Vita ya Uhuru wa Marekani ilipiganwa kati ya Waingereza na walowezi wa makoloni yake 13  kwenye pwani ya Amerika ya Kaskazini katika miaka 1775 hadi 1783.

Jeshi la walowezi lililoongozwa na George Washington na wengine lilishinda Jeshi la Dola la Uingereza kwa msaada wa Ufaransa. Makoloni hayo yakapata Uhuru kama Muungano wa Madola ya Amerika au Marekani.

Sababu za vita

Vita ilitokea kutokana na kutoelewana kati ya dola ya Uingereza na walowezi wa Amerika ya Kaskazini. Uingereza ilikuwa na makoloni 13 Marekani na ilitawaliwa na wahamiaji kutoka Uingereza. Serikali ya Uingereza ilitawala maeneo hayo kwa kutumia magavana na wanajeshi wake.

 

Sheria zilitungwa London na zilikataza kuanzishwa kwa viwanda kwenye makoloni yote 13. Hivyo, walowezi walilazimishwa kununua bidhaa nyingi kutoka Uingereza kwa bei ya juu. Baada ya vita ya miaka saba, Uingereza ilihitaji fedha, kwa hiyo iliongeza kodi kwa bidhaa zilizosafirishwa kati ya makoloni na nchi mama.

 

Kwa vile Walowezi hawakupendezwa na kodi za nyongeza, walidai kupewa wawakilishi katika Bunge la London na nafasi ya kushiriki katika maazimio juu ya sheria zilizowaathiri. Walitangaza wito Wa ‘No taxation without representation’ (hakuna kama hakuna uwakilishi).

 

Mwaka 1767 Bunge la Uingereza lilikataa maombi ya wakoloni na badala yake idadi ya wanajeshi iliongezeka katika koloni. Kwa sababu hizo wakoloni wengi walijisikia vibaya kwa madai ya kuwa wanadharauliwa, wakaongeza ukali wa upinzani.

 

Mwaka 1773 umati mkubwa ulishiriki katika tukio la Boston Tea Party, wakatupa mizigo ya majani ya chai kwenye bandari ya Boston kwa kuonesha upinzani wao dhidi ya kodi ya Waingereza. Waingereza walijibu mapigo mwaka 1774 kwa kutunga sheria mpya kali, na wanajeshi wao walianza kukusanya akiba za baruti katika makoloni.

 

Hatua hiyo iliongeza uchungu na wanamgambo kati ya wakoloni walianza kufanya mazoezi ya kijeshi. Viongozi wao wakaitisha mkutano wa kwanza wa wawakilishi kutoka makoloni yote. Makoloni hayo ni Connecticut, Delaware,  Georgia, Maryland, Massachusetts, New Hampshire, New Jersey, New York, North Carolina, Pennsylvania, Rhode Island, South Carolina na Virginia.

 

Kwa pamoja waliamua kukataa biashara yoyote na Uingereza kwa muda wa mwaka mmoja hadi madai yao ya kupunguza kodi yatakapokubaliwa pia wakaanza kufanya mazoezi ya wanamgambo bila usimamizi wa Waingereza.  Mwaka 1775 Waingereza walitangaza Koloni la Massachusetts kuwa eneo la waasi na sheria ya kukataza wavuvi kutoka Marekani kuvua samaki katika Bahari ya Atlantiki.

 

Mwanzo wa vita

Jaribio la wanajeshi wa kifalme kukamata tena akiba za baruti kati ya walowezi, lilisababisha mapigano ya kwanza ya kijeshi Aprili  19, 1775 karibu na Mji wa Boston. Wanajeshi wa Kiingereza walipigana katika mapambano makali na wanamgambo kwenye Kijiji cha Lexington na wanamgambo wanane  waliuawa.

 

Mapigano yalisambaa pia kwenye vijiji vya karibu na Lexington.

Wanamgambo wengi walifika Boston wakawazuia Waingereza wasitoke ndani ya mji. Baada ya wiki mbili, Waingereza walijaribu kuwafukuza na mapigano ya Bunker Hill nje ya Boston yalitokea. Hayo yalikuwa mapigano makubwa ya kwanza. Waingereza walishinda lakini walipoteza wanajeshi 226 na wanamgambo 140.

