Kila mara tukiwa na mijadala ya maana, katikati hujitokeza upepo wa kutuyumbisha. Tukiwa bado kwenye mjadala wa athari za mabadiliko ya tabia nchi zilizosababisha upungufu wa maji jijini Dar es Salaam, kumeibuka mjadala mwingine wa ‘nani ni nani?’

Sikuona sababu ya kung’ang’ana na mjadala ambao mwanzilishi wake alishakiri hadharani, tena kitambo tu kwamba ana jalada Mirembe. 

Kwa wasiojua, Mirembe hakuna majalada ya kesi za jinai! Hakuna migogoro ya ardhi. Kuna majalada ya wagonjwa wa afya ya akili. Hilo pekee lilitosha kuua mjadala huo.

Wapo wanaoamini kwamba vita kuu ya tatu ya dunia huenda chanzo chake kikawa ugomvi wa rasilimali maji. Kuna minong’ono ya kwamba vurugu zinazoendelea Ethiopia zina mkono wa Misri ambayo ni miongoni mwa wanufaika wakuu wa maji ya Mto Nile. Ethiopia ilikaidi mwito wa Misri na Marekani juu ya ujenzi wa bwawa hilo wa thamani ya dola bilioni 5 za Marekani.

Nitarejea nyuma kidogo: Wakati wa Awamu ya Tatu, wakati huo Edward Lowassa akiwa Waziri wa Maji na Mifugo, nilipata fursa ya kuwa miongoni mwa wanahabari tuliozuru Misri. Lengo kuu la ziara lilikuwa kujenga uhusiano kati ya Misri na Tanzania kutokana na msimamo wetu wa kutoa maji Ziwa Victoria hadi Shinyanga.

Misri ina wasomi wengi, lakini maeneo mawili yametia fora – kwenye maji na jeshi. Lowassa alipata mapokezi makubwa. Kwenye mkutano na waandishi wa habari, nasi tukiwa tumejipanga, ninakumbuka tulimuuliza swali Waziri wa Maji wa wakati huo, Dk. Mahmoud Abu-Zeid, akashindwa kulijibu. 

Swali lenyewe lilitokana na taarifa zetu za kikachero kwamba Misri imehifadhi chini ya ardhi maji mengi kiasi kwamba endapo Mto Nile utakauka, hifadhi waliyonayo itawafaa kwa miongo mitano hadi 10. Walishituka mno kuona Watanzania tunayo siri hiyo.

Wamisri wanaijua Tanzania kweli kweli. Mwandishi mmoja alipomuuliza swali Lowassa, alitaja mito takriban 10 anayoijua nchini Tanzania. 

Akatushangaa tunavyoiacha na kushupalia maji ya Ziwa Victoria! Akauliza ni kwanini tusitumie mito hiyo kuwapelekea wananchi maji, badala ya kuhangaika na maji ya Ziwa Victoria ambayo wao wanayahitaji zaidi. 

Kwa ujasiri wa aina yake, Lowassa akasema Tanzania ni nchi huru, hivyo haiwezi kuheshimu mikataba iliyowekwa na Waingereza ambayo kabla ya Uhuru, Mwalimu Julius Nyerere alishatangaza msimamo wa kutoitambua. Akasema Tanzania itawapa wananchi na mifugo yake maji, na iko tayari kwa lolote (hata kama ni vita). Ukumbi mzima ukawa kama umemwagiwa maji.

Katika ziara hiyo tulizuru maeneo mengi, lakini kwa muktadha wa makala hii ninaomba nizungumzie Bwawa la Aswan lililoko kusini mwa nchi hiyo na kaskazini kwa Sudan. 

Ukubwa wa bwawa hili umelifanya liwe sehemu ya kivutio cha utalii kwa wageni wa ndani na nje. Kumejengwa mnara wenye lifti unaotumika kufaidi mandhari murua. Kuna ufugaji samaki wengi. Linatumika kwa umwagiliaji, na linatumika kama nyenzo ya kupunguza makali ya mafuriko pindi mto Nile unapofurika.

Bwawa la Aswan kwa Misri ni uchumi hasa. Japo inatangazwa kuwa lilijengwa ili kuzalisha umeme, hiyo ni gelesha tu. Umeme wa Misri unazalishwa kwa kutumia mafuta. 

Aswan inazalisha megawati 2,100 za umeme pekee. Mwaka 2015 mchango wake wa umeme kwenye gridi ya nchi hiyo ulikuwa ni asilimia 5.68. 

Hii inathibitisha kuwa Aswan si kwa ajili ya umeme, bali ni kwa kilimo na akiba ya baadaye endapo Misri itakabiliwa na ukame au shida yoyote kutokana na migogoro na nchi wadau wa Mto Nile. Kwenye kilimo, maji ya Aswan yanatumika kustawisha mazao katika eneo la takriban kilometa za mraba 33,000. Hili ni eneo kubwa sana.

