosha, ninapenda kueleza kidogo kuhusu dukuduku walilokuwa nalo baadhi ya wasomaji kuwa fedha si nzuri kwa sababu zinaharibu tabia za watu.

 

Kimsingi fedha imebeba chembechembe nyingi za kisaikolojia zenye uwezo mkubwa wa kuamsha tabia za mtu hata zile ambazo hazijapata kuonekana. Mtu mchoyo akipata fedha uchoyo wake unaongezeka na unakuwa dhahiri. Mtu mwema na mtoaji akipata fedha wema wake huongezeka na ataonekana akitoa zaidi na zaidi.

 

Kwa jinsi hii tunaona kuwa kimsingi fedha haibadilishi wala kutengeneza tabia ya mtu, isipokuwa fedha hudhihirisha tabia na hulka aliyonayo mtu ambayo alishakuwa nayo hata kabla hajapata fedha. Naweza kuifananisha fedha na mfumo wa mashine za sauti “amplifier”.

 

Kwenye “amplifier” ukitoa sauti yako kama ni sauti mbaya, ubaya huo utakuzwa na kama sauti yako ni nzuri basi uzuri wa sauti hiyo utakuzwa vile vile. Kwa kuwa fedha zina mfumo wa kukuza tabia, ni vema mtu akatumia muda na rasirimali maarifa kujenga tabia na hulka zake ili fedha zinapokuja zisilete mushkeli.

 

Ninapotaja habari ya mtu kuwa na fedha isidhaniwe kuwa ninagusia fedha nyingi sana, la hasha! Watu tunatofautiana linapokuja suala la mitazamo na hulka zetu katika fedha. Wapo watu ambao wakiwa na shilingi elfu kumi tu mfukoni lazima ujue kwa maana wataleta vurugu na maujiko kibao.

 

Mtu mwingine akiwa na kiasi hicho cha fedha haoni kama ana fedha, isipokuwa anaweza hata kukueleza kwamba hana fedha kabisa. Kwa mwingine shilingi milioni moja si fedha wakati kwa mwingine kiasi hicho tu ni utajiri!

 

Kinachofanya mtu mmoja aone kuwa shilingi elfu kumi ni fedha na mwingine aone kama si fedha ni kutokana na mtazamo wanaokuwa nao watu hawa katika fedha. Mtazamo huu hauanzi pale mtu anapoishika hiyo elfu kumi, isipokuwa ni kuwa mtazamo wao ulishajengeka mapema kabla hata ya kushika hiyo fedha.

 

Hebu sasa nigeukie upande mwingine kulijibu swali la msomaji yule, “Je, nawezaje kuzalisha fedha?” Kwa wale wenye kumbukumbu bila shaka wangali wanaikumbuka makala niliyopata kuandika wiki chache zilizopita yaliyokuwa na kichwa, “Tumeamua kuichuuza thamani ya fedha yetu.”

 

Katika makala hayo nilieleza kwa kina dhana na maana ya fedha, lakini pia nilisema fedha si mafanikio zikisimama peke yake; isipokuwa fedha ni matokeo ya mtu kufanikiwa. Fedha inatakiwa kumjia mtu baada ya kuzalisha thamani fulani katika uchumi. Hapa tunaangalia maeneo kadhaa zinakopatikana fedha.

 

Kunapotokea mdororo wa uchumi, mara nyingi mitaani huwa tunasema fedha zimepotea, fedha hazionekani! Kitu cha kujiuliza ni “Je, fedha zinapopotea ama kutoonekana zinakuwa zimepotelea wapi?” Ukweli ni kuwa fedha zote zilizopo duniani zinazunguka miongoni mwa watu. Idadi ya fedha huwa haipungui, ila kinachopungua ama kuongezeka ni thamani ya fedha.

 

Ukiwa na fedha leo na kesho ukawa huna basi ujue fedha zipo kwa watu wengine. Kwa maana hii ukitaka kupata fedha lazima uzitafute kutoka kwa watu.  Fedha zinapatikana kwa watu. Je, unazipataje fedha kutoka kwa watu?

 

Watu katika maisha ya kila siku wanakabiliwa na changamoto na matatizo mbalimbali. Unapochukua wasaa wa kutatua changamoto na matatizo yao lazima utapokea ujira wa utatuzi wako. Hii ina maana kuwa wakati wote ikiwa unahitaji fedha lazima uwe mtu unayetazama matatizo na changamoto kama fursa za kukusaidia kupata fedha.

 

Tunaposikia kuwa Tanzania inakabiliwa na tatizo kubwa la ajira; kuna makundi mawili ya watu yanayolitazama hili kwa mitazamo tofauti. Mosi, wapo wanaosimama upande wa kulalamika na wakitazamia kuhurumiwa. Ni vema wasomaji mkafahamu siri hii: Kihisia, fedha ni kama ina masikio, haitaki malalamiko, haitaki manung’uniko!