 

Vita na Uhuru

Mwanzoni, Waingereza walikuwa na silaha na wanajeshi zaidi wakasonga mbele. Lakini wanamgambo kutoka katika upande wa walowezi wakiongozwa na George Washington walikuwa imara  na kuongeza mashambulizi dhidi ya Waingereza.

 

Julai 4, 1776 wawakilishi kutoka makoloni yote walitangaza Uhuru wa Muungano wa Madola ya Amerika. Hata hivyo, bado Waingereza walisonga mbele na kuutwaa mji wa New York. Mwaka 1777, Ufaransa ilianza kwa siri kuwasaidia Wamarekani kwa kutuma silaha kwa Wamarekani. Mwaka 1778 Hispania na Uholanzi nazo ziliungana na kutangaza vita dhidi ya Uingereza. Manowari za Ufaransa zilishambulia meli za Waingereza zilipeleka silaha na askari kwenda Marekani.

 

Mwaka 1781 sehemu kubwa ya Jeshi la Uingereza ilishindwa kwenye mji wa Yorktown wakalazimika kujisalimisha. Tangu siku hiyo mapigano yalipungua na mwaka 1783 Uingereza ilikukubali kutoa  Uhuru kwa makoloni yake ya awali. Wakazi wengi katika makoloni hayo walioendelea kusimama upande wa Uingereza, wakahamia Canada iliyoendelea kuwa Koloni la Uingereza.

 

Vita ya wenyewe kwa wenyewe

Vita hii ilihusisha majimbo ya Kaskazini na yale ya  Kusini ya Marekani,   iliyopiganwa mwaka 1861 hadi mwaka 1865, ikiwa ni vita ya wenyewe kwa wenyewe nchini, kati ya Majimbo ya Kusini (Shirikisho la Madola ya Amerika) na majimbo ya Kaskazini (Maungano ya Madola ya Amerika).

 

Sababu kubwa aya vita hiyo ilikuwa kuhusu suala la utumwa. Kundi la Majimbo ya Kusini lilijiengua kutoka muungano wa madola ya Amerika na kuunda Shirikisho la Madola ya Amerika. Majimbo ya Kaskazini yalipiga marufuku utumwa lakini Majimbo ya Kusini yaliendelea na sheria zilizoruhusu utumwa kwa kuwa matajiri wengi wa Kusini walitegemea kazi za watumwa.

 

Sababu nyingine zilikuwa tofauti za kiuchumi. Majimbo ya Kaskazini yalikuwa na viwanda na miji mingi mikubwa lakini uchumi wa Kusini ulikuwa hasa kilimo kilichokuwa kikiendeshwa na  watumwa.

 

Uchaguzi wa mwanasiasa Abraham Lincoln aliyekuwa mpinzani mkubwa wa utumwa na baadaye kuwa Rais wa Marekani, ulihafanikisha mapigano hayo. Vita ilipiganwa kwa muda mrefu na watu 650,000 walipoteza maisha na Majimbo ya Kaskazini yalishinda vita hiyo.

 

George Washington ni nani

George Washington aliyekuwa Rais wa Kwanza wa Marekani kati ya mwaka 1789 na mwaka 1797,  alizaliwa Februari 22, 1732 na kufariki Desemba 14, 1799. Alikuwa mwanasiasa na kiongozi wa kijeshi.

 

Mtoto na kijana

Alizaliwa akiwa mtoto wa pili wa mlowezi Augustine Washington katika Koloni la Virginia, lililokuwa mali ya Mfalme wa Uingereza. Wazazi  wake walikuwa na shamba kubwa lililolimwa na watumwa wa Kiafrika. George alisoma shule miaka michache lakini hakuendelea kielimu. Baada ya shule alianza kazi ya upimaji na ramani.

 

Mkulima na Kiongozi wa Kijeshi

Baada ya kifo cha kaka yake, alirithi shamba kubwa pamoja na watumwa akawa mkulima tajiri. Alikuwa msimazi wa wanamgambo waliokuwa kikosi cha jeshi la hiari waliotakiwa kusaidiana na wanajeshi wa Kiingereza kutetea koloni dhidi ya majirani Wahindi na Wafaransa walioenea eneo la kusini kutoka katika koloni lao la Canada – Quebec.