Sasa tuje kwetu Tanzania kusikokoma vituko: Nimewasikia wasomi wetu wakisema Dar es Salaam haipaswi kupata shida ya maji kwa sababu serikali inaweza ikachimba visima na kufaidi maji yaliyotuama ardhini kwa miaka 1,000! Tena wametolea mfano wa Zanzibar wanaotumia maji ya visima kwa miaka yote! Niliposoma taarifa hii ndipo nikapata nguvu za kuandika.

Ushauri huu ni mbaya. Kwa kuwa umetolewa hadharani, ngoja tuukosoe hadharani.. Kunradhi, ashakumu si matusi mniruhusu niseme huu ni ushauri wa hovyo – usiostahili kutolewa na mtu msomi. Nikirejea mfano wa Misri, hakuna mtu au taasisi inayoruhusiwa kuchimba kisima bila kibali. Vibali vichache vinavyotolewa, vinatolewa na serikali kuu pekee. Wanafanya hivyo ili kuhifadhi maji ya ardhini kwa lengo la kuwafaa kwa miaka ijayo ya ukame na shida nyingine.

Kwa kuwakumbusha tu ‘wasomi’ wetu hawa, miaka ya 1960 na 1970 Mwalimu alikataa msaada wa Misri wa kutuchimbia visima vya maji pale walipobaini ana mpango wa kutumia maji ya Ziwa Victoria kupeleka huduma hiyo mikoa yenye ukame kama Singida. 

Mwalimu alijua maji ya ardhini ni akiba isiyostahili kuguswa kwa vurugu kwa kizazi hiki. Haya ni mawazo ya kiongozi aliyewaza maisha ya kizazi kijacho. Anayehimiza visima leo ni mbinafsi.

Mtaalamu wa Tanzania anayeshauri visima vichimbwe hasa kwa eneo kama Dar es Salaam huyo hafai hata kidogo. Ni wa kupuuzwa ushauri wake, maana hauna tija kwa maeneo kama Dar es Salaam.

Tangu Awamu ya Kwanza, uongozi wa nchi umeshauriwa lijengwe Bwawa la Kidunda. Miaka 60 bado mpango huo haujatekelezwa. 

Bonde la Mto Ruvu ambalo hufurika maji kwa msimu, sasa pale Mlandizi kunajengwa makuta tu ya viwanda kana kwamba ardhi imekwisha katika nchi hii. Eneo kama lile ni la kujengwa bwawa kubwa ili litumike kwa kilimo na ufugaji wa samaki.

Msomi anayetazama maji wakati wa mvua yakiishia baharini kisha akashauri nchi ichimbe visima hatufai.

Maji ya ardhini si ya kuguswa bila mpangilio. Hatuna sababu ya kuyagusa sasa. Tuna maji mengi yanayopotea baharini. Tuyatumie hayo kwa kuyahifadhi kwenye mabwawa. 

Yaliyo ardhini yabaki akiba, maana kwa mwenendo huu huenda dunia ikaishiwa maji. Tujenge mabwawa kwa ngazi za kaya, vitongozi, vijiji, mitaa, kata, tarafa, wilaya, mikoa na taifa. 

Tuwe na mabwawa mengi kadiri inavyowezekana ili yasaidie shughuli za kilimo na ufugaji wa samaki. Katika nyumba zetu kuwepo bylaw kuhakikisha kila mwenye nyumba anakuwa na hifadhi ya maji yanayotoka kwenye paa au mapaa yao. 

Hili linawezekana kabisa, maana wenzetu huko duniani leo maji hayamwagwi yakapotea. Maji ya chooni yanakuwa recycled na kurejea tena kuwa ya kunywa na kazi nyingine.

Naushauri uongozi wa nchi usiweke kipaumbele kwenye visima. Tutumie kwanza haya yanayomwagika baharini bila mpangilio. 

Kwa wanaoshauri uchimbaji wa visima kama ajenda ya kitaifa, ushauri wangu ni mmoja – wapuuzwe. Hawa ndio wanaoikwamisha Afrika na kuwafanya watu wake waishi kwa kutegemea zaidi miujiza ya makanisani.

Hatuwezi kuwa wazembe kiasi hiki kwa kuacha maji yaishie baharini halafu tuitane kwenye ibada kuomba mvua ili tupate maji! 

Mungu tunamtwika mizigo asiyostahili ilhali akili na maarifa alivyotupatia tumefeli kuvitumia. Matatizo yetu yasimalizwe kwa njia za mkato. 

Visima ni njia za mkato za dhuluma kwa kizazi kijacho. Walimwengu wanapotuona tukilia kiu ya maji ilhali tukiyaangalia yote yakiingia baharini, wana haki ya kutupatia matusi yoyote wanayoona yanatufaa. Tusikubali kutukanwa. Lakini hatuwezi kutoka hapa kwa akili na ushauri wa hao wanaoitwa wasomi! Tanzania na Afrika tuamke sasa. Udhaifu wetu tusimsingizie Mungu.