Wiki iliyopita wadau mbalimbali nchini pamoja na wengine kutoka jumuiya ya kimataifa walishiriki mdahalo mahususi kuhusu masuala ya biashara nchini.

Katika mdahalo huo mengi yalijitokeza yenye lengo la kuboresha ili hatimaye kupata tija zaidi kwa upande wa tasnia ya biashara nchini. Itakumbukwa kuwa wiki kadhaa kabla ya mdahalo huo, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. John Magufuli, alifanya mkutano na kundi kubwa la wafanyabiashara kutoka maeneo mbalimbali ya nchi.

Kwa hiyo mdahalo wa wiki iliyopita umekuwa wenye manufaa zaidi katika kuendelea kutafakari zaidi kile kilichojitokeza kwenye mkutano ule wa awali.

Kwa kuzingatia muktadha huohuo, akifungua mdahalo huo, Kaimu Balozi wa Marekani nchini, Inmi Patterson, ameishauri Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kuwa, kwa kuzingatia ushauri kutoka maeneo mbalimbali kuhusu kuboresha mazingira ya sekta binafsi nchini, Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ianze kutelekeza ushauri huo kwa vitendo, bila kuchelewa.

Kaimu Balozi huyo amesema: “Ili kuweza kuvutia na kuendelea kuaminika kwa wawekezaji kutoka nje ya nchi, wakiwamo wawekezaji kutoka Marekani, Serikali ya Tanzania ni lazima iondoke katika wigo wa midahalo sasa na kuingia kwenye vitendo visivyowavunja moyo wawekezaji.”

Inmi Patterson akaongeza: “Sekta binafsi imekumbwa na changamoto nyingi, na ni lazima zitazamwe ili kupata ufumbuzi wenye kuzingatia haki za mwekezaji. Serikali ya Tanzania ni kama imepoteza imani yake kwa sekta binafsi.

Ingawa wawakilishi wa serikali walioshiriki tukio hilo walieleza namna serikali ilivyokwishaanza kuchukua hatua kukabili changamoto zilizopo katika tasnia ya biashara na hususan sekta binafsi, lakini ukweli ni kwamba, bado juhudi zaidi zinahitajika kama alivyoeleza Kaimu Balozi wa Marekani, Inmi Patterson.

Lakini wakati tunahimiza serikali kuwa karibu na sekta binafsi, vilevile kwa upande wetu, JAMHURI, tunahimiza uadilifu zaidi miongoni mwa wadau walioko kwenye sekta binafsi. Ni lazima tuelewe kuwa, moja ya madaraja muhimu katika ushirikiano baina ya serikali na sekta binafsi ni uadilifu unaotanguliza masuala muhimu ambayo ni pamoja na masilahi ya nchi wakati wote, sambamba na utii wa sheria.

10091 Total Views 2 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!