 

Katika umri mdogo wa miaka 22, Washington alijikuta kama Mkuu wa Wanamgambo katika vita ya Uingereza dhidi ya Wafaransa na Wahindi iliyopanuka baadaye na kudumu kwa  miaka saba. Aliongoza kikosi chake dhidi ya maadui na akafaulu mara kadhaa.

 

Baadaye alishirikiana na jeshi rasmi la Uingereza katika mapigano ya Monongahela na kuongoza mabaki ya jeshi baada ya kifo cha Jemadari Mwingereza.

 

Mwaka 1755 akawa Mkuu wa Jeshi la Koloni la Virginia. Lakini baada ya ushindi Waingereza walikataa kumpa cheo katika Jeshi la Mfalme, hivyo akajiuzulu  na kurudi katika shamba lake na kurudia mambo ya siasa kwenye bunge la koloni. Mwaka 1759 Washington alimwoa mjane tajiri akawa kati ya matajiri sana  wa Virginia.

 

Mapinduzi

Baada ya vita ya miaka saba, uhusiano kati ya Uingereza na walowezi Waingereza katika makoloni yake 13 ya Amerika ya Kaskazini ukazorota.

 

Tangu 1773 Waingereza walitumia sheria ya dharura na nguvu ya kijeshi mjini Boston. Wawakilishi wa makoloni yote 13 wakakutana kama bunge la Amerika na Washington alikuwa miongoni mwao. Baada ya mapigano ya kwanza kati ya wanajeshi Waingereza na wanamgambo wa walowezi, bunge likaamua kuunda jeshi la pamoja la makoloni yote na Washington akateuliwa kuwa Jemadari Mkuu. Aliongoza Jeshi la Marekani katika vita ya Uhuru wa Marekani dhidi ya Uingereza hadi mwaka 1783.

 

Baada ya vita: Mwanasiasa na rais

Baada ya vita ya Uhuru ya Marekani, Geroge Washington alirudi kijijini kwake kuendelea na kilimo, lakini alichaguliwa pia kuwa mwakilishi wa Virginia katika Bunge la Katiba la Marekani mwaka 1787 akawa mwenyekiti wa mkutano huo uliokubali Katiba ya Marekani. 4 Februari 1789 alichaguliwa kuwa Rais wa kwanza wa Marekani na kurudishwa katika kipindi kingine mwaka 1789. Baada ya kipindi chake cha pili alikataa kusimama tena, akaunda utaratibu wa kwamba rais anaweza kurudishwa mara moja tu hawezi kuendelea zaidi.

 

Uzee

Mwaka 1797 akarudi tena shambani na kusimamia kilimo kilichoendeshwa na watumwa 390. Desemba 14 alikufa nyumbani kwake. Kabla ya kuaga dunia, aliamuru katika usia wake  kwamba watumwa wake wote warudishiwe uhuru wao baada ya kifo chake yeye mwenyewe na mke wake. Mji Mkuu wa Marekani, Washington, D.C. na Jimbo la Washington umeitwa jina lake pia picha yake iko kwenye noti ya dola moja.

 

Seneti (Marekani)

Bunge la Muungano wa madola ya Amerika linaitwa Seneti. Neno hilo limetokana na neno la Kilatini “senatus” yaana Baraza la Wazee. Wabunge wake huitwa Maseneta. Kila jimbo kwenye Shirikisho la Maungano ya Madola ya Amerika linachagua maseneta wawili kwa kipindi cha miaka sita bila kubagua kati ya majimbo.

 

Kuchaguliwa kwa maseneta hao hakuangaliwi kwa ukubwa wa jimbo, mfano Jimbo la Wyoming lenye wakazi nusu milioni, lina maseneta wawili sawa na Jimbo la California lenye wakazi milioni 37. Idadi ya majimbo ya Marekani ni 50, hivyo kuna maseneta 100. Uchaguzi haufanyiki kwa pamoja kwa wote, lakini theluthi moja inachaguliwa kila baada ya miaka miwili.

 

Pamoja na sehemu nyingine ya bunge yaani Baraza la Wawakilishi, Seneti inaamua juu ya sheria zinazopaswa kupita pande zote mbili. Seneti ina jukumu la kuamua juu ya vita na amani. Rais anapaswa kupata kibali cha seneti kabla ya kuita maafisa muhimu kama mawaziri na mahakimu wa Mahakama Kuu ya Kitaifa. Seneta anapaswa kuwa na umri wa angalau miaka 30 na kuwa raia wa Marekani tangu miaka akiwa na umri wa miaka 9 au zaidi.

