Sekta ya utalii inatajwa kuwa ya pili katika kuchangia pato la Taifa kutokana na fedha za kigeni, lakini pia  ina fursa nyingi zinazoweza kuzalisha ajira kwa watu wanaozunguka maeneo husika.

Kama ilivyoainishwa kwenye madhumuni na malengo ya Sera ya Utalii toleo la mwaka 1991, ya kuongeza mchango wa sekta hiyo kwenye pato la Taifa, kwa kukuza na kuimarisha shughuli za kiuchumi zinazoambatana na biashara ya utalii kama vile kilimo, viwanda, mawasiliano, uchukuzi, mila, desturi, sanaa na utamaduni, ikiwa ni pamoja na kuimarisha na kudumisha vyombo mbalimbali vinavyohusika na biashara ya utalii, mambo ambayo yanatakiwa kwenda sambamba kuimarisha na kuendeleza mafunzo kwa kada mbalimbali katika uendeshaji wa biashara ya utalii katika fani za hoteli, uhandisi, uwakala, uongozi, uokoaji, upishi na nyinginezo.

Pamoja na kuwa na sera nzuri inayotoa mwelekeo kwa wizara, Serikali na wadau wengine, nini cha kufanya ili kuhakikisha wananchi wanaozungukwa na fursa hizo za utalii wananufaika kwa ajira na kuinua kipato, bado jamii maeneo mengi haijanufaika.

Wilaya ya Serengeti licha ya kuzungukwa na Hifadhi ya Taifa ya Serengeti, mapori ya akiba ya Ikoma na Grumeti, na Maeneo ya Hifadhi ya Jamii (WMA), wafanyabiashara wamewekeza katika biashara za hoteli ambazo zingeweza kutengeneza ajira za kutosha kwa jamii inayowazunguka.

Si kwa kazi tu bali hata biashara mbalimbali ambazo zingesaidia kuinua kipato chao, kujiajiri na kuajiri wengine. Lakini wananchi wanaozunguka maeneo hayo wanageuka watazamaji tu, hawanufaiki na shughuli hizo za kitalii.

Kuna hoteli, kambi za kudumu na za muda za kitalii ambazo, kwa mujibu wa tafiti mbalimbali, zinaweza kutengeneza nafasi zaidi ya 5,000 za ajira, lakini kwa Serengeti wakazi wenye kazi ni wachache, huku wengi wakiwa ni walinzi, wafanya usafi na wapishi.

Lakini inadaiwa kwamba wananchi wengi wilayani hawana sifa ya elimu ya utalii, kazi ambayo ilipaswa kufanywa na Serikali hata kwa kuanzisha Chuo cha Mafunzo ya Ufundi Stadi (VETA) wilayani hapa kama inavyoelezwa kwenye Ilani ya Uchaguzi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) ya mwaka 2005 na 2010.

Samwel Peter, ni Meneja wa Chuo cha Utalii cha Serengeti (STC). Anasema lengo la chuo hiki ni kuziba ombwe lililopo la kuwapa elimu vijana waweze kunufaika na soko la ajira katika sekta
ya utalii.

“Hoteli na kambi zilizomo ndani ya ikolojia ya Serengeti, ni zaidi ya 70 zinazozalisha ajira ya watu zaidi ya 7,000 lakini katika Mkoa wa Mara walioko kwenye soko hilo hawazidi asilimia 10, lakini kila wakati wanaambiwa wajiajiri bila hata kujengewa uwezo,” anasema.

Anasema STC inalenga kuwawezesha vijana kuingia kwenye soko la ushindani la ajira na watu kutoka mikoa mingine, ili kuwaondoa kwenye dhana ya kulalamika kuwa watu wa nje ya mkoa wananufaika wakati tatizo ni ukosefu wa stadi na sifa za kuajiriwa.

Kwa mujibu wa Sera ya Utalii, Chuo cha Mafunzo ya Hoteli cha Forodhani kitaimarishwa ili kitoe mafunzo ya hali ya juu kukidhi mahitaji ya wataalamu mbalimbali wa sekta ya utalii.

Hata hivyo, Peter anakiri kuwa bado mwamko wa vijana wilayani Serengeti katika kuchangamkia fursa za kiuchumi na kielimu ni mdogo.

Kwamba mitizamo hasi waliyonayo inawafanya wanaume wengi kujikita katika kazi za uwindaji haramu wa wanyamapori, huku wakidai kuwa kazi ya upishi ni ya wanawake, hivyo wao kufanya kazi hizo wanajidhalilisha.

“Hata baadhi ya wazee wanachukulia fani hiyo kama ya kihuni kwa kuwa watoto wao watafanya kazi kwenye hoteli na baa, wanashindwa kutofautisha kati ya baa zilizopo mjini Mugumu (Serengeti) na hoteli za kitalii… Wanasiasa wasaidie kubadili mitizamo hiyo,” anaongeza Peter.

Vijana zaidi ya 400 wameshafuzu chuoni hapo katika fani za utalii, ujasiriamali, lakini wengi wao wakitoka Wilaya jirani za Tarime, Manyara, Arusha na nchini Kenya.
Katika juhudi za kuhakikisha Serengeti inakuwa kitovu cha utalii, tayari imesajili kampuni ya kusafirisha wageni ya Mara Bush Adventure Safari Ltd, ambayo itasaidia kutoa elimu kwa vitendo, na wageni wa kampuni hiyo watahudumiwa na wanachuo.

Anabainisha kuwa mpango wa ujenzi wa uwanja wa ndege wa kimataifa wa Serengeti utasaidia kukuza uchumi wa wilaya hiyo kupitia sekta ya utalii, hivyo wananchi wanatakiwa kujiandaa kutumia vema fursa hiyo.

Chuo hicho kwa sasa kinakusudia kutoa msaada kwa wanafunzi wilayani hapo, kwa kuwalipia wasiojiweza wakati kwa kuanzia wanatarajia kuanza na Sh milioni mbili kwa kazi hiyo.

Pia chuo hicho kina mpango wa kuanza kutoa elimu ngazi ya digrii, na kuwataka wakazi wa wilaya hiyo kujitokeza kwa ajili ya kupata elimu waweze kushika soko la utalii ili waache kulalamika.

Please follow and like us:
Pin Share