Uzembe wa serikali kushindwa kutangaza kwenye gazeti lake makubaliano na kampuni ya kigeni kuhusu msamaha wa kodi uliotolewa kwa kampuni hiyo umezua mzozo wa kodi inayozidi Sh bilioni 1.3.

Mzozo huo unatokana na hatua ya serikali kuipa taasisi hiyo msamaha wa kodi lakini ikashindwa kulitangaza suala hilo katika Gazeti la Serikali.

Kukosekana kwa taarifa hizo kuliifanya Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) kuiandikia taasisi hiyo kuidai kodi ya Sh milioni 858 baada ya kubaini kuwa baadhi ya watumishi wake kutoka nje ya nchi walikuwa hawalipi kodi ya mishahara.

Taasisi hiyo, ICAP Columbia Univesirty iliyosajiliwa nchini kama Mailman School of Public Health Tanzania LLC (MSPH Tanzania LLC), imelazimika kukimbilia mahakamani kupinga madai ya kodi ya zaidi ya Sh milioni 858 yaliyoibuliwa na TRA.

Taasisi hiyo imesajiliwa kutoa elimu ya afya kwa umma hasa kuhusu maambukizi ya virusi vya ukimwi.

Pamoja na msamaha wa PAYE, ripoti hiyo inaonyesha pia kuwa walikuwa hawakatwi tozo ya zuio kutokana na mishahara yao (withholding tax), kodi ya pango (rental tax), kodi ya kuendeleza ufundi stadi (SDL) na ushuru wa stempu (stamp duty) ambapo tangu mwaka 2013 kodi hizo zilizokwepwa zinafikia Sh 521,463,374.

Tangu mwaka 2013 hadi 2018 jumla ya Sh 1,380,009,731 ambazo ni makato ya PAYE pamoja na tozo nyingine zilistahili kukatwa kutoka kwenye mishahara yao.

Mchanganuo wa kodi ya pato linalotokana na mshahara ambao Gazeti la JAMHURI limeuona unaonyesha kuwa mwaka 2015 taasisi hiyo haikukata PAYE ya Sh 77,159,262 na kwa mwaka 2016 makato ya jumla ya Sh 298,065,575 hayakulipwa.

Kwa mwaka 2017 ripoti hiyo inaonyesha kuwa taasisi hiyo ilishindwa kuwasilisha jumla ya Sh 335,177,486 zilizopaswa kukusanywa kama mapato kutoka kwenye mishahara ya wafanyakazi hao huku kwa mwaka 2018 ikionyesha kuwa makato hayo yangefikia jumla ya Sh 148,144,035.

Jitihada za kuwasiliana na uongozi wa taasisi hiyo ili kupata ufafanuzi zimegonga mwamba kwa zaidi ya wiki tatu sasa.

TRA iliiandikia taasisi hiyo Agosti 10, mwaka jana kuidai kiasi hicho cha fedha baada ya ukaguzi uliofanywa na kitengo cha mapato ya ndani cha TRA Mkoa wa Kodi wa Ilala.

Ukaguzi uliofanywa na ofisi za TRA Mkoa wa Kodi wa Ilala kwa kuangalia historia ya ulipaji kodi katika taasisi hiyo tangu mwaka 2013 hadi 2018, ulibaini kuwa wafanyakazi wa ngazi ya juu katika taasisi hiyo waliondolewa kwenye makato ya Kodi ya Pato la Mishahara (PAYE) mwaka 2015.

Ukaguzi huo ulibaini kuwa kuondolewa kwa PAYE ya wafanyakazi hao kumelikosesha taifa jumla ya Sh 858,546,357. Kiasi hicho cha fedha kinahusisha kodi ya PAYE iliyopaswa kulipwa na kampuni hiyo kwa ajili ya watumishi wake wa ngazi za juu tangu Septemba 2015 hadi Julai 2018.

Hadi wakati ukaguzi huo unafanyika, sababu za wafanyakazi hao ambao kwa idadi kubwa ni raia wa kigeni kuondolewa kwenye makato ya PAYE na kodi nyingine ambazo zilibainika kutolipwa, hazijawekwa wazi.

Akizungumzia sakata hilo, Kaimu Meneja wa Mamlaka ya Mapato (TRA) Mkoa wa Kodi Ilala, Stephano Kauzeni, amesema walipata taarifa ya kampuni hiyo kuwaondoa wafanyakazi wake kwenye orodha ya wanaopaswa kulipa PAYE na kuifanyia kazi kupitia kitengo chao cha ukaguzi wa mapato ya ndani na kubaini kuwa taasisi hiyo ilikuwa na wafanyakazi wasiolipa kodi.

“Hii taasisi ni ya watu wa Marekani, ninaifahamu, kwa hapa nchini inafahamika kama MSPH Tanzania LLC, suala lake wameshakuja watu zaidi ya watano kuulizia, na wewe ni mtu wa sita.

“Nikueleze tu, hawa walifanyiwa ukaguzi na wataalamu wetu wa kodi na tukayabaini madudu hayo na tulichukua hatua ya kuwaandikia barua ya kuwachukulia hatua,” amesema Kauzeni.