 

Dola ya Marekani

Fedha ya Marekani ni dola (USD), ambayo ni fedha halali ya nchi hiyo. Alama yake ni USD au mara nyingi $. Dola ya Marekani inapatikana kwa noti za dola 1, 2, 5, 10, 20, 50 na 100. Kuna pia sarafu ya dola 1. Dola moja ina senti 100. Senti huitwa pia ‘penny’ nchini Marekani. Kuna sarafu za nusu dola (senti 50), robo dola (senti 25) na sarafu za senti 10 (dime), 5 (nickel) na 1 (penny).

 

Hadi 1969 noti ya dola ya Marekani ilikuwa na ahadi ya kwamba Serikali ya Marekani atampatia kila mtu dhahabu kulingana na thamani ya dola hizi akipenda kuibadilisha. Usawa huu na thamani ya dhahabu ulifutwa. Leo  dola ya Marekani ni fedha ya kuiaminika. Maana yake watumiaji husadiki ya kwamba serikali haitachapisha dola kushinda uwezo wa uchumi na thamani ya bidhaa zilizopo nchini.

 

Tangu mwisho mwa Vita Kuu ya Pili ya Dunia mwaka 1945, dola ya Marekani imekuwa fedha kuu duniani na sehemu kubwa ya biashara ya kimataifa hukadiriwa kwa bei za dola hizi. Lakini tangu kupatikana kwa euro mwaka 1999, umuhimu wa dola ya Marekani umeanza kupungua polepole.

 

Pearl Harbor

Pearl Harbor (Bandari ya Lulu) au Pu’uloa kwa Kihawaii ni bandari ya kijeshi ya Marekani kwenye kisiwa cha Oahu katika jimbo la visiwani la Hawaii (Marekani).

 

Kituo hiki cha kijeshi kipo ndani ya iliyo bandari asilia, ambako meli na manowari zinafunga gati kwa usalama wakati wa dhoruba. Katikati ya kidaka, kuna kisiwa kinachoitwa Ford Island ambayo ni Kitovu cha Kituo cha Kijeshi. Tangu Marekani kuitwaa Hawaii wakati wa vita ya Marekani dhidi Hispania mwaka 1898, bandari hii ilikuwa Makao Makuu ya Kundi la Manowari za Marekani katika Bahari Pasifiki.

 

Pearl Harbor ilikuwa maarufu kutokana na mashambulio ya ghafla ya Japani dhidi ya manowari za Marekani yaliyotokea Desemba 7, 1941. Hatua hii ilisababisha Marekani kuingia katika Vita Kuu ya Pili ya Dunia na kujiunga rasmi na mataifa ya ushirikiano.

Siku kabla ya  Desemba 7, wanamaji wa Japan walifaulu kukaribia fungu visiwa na kundi la manowari pamoja na manowari-ndege 6, ndege 350 kutoka manowari-ndege hizo zilishambulia Pearl Harbor zikafaulu kuzamisha manowari 9 na kuleta uharibifu mkubwa kwa manowari 21 nyingine, tatu kati hizi hazikuweza kutengenezeka tena. Wamarekani 2,350 waliuawa. Pia ndege nyingi za kijeshi za Marekani ziliangamizwa.

 

Shabaha ya shambulio la Japan ilikuwa kuharibu uwezo wa manowari za Marekani kuingilia katika upanuzi wa Mamlaka ya Japani katika Pasifiki hasa kwenye maeneo chini ya utawala wa Uingereza, Uholanzi, Ufaransa na China. Lakini shambulio halikugusa kituo cha nyambizi, akiba za fueli, karahana za kijeshi na ofisi za viongozi vya jeshi.

 

Pia manowari-ndege zilizokuwa sehemu ya kundi ya Pearl Harbor hazikuharibiwa kwa sababu zote tatu hazikuwapo Hawaii wakati wa shambulio. Kwa hiyo, uwezo wa Pearl Harbor kuhudumia kundi la manowari haukuharibiwa na baadaye Marekani ilitumia kituo hiki pamoja na Visiwa vya Hawaii kama msingi wa vita yake dhidi Japani.

