Home Kitaifa Utendaji wa Puma wamkuna Kalemani

Utendaji wa Puma wamkuna Kalemani

by Jamhuri

Waziri wa Nishati, Dk. Medard Kalemani, amesema serikali inaridhishwa na utendaji wa Kampuni ya kuagiza na kuuza mafuta ya Puma Energy Tanzania Limited na kuitaka kuendelea kuboresha shughuli zake hapa nchini.

Dk. Kalemani ameyasema hayo jijini Dar es Salaam mwishoni mwa wiki katika hafla iliyoandaliwa na Puma kuwazawadia mawakala wake ambao wamefanya vizuri.

Serikali inamiliki asilimia 50 ndani ya kampuni hiyo ambayo imekuwa ikitoa gawio kwa serikali kila mwaka.

“Utendaji mzuri wa kampuni unadhihirika kupitia ongezeko la gawio ambalo linatolewa kwa serikali kila mwaka,” anasema Dk. Kalemani na kubainisha kuwa mwaka 2018 Puma ilitoa Sh bilioni 9 kama gawio kwa serikali na mwaka 2019 kiasi hicho kiliongezeka hadi Sh bilioni 11.

“Ni matarajio yangu kuwa kiasi cha gawio kitaongezeka hadi Sh bilioni 13 mwaka huu na ikiwezekana zaidi ya hapo,” anasema.

Aidha, Dk. Kalemani ameitaka kampuni hiyo kupanua shughuli zake nchini kwa kuanzisha vituo vidogo vidogo vya kuuza mafuta katika maeneo ya vijijini kama njia ya kuhakikisha kuwa Watanzania wengi wananufaika na huduma zake.

Anasema kupanuka kwa biashara ya usafirishaji kumetoa fursa hadi maeneo ya vijijini ambako hivi sasa watu wanalazimika kuhifadhi mafuta kwenye madumu na chupa za maji.

“Katika maeneo ya vijijini mnaweza kuweka vituo vidogo ambavyo vitaendana na hali za huko. Kikubwa ni kuwa watu wameshaonyesha wanahitaji huduma hizi,” anasisitiza.

Anasema kampuni hiyo inatakiwa kufanya hivyo kwa sababu itakuwa inatekeleza sera ya serikali inayotaka kusambazwa kwa huduma za nishati kwa Watanzania wengi zaidi, hasa wale wa maeneo ya vijijini.

Awali, Dk. Kalemani alibainisha kuwa hali ya mafuta nchini ni nzuri. Anasema kwa kipindi cha miaka minne iliyopita Tanzania haijawahi kukumbwa na msukosuko kwenye suala la mafuta na hivi sasa nchi ina hifadhi ya kutosha ya mafuta ya aina zote.

Aliiambia hadhira hiyo kuwa hadi kufikia mwishoni mwa mwezi uliopita nchi ilikuwa na hifadhi ya lita milioni 197 za mafuta aina ya dizeli ambayo yanatosheleza mahitaji ya siku 28, wakati kulikuwa na hifadhi ya lita milioni 97 za petroli zinazotosheleza mahitaji ya siku 38.

Dk. Kalemani anasema pia kulikuwa na hifadhi ya lita milioni 30.09 za mafuta ya ndege yanayotosheleza mahitaji ya siku 56, wakati huo huo kukiwa na hifadhi ya lita 660,000 za mafuta ya taa.

“Tuna hifadhi ndogo ya mafuta ya taa kwa sababu kutokana na kazi ya kusambaza umeme vijijini matumizi ya mafuta hayo yamepungua sana maeneo ya vijijini,” anafafanua.

Awali, Mkurugenzi Mkuu wa Puma, Dominic Dhanah, alisema kuwa tuzo hizo ni za kwanza za aina yake nchini na Puma iliamua kufanya hivyo ili kuonyesha jinsi inavyowathamini wadau wake.

“Lengo la tuzo hizi ni kutoa hamasa na kuwapa changamoto waendesha vituo ili waweze kutoa huduma bora zaidi,” anasema.

You may also like