Lakini amesema jitihada zao za kudai kodi hiyo zimegonga mwamba kwa sababu taasisi hiyo inaeleza kuwa walikwisha kupewa msamaha wa kodi na serikali.

“Wanasema kuwa baada ya kuingia nchini miaka ya 1990 waliingia makubaliano na serikali ya kufanya kazi bila wafanyakazi wake, hasa raia wa kigeni wanaochaguliwa kuongoza taasisi hiyo kutotozwa kodi,” amesema kaimu meneja huyo.

Kwa mujibu wa taratibu, serikali inapotoa msamaha wa kodi kama huo inapaswa kulitangaza suala hilo katika Gazeti la Serikali. Lengo la kufanya hivyo ni kuzijulisha taasisi zinazohusika na masuala ya ukusanyaji wa kodi ili wasiwabughudhi waliosamehewa, pia isiweke makadirio ya kodi hizo katika hesabu zao.

Kauzeni amesema walipoipatia taasisi hiyo barua ya kuwadai kodi hiyo walipinga na wakaamua kwenda kwenye bodi ya usuluhishi wa mambo ya kodi na baadaye kufungua kesi Mahakama Kuu kupinga madai hayo.

Ripoti ya ukaguzi ya TRA inabainisha kuwa kuondolewa kwa wafanyakazi hao kwenye makato ya PAYE ni kinyume cha Sheria ya Kodi ya mwaka 2004, Kifungu cha 81, ambacho kinamtaka mwajiri kuzingatia makato ya kodi kutoka kwenye pato la mshahara wa mfanyakazi wake.

Ukaguzi wa TRA ulibaini kuwa raia wa kigeni ambao hawakulipa kodi hiyo ya mishahara kuwa ni pamoja na mwakilishi wa ICAP nchini, Fernando Morales, raia wa Argentina, ambaye bado anaendelea kulitumikia shirika hilo hapa nchini.

Wengine ni Wessen Nenga kutoka Ethiopia, Claire Stainer raia wa Australia, Veronica Mugisha raia wa Uganda, Haruka Maruyama raia wa Japan na Elisaphane Mnyazesa raia wa Rwanda ambao wote kwa pamoja wanatajwa kuondoka nchini bila kulipa kodi hadi mikataba yao inafikia ukomo.

Viwango vya mishahara ya wafanyakazi hao ambavyo havikukatwa kodi ya pato la mshahara wa kila mwezi ni pamoja na Fernando Morales anayelipwa Dola za Marekani 12,580 kwa mwezi, ambazo kwa fedha ya Tanzania ni zaidi ya Sh milioni 28 na posho ya kila mwezi dola za Marekani 3,774 ambazo ni zaidi ya Sh milioni 8 za Tanzania.

Claire Stainer ambaye mshahara wake ulikuwa dola za Marekani 2,708 sawa na takriban Sh milioni 6 za Tanzania na posho ya kila mwezi ya dola 813 sawa na Sh milioni 1.7 za Tanzania na Huruka Maruyama ambaye mshahara wake ulikuwa dola za Marekani 6,350 sawa na Sh milioni 14 na posho ya dola 1,905 kila mwezi sawa na Sh milioni 4.

Wesseni Nenga raia wa Ethiopia alikuwa analipwa mshahara wa dola za Marekani 4,335 kila mwezi sawa na Sh milioni 9.5 na posho ya dola za Marekani 1,301 kila mwezi sawa na Sh milioni 2.6.

Baadhi ya wafanyakazi wazawa katika taasisi hiyo wamelieleza Gazeti la JAMHURI kuwa wanashangazwa na kitendo cha wafanyakazi hao wageni kutolipa kodi huku wao wakikatwa kodi hizo kila mwezi.

Wafanyakazi hao wanatilia shaka kuondolewa kwa raia hao wa kigeni kwenye makato ya PAYE kuwa mchezo unaowahusisha vigogo wachache wa TRA.

Wanahoji ilikuwaje wafanyakazi hao wa ngazi ya juu waondolewe mwaka 2015 kwenye PAYE ilhali ripoti hiyo inaonyesha raia hao walikuwa wachangiaji wazuri wa pato hilo tangu mwaka 2013.

Mmoja wa wafanyakazi hao (jina linahifadhiwa) amesema: “Inashangaza kuwa TRA Ilala walifanya ukaguzi na kubaini madudu yote lakini hadi sasa hakuna hatua zozote zilizochukuliwa… kuna michezo inafanyika brother,” amesema.

Hata hivyo Kaimu Meneja Kauzeni anakanusha maofisa wa TRA kuhusika na msamaha wa kodi kwa watumishi hao na kubainisha kuwa kama msamaha huo ungekuwa umetolewa na Mamlaka hiyo isingegeuka na kuanza kuidai taasisi hiyo kodi.

“Kumbuka kuwa watu hawa wamekwenda mahakamani kupinga kodi ambayo TRA inawadai. Lingekuwa jambo la ajabu kama tungekuwa tumewasamehe kodi na kisha kurudi kuwadai tena kodi ambayo tuliisamehe,” amefafanua.

By Jamhuri