 

Vita ya miaka saba ilitokea kati ya 1756 hadi 1763. Ilianza kutokana na mashindano ya nchi za Ulaya ikasambaa pande nyingi za dunia. Hivyo imeitwa “Vita Kuu ya kwanza ya Dunia hata kama jina hili kwa kawaida latumiwa kwa ajili ya vita kati ya 1914 na 1918.

 

Washiriki

 

Washiriki katika vita hiyo walikuwa nchi za Ulaya na makoloni yao pia watu wa sehemu mbalimbali za dunia walioshikamana nao. Nchi za Ujerumani, Prussia na Hannover pamoja na Uingereza na makoloni yake Marekani na Asia upande mmoja, wakati nchi za Austria na Saksonia pamoja na Urusi, Uswisi na Ufaransa pamoja na makoloni yake Marekani na Uhindi. Ureno na Hispania zilivutwa baadaye, pia Waholanzi ambao hawakushiriki katika vita walishambuliwa katika Uhindi.

 

Sababu za vita

Vita ilitokea kwa sababu mbili hasa Amerika ya Kaskazini Ufaransa na Uingereza zilishindana kuhusu upanuzi wa maeneo yao. Katika Ulaya Prussia iliwahi kutwaa jimbo la Silesia kutoka Austria na Austria ilitaka kuchukua jimbo hilo tena. Nchi nyingi za Ulaya ziliogopa uwezo mkubwa mno wa nchi nyingine, ikiruhusiwa kushinda vita hiyo, ziliamua kuingilia kati mashindano na hofu hizi zilisababisha kutokea kwa kambi hizi mbili kubwa.

 

Mapigano

Mapigano yalitokea katika Ulaya hasa Ujerumani, halafu katika Uhindi, Amerika ya Kaskazini, kwenye Visiwa vya Karibi, Pwani za Afrika na Ufilipino. Uingereza ilitwaa “Ufaransa mpya” au sehemu ya Kifaransa ya Canada ya leo na kuwafukuwa Wafaransa katika maeneo ya magharibi ya makoloni zao.

 

Katika Karibi, Waingereza walitwaa visiwa vingi vya Wafaransa isipokuwa Martinique na Guadeloupe. Katika Uhindi vituo vya Ufaransa vingi vilitwaliwa isipokuwa Pondicherry iliyobaki kama koloni dogo la Ufaransa (hadi 1960).

 

Waingereza kwa kutoa kipaumbele katika Ubengali, waliweka msingi wa utawala wao wa baadaye juu ya Uhindi wote. Katika Afrika, Waingereza walitwaa Kituo cha St. Louis nchini Senegal kutoka Ufaransa (ilirudishwa baada ya vita)

 

Prussia ilitetea Jimbo la Silesia dhidi ya Austria ikapata sifa nyingi kwa sababu jeshi lake lilishindana na Waaustria, Warusi na Wafaransa wakati moja. Lakini mwaka 1762 nguvu za Prussia zilikwisha ikaelekea kushindwa. Iliokolewa kwa sababu malkia Elizabeth wa Urusi alikufa na mfalme mpya Peter III alimpenda mfalme wa Prussia, akaamua kupatana amani naye badala ya kumshambulia tena.  Hivyo Austria ikabaki kama mpinzani wa pekee ikashindwa.

 

Matokeo makuu ya vita yalikuwa, Uingereza ilikuwa nchi yenye makoloni mengi duniani baada ya Hispania ikaelekea kuipita. Pia ilitawala bahari za dunia kwa ilikuwa taifa lenye manowari nyingi na vituo pamoja na bandari kwenye mabara yote. Uwezo wa Ufaransa ulipunguzwa ikipoteza makoloni yake katika Amerika ya Kaskazini na kubaki na maeneo madogo tu katika Karibi na Uhindi. Prussia ilitoka vitani kama nchi muhimu ya tano ya Ulaya pamoja na Ufaransa, Austria, Uingereza, na Urusi.

 

Matokeo ya baadaye

Msingi wa Kiingereza kuwa lugha ya kwanza duniani, uliwekwa kwa sababu kilitumiwa kote katika makoloni ya Uingereza.  Ushindi wa Uingereza ulikuwa msingi kwa ajili ya mapinduzi na uhuru wa Marekani miaka 13 baadaye. Walowezi walijifunza mitindo ya vita waliposhiriki katika vita upande wa Uingereza na walitumia ujuzi huo baadaye dhidi ya Uingereza.

