Makala yetu leo yahitaji kwanza kabisa kujibu swali; Nini Ukristo? Nini Uislamu? Bila ya kuzama kwenye fasili za mabingwa wa teolojia na historia za dini, kwa mujibu wa Kamusi Elezo Huru, Ukristo (kutoka neno la Kigiriki Khristos, ambalo linatafsiri lile la Kiebrania Mašîah, linalomaanisha ‘Mpakwa Mafuta’), ni dini inayomwamini Mungu pekeekama alivyofunuliwa kwa Waisraeli katika historia ya wokovu ya Agano la Kale na hasa Yesu Kristo (Amani iwe juu yake) katika Agano Jipya ambaye ni mwanzilishi wake katika karne ya kwanza. 

Kamusi Elezo Huru pia imeuelezea Uislamu (kwa Kiarabu Al-Islam) kuwa ni dini inayotokana na mafunzo ya Mtume Muhammad (Allaah Amrehemu na Ampe Amani). Uislamu ni ile imani kuwa muumba ni mmoja tu kwa dhati na sifa zake. 

Nguzo nyingine za imani zinajengwa juu ya imani ya Mungu mmoja wa kweli, imani juu ya maisha baada ya kifo, imani juu ya Malaika wa Mungu, vitabu vyake na kudra na tafsiri ya vitendo ya imani hii ni: sala, zakah, saumu na hija.

Fasili hii ya Uislamu ni finyu na inauzungumzia Uislamu ukihusishwa na Mtume Muhammad. Ama Uislamu kwa tafsili pana ni Dini ya Allaah waliyokuja nayo mitume wote kutoka Adam (Amani iwe juu yake) hadi Mtume Muhammad na huo ni mfumo kamili na muongozo wa maisha ambao Mwenyezi Mungu amewatuma mitume wake waufikishe kwa watu ili waufuate katika vipengele vyote vya maisha yao.

Dini mbili hizi ambazo msingi wake mkuu, kwa mujibu wa fasili iliyotangulia, ni Imani ya Mungu mmoja pekee, ni miongoni mwa dini tatu zinazohusishwa na Mtume Ibrahimu (Amani iwe juu yake) hivyo kuitwa Dini za Ibrahimiya. Dini ya tatu ni Uyahudi.

Katika makala hii nakusudia kuyaweka wazi mambo mawili yanayozihusu dini mbili hizi za Uislamu na Ukristo ambazo ndizo dini kuu nchini Tanzania ili mambo haya yaturejeshe katika mstari wa tafakuri sahihi ya uhusiano wa dini mbili hizi nje ya yale yaliyozikumba kama athari hasi za ukoloni mkongwe, ukoloni mamboleo, mila na desturi za watawala waliotumia dini kama nyenzo ya kutawalia, propaganda za kuutukuza Uarabu (Arabization) na Uzungu wa Mashariki na Magharibi (Eastern and Western Civilization).

Nimetangulia kueleza kuwa Ukristo na Uislamu (kwa tafsiri finyu) ni dini zinazohusishwa na Mtume Ibrahimu kwa kuwa ni dini zinazohusishwa na ufunuo uliofikishwa kwa manabii na mitume kupitia Malaika Jibril. Dini hizi zinaitwa Dini za Mbinguni na zote zinaamini siku ya hukumu na kulipwa pepo au kuadhibiwa motoni.

Baada ya utangulizi huu turudi katika anuani ya makala yetu leo: Unayajua haya kuhusu Ukristo na Uislamu?

1. Uislamu uliutambua Ukristo wa Roma

Wakati ninafuatilia mafunzo ya shahada yangu ya kwanza iliyokusanya Falsafa, Taaluma za Dini na Lugha ya Kiswahili nilikumbana na wasomi wanaouhusisha Ukristo na Wayahudi na kwamba wanaposoma kwenye Qur’aan Tukufu habari za Wakristo huamini Ukristo unaozungumziwa ni ule unaowahusu Wayahudi. Ukweli ni kuwa Wayahudi hawajapata kuwa Wakristo kwani kwao Uyahudi ni Dini, Kabila na Taifa.

