Katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa (UN), Antonio Guterres, amesema kuwa bado kuna maeneo mengi ulimwenguni yanakabiliwa na kushindwa kwa suala la amani.

Ameyasema hayo kupitia ujumbe wake wa siku ya kimataifa ya amani alipokuwa akihutubia umoja huo huko jijini NewYork Marekani
“Lakini bado katika maeneo mengi, katika mazingira mengi sana, tunashindwa katika suala la amani.” amesema Guterres.

Kila ifikapo Septemba 21 kila mwaka Umoja wa Mataifa huadhimisha Siku ya Amani Duniani ambapo katika maadhimisho hayo kauli mbiu ya mwaka huu ni ni “Komesha ubaguzi wa rangi, jenga amani”

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa António Guterres akigonga kengele ya amani kwenye hafla iliyofanyika kwenye makao makuu ya Umoja wa Mataifa kuadhimisha siku ya kimataifa ya amani. Picha na UN

Katika kuadhimisha siku hiyo Guterres ameyahimiza mataifa ulimwenguni yanayokabiliwa na migogoro umasikini na ukosefu wa usawa kusitisha mapigano na na kuinua harakatiza kupambania haki za binaadamu.

“Badala ya kupigana sisi kwa sisi, tunapaswa kufanya kazi ili kuwashinda maadui wetu wa kweli ambao ni ubaguzi wa rangi, umaskini, ukosefu wa usawa, migogoro, changamoto za tabianchi na janga la COVID-19 Tunapaswa kubomoa miundo inayoendeleza ubaguzi wa rangi, na kuinua harakati za kupigania haki za binadamu kila mahali” amesema Guterres .

Guterres ameyataka mataifa kutokupigana yenyewe kwa yenyewe na kukomesha majanga na masuala yanayochangia uvunjifu wa amani akitaja ubaguzi wa rangi ukosefu wa usawa na changamoto za tabianchi kama mambo yanayochangia kwa kiasi kikubwa katika uvunjifu wa amani.

Aidha Guterrs amehitimisha ujumbe wake kwa kusema kuwa “Katika siku hii muhimu, wakati wa kuzingatia saa 24 za kutokuwa na vurugu na kusitisha uhasama tunasisitiza wito wetu kwa watu wote kufanya juhudi zaidi zaidi ya kuweka chini silaha zao.

Tunatoa wito kwao kuthibitisha tena vifungu vya mshikamano tunaoshiriki kama binadamu na kufikia mchakato wa kujenga ulimwengu bora na wa amani zaidi.”

Waziri wa Mambo ya Ndani, Hamad Masauni, alipokuwa akiwasilisha azimio la Mkataba wa Umoja wa Nchi Huru za Afrika wa Kuzuia na Kupambana na Ugaidi jana Jumanne Septemba 20,2022 bungeni, alieleza kuwepo kwa matukio yenye viashiria vya ugaidi ndani ya nchi katika mikoa ya Arusha, Geita Mwanza, Pwani na Tanga.

Waziri Masauni, amesema mwaka 2004 ilianzishwa Itifaki ya Mkataba wa Umoja wa Nchi Huru za Afrika wa Kuzuia na Kupambana ikiwa ni katika kuzingatia Ibara ya 21 Ibara Ndogo ya Kwanza ya Mkataba wa Umoja wa Nchi Huru za Afrika wa Kuzuia na Kupambana na Ugaidi wa mwaka 1999 na Tanzania ilisaini Itifaki hiyo Januari 27, 2005.

Amesema itifaki hiyo itaimairisha ulinzi na usalama wa raia na mali zao, na kurahisisha ubadilishanaji wa taarifa za kiintelijinsia zinazohusu ugaidi kupitia ushirikiano na nchi wanachama.

Hata hivyo Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, liliridhia Itifaki ya Mkataba wa Umoja wa Nchi Huru za Afrika wa Kuzuia na Kupambana na Ugaidi ya Mwaka 2004, kama uliowasilishwa na Waziri Masauni.

Kwa mujibu wa ripoti ya Global Peace Index iliyotolewa Agost 2022 Tanzania inatajwa kuwa ya 86 kati ya nchi 163 zenye amani duniani zilizofanyiwa utafiti na vipimo vya nchi zenye amani Zaidi duniani Nchi ya Iceland ikishika nafasi ya kwanza.

By Jamhuri