 

Kuondolewa kwa Ufaransa kulipungua vizuizi dhidi ya upanuzi wa Marekani katika Amerika ya kaskazini. Uadui wa Ufaransa dhidi ya Uingereza ulibaki ukaimarishwa na kusababisha usaidizi wa Ufaransa kwa waasi wa Amerika ya Kaskazini mwaka 1776, hivyo kuzaliwa kwa taifa jipya la Marekani.

 

Kudhoofishwa kwa Ufaransa kwa sababu ya gharama kubwa ya vita na gharama ya kusaidia Wamarekani baadaye, uliathiri uchumi na sifa za utawala wa kifalme na kuwa sababu muhimu ya mapinduzi ya kifaransa. Ushindi wa Prussia ulisababisha mashindano ya mfululizo kati Prussia na Austria juu ya kipaumbele katika Ujerumani yaliyoonekana baadaye hadi vita ya 1866.

 

Vita ya Marekani dhidi Hispania ilitokea mwaka 1898. Ilianza kwa shambulio la Marekani Aprili 25 mwaka huo dhidi ya Puerto Rico lililokuwa koloni la Hispania na kumalizika Agosti 12, 1898 Jeshi la Hispania katika Manila (Ufilipino) lilipojisalimisha. Marekani ilitwaa makoloni ya Hispania ya Puerto Rico, Cuba na Ufilipino. Vita hiyo ilikuwa mwanzo wa Marekani kufuata siasa ya nje ya upanuzi hata katika maeneo ya mbali.

 

Kabla ya vita hii, Marekani ilishughulika kupanua eneo lake kwenye bara la Amerika ya Kaskazini dhidi ya wenyeji asilia na dhidi ya Mexico. Marekani ilitumia nafasi ya ghasia ya wenyeji wa Cuba dhidi ya utawala wa kikoloni ya Hispania.

 

Baada ya mlipuko kwenye manowari ya Marekani ya USS Maine katika Bandari ya Havana, Marekani ilitangaza vita dhidi ya Hispania ingawa sababu ya mlipuko haikujulikana hadi leo ilikuwa nini. Hispania haikuweza kushindana na manowari na silaha za Marekani zilizokuwa zimeendelea kiteknolojia. Pia Marekani ilikuwa karibu na mahali pa vita na Hispania ilishindwa kuongeza wanajeshi au silaha.

 

Vita ya Korea kati ya 1950 na 1953

Ilianzishwa na Korea ya Kaskazini iliyovamia Korea ya Kusini. Korea ya Kaskazini ilisaidiwa na Jamhuri ya Watu wa China na Umoja wa Kisovieti. Korea ya Kusini ilisaidiwa na Marekani hasa. Lakini Marekani ilishiriki katika vita hiyo kwa jina la Umoja wa Mataifa pamoja na wanajeshi wa nchi 16.

 

Shambulio la Kaskazini

Katika awamu ya kwanza kuanzia mwezi Mei 1950, Jeshi la Kaskazini lilivamia Korea ya Kusini likateka mji mkuu wa Seoul na kusukuma watetezi hadi Kusini ya Rasi ya Korea Agosti/Septemba 1950 likiwa eneo la Pusan.

 

Kuingilia kati kwa Umoja wa Mataifa na Marekani

Julai 30, 1950 Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa liliamua kuingilia kijeshi dhidi ya uvamizi kutoka Korea Kaskazini. Azimio hilo lilipita kwa sababu Umoja wa Kisovieti haukuhudhuria kikao, hivyo ulishindwa kupiga veto yake. Jeshi lililoingia kwa niaba ya Umoja wa Mataifa liliunganisha vikosi kutoka nchi 22, jumla askari 500,000 na wengi wao kutoka Marekani.

 

Katika awamu ya pili Jeshi la Umoja wa Mataifa, lilifika Pusan kuanzia Agosti 1950. Ndege za Marekani zilishambulia madaraja na sehemu nyingine kote kwenye rasi. Korea ya Kaskazini ilikosa ndege za kijeshi. Jeshi la Marekani na Korea Kusini lilielekea Kaskazini na kuiteka Seoul  Septemba 21, 1950. Likaendelea kuwarudisha Wakorea wa Kaskazini pia kuteka mji mkuu wa Korea Kaskazini Pyonyang Oktoba 19 hadi kukaribia mpaka wa Korea na China kuanzia mwisho wa mwezi wa kumi 1950.