Tunaposoma katika Qur’aan Tukufu tunaikuta Sura ya 30 (Surat Ar-Rum). Neno Ar-Rum lina maana ya ‘Roma’. Sura hii inalielezea tukio lilitokea mwaka 613 ambapo Waajemi (Washirikina wanaoabudu masanamu) waliwashinda Warumi (Wakristo, Watu wa Kitabu). Habari hii ilipowafikia Washirikina wa Makkah walifurahi sana na walimwambia Mtume Muhammad kuwa: “Wakristo (Warumi), Watu wa Kitabu kama nyinyi, nao wameshindwa na washirikina wenzetu, na hii ni alama ya kuwa karibuni na sisi tutakushindeni.”

Qur’aan Tukufu ikajibu tambo hizo kwa kutoa bishara mbili zitakazotokea wakati mmoja, nazo ni; mosi, Wakristo Warumi kuwashinda Waajemi Washirikina; pili, Waislamu kuwashinda Washirikina wa Makkah. Tunasoma katika Qur’aan Tukufu Sura ya 30 (Surat Ar-Rum) aya ya 2 hadi ya 6 kuwa:

“Warumi wameshindwa. Katika nchi iliyo karibu (na nchi ya Bara Arabu. Nayo ni Shamu), nao baada ya kushindwa kwao, watashinda. Katika miaka michache, Amri ni ya Mwenyezi Mungu kabla (yake) na baada (yake); na siku hiyo (Warumi watakaposhinda) Waislamu watafurahi. Kwa nusura ya Mwenyezi Mungu (Anayowapa wao. Nayo ni kuwashinda Washirikina wa Makkah siku hiyo). (Mwenyezi Mungu Humnusuru amtakaye, naye ni mwenye nguvu (na) mwenye rehema. (Hii ni) ahadi ya Mwenyezi Mungu, Mwenyezi Mungu havunji ahadi yake, lakini watu wengi hawajui.”

Naam! Bishara hii njema ilitimia kwa Hirakla, Mfalme wa Warumi, kuingia Media (Madayin) katika nchi ya Waajemi na mwaka huohuo Waislamu 313 walilishinda jeshi la Washirikina wa Makkah 1,000 mastadi wa vita waliokuja kwa nia ya kuwaangamiza. Vita ikapiganwa katika Mtaa wa Badri na Washirikina wakashindwa vibaya.

Tunachojifunza hapa ni kuwa wakati Mtume Muhammad anapewa Utume mwaka 610 A.D. Ukristo alioukuta ni Ukristo wa Roma (Ukatoliki) ambao ulishaenea hapo tangu mwaka 313 A.D. wakati Kaisari Konstantino Mkuu alipotangaza huko Milano uhuru wa dini kwa wananchi wote na ukashamiri mwaka 380 wakati Kaisari Theodosius wa Kwanza alipoufanya Ukristo wa Kikatoliki kuwa dini rasmi ya Dola ya Kirumi.

2. Padri wa Kikatoliki alimuokoa Mtume Muhammad asiuawe

Katika Historia ya maisha ya utotoni ya Mtume Muhammad (Allaah Amrehemu na Ampe Amani) tunasoma tukio lilitokea mwaka 582 A.D. ambapo Mtume Muhammad akiwa na umri wa miaka 12  alifuatana na baba yake mdogo Abu Twalib Bin Abdil-Mutwalib kwenda Shamu, lakini walipofika Busra – mji wa kusini kabisa katika nchi ya Shamu – walikutana na padri jina lake Bahyra ambaye alimkataza asisogee na mwanawe zaidi kuliko hapo, akamwambia: “Mtoto huyu ninamwona ana alama zote za Mtume aliyetabiriwa kuwa atakuja, basi naona ni hatari kubwa akienda Shamu, asije akauawa na Wayahudi huko. Nakusihi sana urejee naye, au umpe mtu mwaminifu arejee naye, nawe uende katika biashara zako.”

