NA EDITHA MAJURA

Dodoma

Agizo la Rais John Magufuli kuzuia wazazi wa wanafunzi wanaosoma katika shule za msingi na sekondari zinazomilikiwa na Serikali wasitozwe michango, limeibua changamoto katika uendeshaji wa shule hizo mkoani hapa, imebainika.

JAMHURI limebaini hayo baada ya kuzungumza na baadhi ya wanafunzi, walimu na wazazi walio walengwa katika utekelezaji wa agizo hilo.

Hali iliyopo kwenye shule kadhaa imeonesha upungufu wa fedha na rasilimali zinazohitajika hasa kwa kufundisha na kufundishia, hali inayoibua hamasa ya uchangiaji wa gharama kutoka kwa jamii.

Mathalani, taarifa ya Afisa Elimu wa Mkoa wa Dodoma inaeleza kuwapo upungufu wa matundu 12,057 ya vyoo kwa shule za msingi pekee.

Miongoni mwa shule hizo ni Shule ya Msingi Nzuguni ‘B’ iliyopo Manispaa ya Dodoma, yenye matundu 8 ya vyoo yanayotumiwa na wanafunzi zaidi ya 2,000.

Idadi hiyo ni tofauti na utaratibu unaoelekezwa na mkoa kwa tundu moja la choo kutumiwa na wanafunzi wavulana 25 (1:25) na kwa upande wa wasichana ni wanafunzi 20.

Mwenyekiti wa kamati ya shule hiyo, Joseph Masinga, amesema ingawa agizo la Rais Magufuli lina nia njema, kuna baadhi ya mahitaji yasiyohitaji kusubiri bajeti ya Serikali kushughulikiwa.

Anatoa mfano kuwa shule hiyo inapokea Sh. 270,000 kila mwezi kwa ajili ya ukarabati wa miundombinu, kiasi ambacho ni kidogo ikilinganishwa na mahitaji yaliyopo ambayo hata hivyo hakuyataja.

Wazazi walipofika na kushuhudia vyoo vinavyotumiwa na wanafunzi, wengine walitokwa na machozi, tukaafikiana kila mwanafunzi achange Sh 2,000 ili matundu yaongezwe,” amesema.

Kwa mujibu wa Masinga, michango hiyo imefanikisha kupatikana mifuko 60 ya saruji huku wazazi na walezi wakiendelea kutoa michango, lakini sasa imekoma ili kuitikia agizo la Rais Magufuli.

Amesema mwaka jana, Afisa Afya wa Manispaa alitoa ilani ya kufunga shule hiyo kutokana na ubovu wa vyoo, ikalazimu kutumia sehemu ya fedha zilizochangwa na wazazi kukodi gari la majitaka kwa ajili ya kusafisha mashimo hayo ambayo yalijaa.

Anatoa mfano mwingine katika fungu la michezo, kila wanafunzi anapata kati ya Sh 30 na 50 ambapo anatakiwa kupelekwa kwenye shule nyingine ndani ya kata husika kushiriki michezo.

MADARASA

Masinga anasema shule hiyo ina vyumba tisa, vitatu kati ya hivyo vikiwa pekee vyenye ubora unaokidhi viwango, hali ambayo inasababisha wanafunzi waingie madarasani kwa kupokezana.

Amesema vyumba vyenyewe vilijengwa mwaka jana kwa usimamizi wa aliyekuwa Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Seleman Jafo, ambaye kwa sasa ndiye Waziri wa wizara hiyo.

Kwa mujibu wa Masinga, ujenzi wa vyumba hivyo ulifanikiwa kwa muda mfupi kutokana na michango ya wadau wakiwamo walimu na wajumbe wa kamati ya shule.

CHAKULA

Masinga anasema shule hiyo imekuwa na utaratibu wa mzazi kuchangia Sh 10,000 kwa kila wanafunzi wa darasa la saba kwa ajili ya chakula cha mchana na mafunzo ya ziada ikiwa sehemu ya maandalizi ya mitihani ya Taifa.

Amesema uamuzi huo ulifikiwa kati ya wazazi na uongozi wa shule, lengo likiwa ni kuzikabili changamoto zilizosababisha shule hiyo kufanya vibaya katika mitihani ya kuwashindanisha wanafunzi katika Kata ya Nzuguni

Rehema Alfonce, mkazi wa Nzuguni ‘B’ ambaye mtoto wake anasoma darasa la tano shuleni hapo, amesema kinachotakiwa kufanywa ni Serikali kuweka utaratibu ili michango inayotolewa kuboresha mazingira ya shule badala ya kuwanufaisha watu binafsi.

Masinga anashauri viongozi wanaozungumza au kumpelekea taarifa Rais Magufuli, wamueleze ukweli kuhusu hali halisi ilivyo kwenye shule hizo.

Masinga ameshauri utafutwe utaratibu ulio rafiki na rahisi kufikiwa na wachangiaji wengi, na utakaowezesha michango kuwafikia walengwa kwa wakati.

Mwalimu wa shule moja ya sekondari mkoani humo (jina tunalihifadhi) ameliambia JAMHURI kwamba kuzuia michango mashuleni kutafifisha uboreshaji wa sekta ya elimu.

Elimu bila kuchangia ni vigumu kutolewa shuleni kwa kuwa kuna maeneo mengi yanapwaya, hasa taaluma, mitaala yetu ni mirefu kiasi kwamba muda wa kawaida wa vipindi uliyopangwa ni mdogo, mara nyingi mwalimu anatumia muda wa ziada kujengea wanafunzi uzoefu,” amesema

Ametoa mfano wa shuleni kwake kwamba kila mwanafunzi alichangia Sh 20,000 kwa muhula ili kugharamia masomo ya ziada ikiwa ni malipo kwa walimu wanaojitolea.

Utaratibu huo umeelezwa kuwapo kwa miaka mingi, hivyo ikiwa michango hiyo itapita kwa Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya inaweza kuibua ugumu kuwafikia walimu na hivyo kukwamisha utaratibu huo.

Amesema palikuwa mchango mwingine wa Sh 20,000 kwa kila mwanafunzi kwa mwaka, iliyotumika kuwapeleka wanafunzi kushiriki mashindano ya mitihani na midahalo kati ya shule za mkoani humo.

Mwalimu huyo amesema shughuli nyingine ya fedha hizo ilikuwa kuwalipa walimu wa kukodi, kwa ajili ya kuziba mapengo ya walimu yaliyotokana na uhaba wa walimu kwa baadhi ya shule.

Kwa mujibu wa taarifa ya sekta ya elimu kwa Kamati ya Ushauri ya Mkoa wa Dodoma, kuna walimu 834 wa masomo ya sayansi wakati mahitaji ni walimu 1,361, hivyo upungufu kuwa ni walimu 527.

1506 Total Views 3 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!