 

Kutokana na mashambulio ya ndege kutoka kwa Marekani, Wachina walitoa onyo kwa Wamarekani wasisonge mbele zaidi lakini Jemadari Mkuu, MacArthur, hakujali onyo hilo. Katika awamu ya tatu kuanzia Novemba 1950, Jeshi la China likaingia kati na kuwasukuma Wamarekani Kusini na kuteka Seoul mara ya pili  Januari 3, 1951.

 

Ndege za Kijeshi za Umoja wa Kisovieti zilisaidia kulinda anga nyuma ya mstari wa mapigano lakini bila kuwashambulia Wamarekani juu ya eneo lao. Wachina walisogea mbele ndani ya Korea ya Kusini lakini walikwama kwa sababu walishindwa kupata mahitaji yao kutokana na nguvu ya Marekani angani.

 

Kurudi kwa hali ya awali

Katika awamu ya mwisho hadi Julai 1951 mashambulio ya Kaskazini na Kusini yalibadilishana na China ilirudishwa polepole hadi mpaka wa 38 °C latitudo uliowahi kuwa mpaka kabla ya vita. Marekani iliamua kutosonga mbele zaidi ikitafuta majadiliano ya kusimamisha vita. Majadiliano haya yalianza Julai 10, 1951 yakaendelea hadi 1953.

 

Muda wote vita iliendelea kwa njia ya mashambulizi kila upande lakini kwa shabaha ya kushika maeneo yaliyowahi kuwa upande mmoja au mwingine kabla ya vita lakini kushikwa na adui kwa sasa. Julai 27, 1953 mapatano ya kusimamisha vita yalifikiwa. Eneo lenye upana wa kilomita nne pande zote mbili za mstari wa latitudo ya 38 lilitangazwa kuwa “Ukanda usio na jeshi”. Hadi leo ni mpaka kati ya nchi zote mbili za Korea na kulindwa na wanajeshi wengi sana.

 

Vita ya Vietnam

Vita ya Vietnam ilikuwa iliyopiganwa katika nchi ya Vietnam kati ya 1960 na 1975 lakini mapigano yake yaliendelea hadi nchi jirani za Kambodia na Laos. Wakati ule Vietnam iligawiwa kwa madola mawili ya Vietnam Kusini na Vietnam Kaskazini. Ilikuwa hasa vita ndani ya Vietnam Kusini. Kwa upande moja walisimama Serikali ya Vietnam Kusini pamoja na askari za Marekani na nchi mbalimbali zilizoshikamana nao; kwa upande mwingine wanamgambo ya Vietkong pamoja na Jeshi la Vietnam Kaskazini iliyosaidiwa na nchi za kikomunisti kwa pesa na silaha.

 

Mapigano yalitokea hasa ndani ya Vietnam Kusini. Vietnam Kaskazini ilishambuliwa kwa mabomu ya ndege ya Marekani na wanajeshi wake walitumwa kupiga vita katika Kusini. Vita ilikwisha kwa ushindi wa Kaskazini mwaka 1975.

 

Mdororo Mkuu

Mdororo Mkuu kilikuwa kipindi ambacho uchumi wa Marekani na sehemu nyingine za dunia ulikuwa mbaya sana. Ilianza na kuanguka kwa Soko la Hisa la Marekani 1929. Bei za masoko katika Soko la Hisa la Marekani zilianguka kuanzia Oktoba  24 hadi hapo Oktoba  29, 1929. Watu wengi walipoteza kazi zao, wengi wakawa hawana makazi na maskini. Hii ilimaliza utajiri wa Roaring Twenties. Ile siku ambayo imesemwa kuanzia kwa Mdororo Mkuu inaitwa “Black Tuesday.”

 

Wakati Mdororo Mkuu umeanza, Rais wa Marekani alikuwa Herbert Hoover. Watu walipiga kura kwa ajili ya rais mpya mwaka 1932. Jina lake lilikuwa Franklin D. Roosevelt. Roosevelt alivyopata serikali akapata kupitisha sheria mpya na mipango ya kusaidia watu ambao walipata kuumizwa na Mdororo Mkuu. Hiyo mipango ilikuwa ikiitwa New Deal. ulikuwa mbaya, lakini kwa msaada wa kila mmoja halia kikiwa shwari kila kitu kikawa sawa.