Abu Twalib alimpa mtu arejee naye Makka naye akaendelea na safari yake.

Kitendo cha padri huyu kumnusuru Mtume Muhammad na shari za Wayahudi ambao kwa elimu waliyonayo, kama aliyokuwa nayo padri huyu, wangeng’amua alama za utume alizokuwa nazo Mtume Muhammad na wangeamua kumuua, kinasadifu yaliyokuja kwenye Qur’aan Tukufu juu uhusiano wa watu wa dini hizi tatu za Ibrahimiyya – Uyahudi, Ukristo na Uislamu.

Tunasoma katika Qur’aan Tukufu, Sura ya 5 (Surat Al-Maidah) Aya ya 82 kuwa: “Hakika utawakuta walio shadidi kuliko watu wote katika uadui kwa walioamini (Waislamu) ni Mayahudi na Washirikina. Na utawakuta walio karibu mno kwa mapenzi ni wale wanaosema: Sisi ni Wakristo. Hayo ni kwa sababu wapo miongoni mwao makasisi (mapadri) na watawa (Wamonaki), na kwa sababu wao hawafanyi kiburi.

Katika tukio hili na mafunzo haya ya Qur’aan Tukufu tunajifunza uhusiano mwema, kuhurumiana na mapenzi mema yaliyokuwepo na yanayostahili kuendelea kuwepo baina ya Waislamu ambao wametakiwa kujipamba na uadilifu na kutenda haki na insafu kwa wote na Wakristo wenye mapenzi kwa watu wakiwemo Waislamu na ambao wanapambwa na tabia njema zinazoongozwa na makasisi na watawa wasio na kiburi.

Kama hali ni hii, kwa nini tunawapa nafasi wale wanaopanda chuki kwa misingi ya kidini katika jamii yetu? Wanafanya hayo kwa mafundisho ya nani? Kiburi na maneno yasiyo staha yanayotolewa na baadhi ya wahubiri wetu yanafuata mafunzo yepi nje ya mafunzo ya Uislamu na Ukristo wanaokwenda tofauti nao?

Nihitimishe makala hii kwa kuwakumbusha Waislamu na Wakristo kurudi katika mstari wa asili wa uhusiano mwema na mapenzi baina yao, jambo tunalolihitajia sana katika kuimarisha umoja na mshikamano wa taifa letu la Tanzania ili kujenga nyenzo muhimu za kupambana na changamoto mbalimbali za kitaifa na kimataifa.

Hatuna budi kuchuja na kupembua mafunzo sahihi ya dini zetu na biashara na propaganda za wale wanaotumia dini kama nyenzo ya kufanikisha malengo yao mabaya kwetu na yasiyo na faida nasi. Msingi wa dini zote mbili hizi ni kuhubiri amani, upendo, kuhurumiana, kusaidiana na kuishi vema tukiwa ndugu na majirani. Yeyote anayehubiri kinyume cha haya huyo ana yake na hatutakii mema.

Makala hii iturudishe katika tafakuri juu ya chanzo cha yale tunayoyaona leo katika baadhi ya maeneo, hususan katika mitandao ya kijamii, yakiwahusisha wafuasi wa dini mbili hizi yaliyo kinyume cha mafunzo haya; tunapoona chuki mahali pa mapenzi, uhusiano mbaya mahali pa uhusiano mwema, ni dhahiri hapo kinachosumbua si dini, bali masilahi binafsi au athari hasi za ukoloni mkongwe, ukoloni mamboleo, mila na desturi za watawala waliotumia dini kama nyenzo ya kutawalia, propaganda za kuutukuza Uarabu na Uzungu wa Mashariki na Magharibi.

Haya tukutane Jumanne ijayo, In-Shaa-Allaah.

Sheikh Khamis Mataka ni Mwenyekiti wa Halmashauri Kuu ya Baraza Kuu la Waislamu wa Tanzania (Bakwata).

Simu: 0713603050/0754603050

699 Total Views 2 Views Today
||||| 1 Unlike! |||||
Sambaza!