Ukizoea kulalamika na kunung’unika ovyo unaifukuza fedha! Lakini ukichunguza upande wa hawa walalamishi na wanung’unikaji sana; utagundua kuwa wengi wao huamini kuwa kushindwa kwao ikiwamo kiuchumi (kifedha) ni matokeo ya uzembe ama kutokuwajibika kwa wengine.

 

Kundi la pili ni wale wanaofikiri namna ya kuikabili na kuitatua changamoto hii. Ndani ya kundi hili la pili ndimo wanakopatikana wale wanaoamua kujiajiri, lakini ninaowakusudia zaidi hapa ni wale wanaowasaidia wengine kujiajiri. Hawa ni kundi la watu wanaoamua kufanikiwa katikati ya matatizo na changamoto.

 

Ndiyo maana ukichunguza kwa umakini utabaini kuwa watu wanaofanikiwa katika maeneo mbalimbali (ikiwamo kifedha) huwa wako “bize” na mambo yao, hawana muda wa kulalamika wala kunung’unika ovyo. Wanaofanikiwa mara zote huwa hawawanyooshei vidole watu wengine kutokana na kushindwa kwao. Wanaofanikiwa huamini kuwa wanawajibika kwa sehemu kubwa katika mafanikio yao.

 

Kwa kuwasaidia wengine kuweza kujiajiri kundi hili hufanikiwa kujipatia fedha. Unapotatua changamoto ama tatizo lolote kiubunifu lazima unufaike.

 

Tunatakiwa tufahamu kuwa matajiri wote duniani wameupata utajiri wao kwa kutatua changamoto na matatizo waliyoyabaini miongoni mwa watu. Fedha zinapatikana kwenye matatizo na changamoto.

 

Tunapoangalia kuwa fedha zinapatikana kwa kutatua changamoto na matatizo tunajiuliza, “Je, unawezaje kutatua hayo matatizo na changamoto?” Jibu lipo hivi: Ili kutatua tatizo ama changamoto lazima ubuni bidhaa na huduma zinazojibu matatizo na changamoto hizo.

 

Watu walipoonekana wanatembea peku na kuhatarisha afya zako, alitokea mtu akabuni viatu. Mpaka leo tunawalipa wanaotengeneza viatu. Baada ya kuona watu wanahitaji kusafiri kwa haraka na kwa ufanisi, walitokea waliogundua ndege na hadi leo tunawalipa watu mbalimbali wanaofanikisha usafiri huo kila tunapotaka kuutumia.

 

Kila bidhaa unayonunua ama huduma unayolipia unatakiwa kutambua kuwa ni matokeo ya ubunifu wa wajasiriamali uliochagizwa na changamoto na matatizo waliyaona miongoni mwa watu.

 

Wapo wajasiriamali mbalimbali ambao wamechangamkia fursa zilizotokana na ukosefu wa ajira na sasa wameanzisha kampuni zinazotoa huduma za kiushauri na kimafunzo kuwawezesha watu kujiajiri. Hivyo, tunaona kuwa eneo jingine ambako fedha zinakaa ni katika bidhaa na huduma.

 

Njia rahisi ya kubuni bidhaa na huduma zitakazowavutia wengine kukuletea fedha ni kutumia karama na vipaji vyako. Kama wewe ni mwimbaji, ukiimba nyimbo nzuri moja kwa moja utauza nakala na utatumbuiza katika matamasha. Kama wewe ni daktari mwenye uwezo na kipaji kikubwa cha kutibu kwa ustadi, lazima watu watakuja kupata huduma na kukuletea fedha. Ndani ya karama na vipaji ndiko zinakopatikana fedha.

 

Kitu ambacho tunatakiwa kuepukana nacho ni mawazo ya kupata fedha za mkato-mkato. Shida ya fedha za mkato-mkato kama ufisadi, wizi, utapeli, udokozi na uhujumu si tu hatari ya kukamatwa na kufungwa jela, isipokuwa zipo hatari kubwa zaidi ya hapo ambazo ndizo ambazo mimi daima huzitambulisha.

 

Ukifanya ufisadi kazini na ukajipatia fedha kisha ukajenga majumba na kuanzisha miradi lukuki, hata usipokamatwa usidhani upo salama! Kuna kitu kinaitwa hukumu ya moyoni (spiritual condemnation) ambacho kinaweza kukutesa sana. Spiritual Condemnation ni hatia anayokuwa nayo mtu kwa ndani kutokana na njia alizotumia kupata fedha zake.

 

Hili la madhara ya kutafuta  fedha na mafanikio kwa njia zisizo halali linahitaji makala ya peke yake. Hata hivyo, kitu cha kufahamu na kuamini ni kuwa inawezekana kupata fedha na utajiri kwa njia halali; huna sababu kupita njia za mikato zitakazokutesa unapofanikiwa.

 

Nihitimishe kwa kusema kuwa inawezekana na tena ni rahisi kuzalisha fedha ikiwa tutajizoeza kuyafuatilia na kuzingatia maeneo niliyoyataja ambako fedha zinapatikana.

 

Ni haki ya kila Mtanzania kuwa na fedha za kutosha.

 

0719 127 901

[email protected]

By Jamhuri