 

Wakati wa Vita Kuu ya Pili ya Dunia kati ya mwaka 1939 na 1944, watu wengi walipata tena kazi kwa sababu ya vita hiyo, na wakati huo huo Mdororo Mkuu ukawa unaelekea ukingoni na maisha yakawa kawaida na si kama hapo awali.

 

Madeni ya Marekani yaongezeka

Pamoja na kuwa ni taifa lenye nguvu duniani Marekani inakabiliwa kuwa na deni kubwa kuliko nchi nyingine

 

Wizara ya Fedha ya Marekani ilitangaza kuwa madeni ya taifa ya nchi hiyo yameongezeka na kupindukia dola trilioni 16. Imeelezwa kuwa kila siku takribani dola bilioni nne zimekuwa zikiongezeka katika madeni ya nchi hiyo.

 

Ripoti ya hivi karibuni ya taasisi za kiuchumi za Marekani inaonesha kuwa kiwango cha madeni ya Marekani mwaka 2008 kilikuwa takribani asilimia 70. Mwaka 2011 kilipanda na kufikia takribani asilimia 102 na inatabiriwa kwamba hadi kufikia mwaka 2015 kitavuka dola trilioni 23.

 

Baraza la Uhusiano wa Kigeni la Marekani linaamini kwamba nakisi kubwa ya bajeti ambayo na tija yake ni kuongezeka kwa madeni ya Marekani mwanzoni mwa miaka ya karne ya 21, imetokana na siasa za Rais aliyepita wa Marekani, George W. Bush, za kupunguza kodi na gharama kubwa alizotumia katika vita huko Iraq na Afghanistan. Wachambuzi wa mambo nchini Marekani wanaamini kwamba mwenendo huo ndiyo chanzo cha kuzorota uchumi wa nchi hiyo. Aidha, siasa hizo zinatajwa kuwa ndizo zilizosababisha kuongezeka maradufu kwa madeni ya uzalishaji wa ndani baina ya mwaka 2007 na 2011.

 

Wajumbe wa Chama cha Republican katika Kamati ya Bajeti ya Baraza la Seneti la Marekani, wanasema kuwa endapo Rais Barack Obama atashinda katika awamu ya pili ya uchaguzi wa rais nchini Marekani, dola trilioni 4.4 zitaongezeka katika mzigo wa deni la nchi hiyo. Wakati Obama aliposhika hatamu za uongozi nchini Marekani mwaka 2009, deni la taifa la nchi hiyo lilikuwa kiasi cha dola trilioni 10 na bilioni 600. Kabla ya kuingia Ikulu ya White House, Obama aliahidi kwamba atafanya juhudi za kupunguza mzigo wa deni la nchi hiyo. Hivi sasa kinyume na alivyoahidi, deni hilo linazidi kuongezeka siku baada ya siku.

 

Mara baada ya kutangazwa ripoti ya Wizara ya Fedha ya Marekani inayoonesha kuongezeka deni la nchi hiyo, Mitt Romney, mgombea wa kiti cha Urais wa Marekani alishikia bango jambo hilo na kukosoa uwezo wa Obama wa kupunguza madeni ya nchi hiyo. Wataalamu wa mambo wanaamini kutangazwa ripoti hiyo inayobainisha kuongezeka madeni ya Marekani, ambako kumekwenda sanajari na kuanza mkutano mkubwa wa Chama cha Democratic katika Jimbo la Carolina Kaskazini, kunaweza kusababisha kushamiri kwa ukosoaji wa Chama cha Republican dhidi ya sera za kiuchumi za Rais Obama.

 

Wachambuzi wa mambo wanaamini pia kuwa sababu kuu tatu ndizo zilizochangia kuongezeka madeni ya Marekani. Hali ya kiuchumi, sera jumla na mabadiliko ya kijamii. Weledi wa masuala ya kiuchumi wanaamini njia pekee ya kupunguza nakisi ya bajeti ya Marekani ni kuongeza kodi na serikali kupunguza gharama za matumizi yake.

By Jamhuri