Shirika la Viwango Tanzania (TBS) wamelikoroga baada ya kutoa matokeo ya uchunguzi yaliyojaa utata kuhusu shehena ya mahindi kutoka nchini Marekani ambayo imekaa bandarini kwa miaka miwili. 

Uchunguzi wa Gazeti la JAMHURI umebaini kwamba Oktoba mwaka jana Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari (TPA), iliamua kuchukua hatua za kupiga mnada shehena ya mahindi ambayo imekaa katika maghala ya TPA kwa miaka miwili. 

Kabla ya kufikia uamuzi kwa kushirikiana na taasisi nyingine za serikali, ilibidi kuifahamisha TBS ili ipime viwango vya ubora wa mahindi hayo kama yanafaa kwa matumizi ya binadamu na wanyama, kutokana na kukaa bandarini hapo kwa muda mrefu. 

Chanzo cha kuaminika kimeliambia JAMHURI kwamba zimekuwapo jitihada za kutaka kuhakikisha shehena hiyo ya mahindi inaharibiwa na serikali kukosa mapato yake, vilevile TPA kukosa tozo zake ambazo zinakadiriwa kufikia kiasi cha dola za Marekani milioni 6.2 hadi kufikia Disemba mwaka jana. 

“Shehena hiyo ilitakiwa kupigwa mnada na TPA kwa kushirikiana na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) ili kuanza taratibu za mnada, kwa kuwa shehena hiyo ilikuwa ya mahindi kabla ya taratibu za mnada kuanza walijulishwa TBS.

“Ili kujiridhisha na ubora wa shehena hiyo ya mahindi, taarifa ya uchunguzi ya TBS ilielekeza mahindi hayo yateketezwe, maana hayakuwa yanafaa kwa matumizi ya binadamu wala wanyama,” kinaeleza chanzo chetu. 

Chanzo chetu ambacho hakikutaka kutajwa gazetini kinasema: “Baada ya ripoti hiyo ya uchunguzi kuonyesha dosari ya shehena ya mahindi, Novemba mwaka jana Waziri Mkuu Kassim Majaliwa aliingilia kati kwa kuwaita TRA, TPA, TBS, Ofisi ya Mkemia Mkuu wa Serikali pamoja na Mamlaka ya Dawa na Vifaa Tiba (TMDA).

“Baada ya kikao hicho TBS walipima tena sampuli ya shehena hiyo ya mahindi na kutoa majibu kwamba mahindi hayo yanaweza kutumika kwa wanyama tu, si binadamu. 

“Waziri Mkuu alielekeza kwamba taratibu za mnada huo ziendelee na mnada huo ufanyike kwa kuzingatia taratibu za forodha, mahindi hayo yauzwe nje ya nchi, maana wenye mahitaji nayo walikuwa wa nje ya nchi na TRA walitakiwa kusimamia mnada huo,” kinasema chanzo chetu. 

Hata hivyo mtoa taarifa wetu anasema kwamba zimekuwapo harakati nyingi zinazofanywa katika kuhakikisha kwamba shehena hiyo ya mahindi ambayo ilitakiwa kupelekwa nchini Zambia inaondolewa bure ama inateketezwa kwa kigezo kwamba haifai. 

“Kama Waziri Mkuu Kassim Majaliwa asingeingilia na kuweka mambo sawa, ninakuhakikishia ndugu yangu serikali ilikuwa inakwenda kukosa kodi yake. Maana tayari ilishatoka taarifa kwamba shehena ile haifai, ila cha kushangaza baada ya waziri mkuu kuingilia kati, eti ikatoka ripoti ya uchunguzi inayosema mahindi yale yanafaa kwa chakula cha wanyama,” kinasema chanzo chetu. 

JAMHURI limezungumza na Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Viwango Tanzania (TBS), Dk. Yusuf Ngenya, ili kupata ufafanuzi wa kituko cha kutoa majibu yanayokinzana, huku yakiwa yametolewa na taasisi yake. 

“Unasema kwamba kulikuwa na sampuli za yale mahindi mara mbili? Mimi naitambua hiyo ya pili, lakini hiyo ya kwanza siitambui hata kidogo,” anasema Dk. Ngenya. 

Kimsingi Dk. Ngenya anasema kwamba yeye anaitambua ile sampuli iliyochukuliwa na TBS mara ya pili, ambayo ilitoa majibu kwamba mahindi hayo yanafaa kwa chakula cha mifugo na si ile ya kwanza iliyosema mahindi hayo hayakuwa yanafaa kwa binadamu wala mifugo. 

Mahindi hayo ni ya nani?

Uchunguzi wa JAMHURI umebaini kwamba shehena hiyo ya mahindi kutoka nchini Marekani ilikuwa mali ya Kampuni ya Zdenakie Commodities Ltd ya Zambia. Shehena hiyo iliwasili katika Bandari ya Dar es Salaam Machi 14, mwaka juzi, mzigo huo ulitakiwa kwenda nchini Zambia. 

Shehena hiyo imekaa muda mrefu katika Bandari ya Dar es Salaam kutokana na kubadilika kwa eneo ambalo mzigo ulitakiwa kwenda. 

JAMHURI limebaini kwamba baada ya shehena hiyo kufika Bandari ya Dar es Salaam, Kampuni ya Zdenakie Commodities Ltd ya nchini Zambia ilielekeza shehena hiyo iende kwa Kampuni ya African Service Maintenance Ltd ya nchini Kenya. 

Chanzo chetu kinasema TPA pamoja na TRA walishtuka baada ya kuona kuna jitihada za kutaka kubadili uelekeo wa shehena hiyo ya mahindi kutoka kupelekwa Zambia na badala yake kutakiwa kupelekwa Rwanda na Kenya. 

“Mmiliki mpya alielekeza shehena hiyo isafirishwe kuelekea Rwanda na Kenya, badala ya Zambia kama ilivyokuwa awali. Mabadiliko hayo yalihitaji vibali ili kusafirisha shehena hiyo, jambo ambalo halikuwa limefanyika,” kinasema chanzo chetu. 

Anasema jambo jingine lililofanya shehena hiyo kukaa muda mrefu ni mmiliki wa shehena hiyo Zdenakie Commodities Ltd kushindwa kulipa tozo ya thamani ya dola za Marekani 967,500 (zaidi ya Sh bilioni 2). 

JAMHURI limewatafuta wamiliki wa kampuni zote mbili za Zdenakie Commodities Ltd pamoja na African Service Maintenance Ltd, ambao hawakupatikana ili kutoa ufafanuzi wa mkanganyiko wa shehena ya mahindi iliyoko bandarini kwa miaka miwili na sasa inaingia mwaka mwingine. 

Gazeti la JAMHURI linafahamu kwamba kuna taratibu ambazo zinaendelea ndani ya TRA pamoja na TPA kuondoa mzigo huo. Hata hivyo jitihada za JAMHURI kumpata Mkurugenzi wa Elimu kwa mlipa kodi kutoka TRA, Richard Kayombo, hazikufanikiwa.