Vitalu vya uwindaji yale yale

DAR ES SALAAM

NA MWANDISHI WETU

Ugawaji wa Vitalu vya Uwindaji wa Kitalii kwa njia ya kielektroniki umelalamikiwa na sasa baadhi ya wadau wenye tasnia hiyo wameshauri mnada urejewe.

Wanasema kurejewa huko si tu kwamba kutakuwa ni kuwatendea haki waombaji waliovikosa kwa mizengwe, bali kutaiwezesha serikali kupata mapato makubwa na wawekezaji makini.

Wadau hao wanamuomba Rais Samia Suluhu Hassan kwa mamlaka aliyonayo aunde timu itakayompa ukweli kuhusu hujuma zinazofanywa kwenye mnada.

Hivi karibuni Waziri wa Maliasili na Utalii, Dk. Damas Ndumbaro, akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam aliagiza waombaji na washindi wa mnada wa vitalu vya uwindaji wa kitalii wawe na dhamana ya benki kabla ya kukabidhiwa vitalu.

Alimwagiza Kaimu Kamishna wa Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania (TAWA), Mabula Misungwi, kutekeleza agizo hilo.

Hata hivyo, habari za uhakika kutoka TAWA zinasema tayari agizo hilo limepigwa ‘zengwe’, kwa kukwepesha aina ya dhamana.

Wakati dhamana ya benki ikitakiwa iwekwe kwenye kila kitalu kinachoombwa, TAWA na Wizara ya Maliasili na Utalii wamekuja na utaratibu wa dhamana kuwekwa kwa kampuni inayopewa kitalu. Tayari maelekezo hayo yametolewa na kutakiwa kuanza kwenye mnada wa vitalu zaidi ya 30 uliotangazwa hivi karibuni.

“Dhamana ya benki inatakiwa iwe kwa kila kitalu, si kwa kampuni, kwa sababu kuna kampuni zina vitalu hadi vitano…huwezi kusema vitalu vyote hivyo viwe na dhamana moja.

“Vitalu ni mali ya serikali, kazi ya serikali inayotolewa kwa njia ya mnada kama vile ujenzi wa majengo au miradi mikubwa yoyote ya serikali lazima kuwe na bank guarantee, sasa iweje kwenye vitalu hilo likwepwe?” kimehoji chanzo chetu.

Kuna wasiwasi kuwa endapo utaratibu wa washindi wa zabuni hautakuwapo, baadhi ya vitalu vitatelekezwa miaka michache baada ya kukabidhiwa.

“Hatuna hakika kama wote wanaopewa vitalu ni wahifadhi, na inashangaza kuona due diligence eti inafanywa baada ya mtu kushinda zabuni. Hii ilitakiwa ifanywe kabla ya mnada ili watu safi pekee washindanishwe. 

“Tusipokuwa makini hawa watu watapewa vitalu, wataua wanyama kwa kuongeza quota na baadaye watavitelekeza na kukimbia wakijua hakuna dhamana yenye kuwabana,” wamesema kwenye taarifa yao.

Malalamiko mengine ya wadau wa tasnia ya uwindaji ni kuwa mfumo wa kielektroniki umechezewa, hivyo kutoa upendeleo kwa baadhi ya waombaji.

“Mfumo umechezewa, hilo tuna hakika nalo kwa asilimia 100 ndiyo maana tunaomba Mheshimiwa Rais aingilie kati kwa kuteua watu anaowaamini wampe taarifa sahihi.

“Wapo maofisa wa wizara (majina tunayo) ambao ni wabia kwenye kampuni kadhaa zilizopendelewa kupata vitalu. Tunatambua kuwa Mheshimiwa Waziri anajua haya, lakini nadhani anawahofu wenzake hasa kwenye suala la bank guarantee,” imeeleza taarifa ya wadau wa tasnia ya uwindaji kwa JAMHURI.

 Waziri alitoa maelekezo hayo ikiwa ni majibu yake kwa swali aliloulizwa kuhusu uwepo wa ‘bank guarantee’ kwa wanaopewa vitalu kama njia ya kuwazuia waliovipata kuvitelekeza baada ya kuvuna faida.

“Hili suala ni zuri sana…Mabula umesikia, vitalu wanaviharibu halafu wanavirudisha, sasa hii bank guarantee itafanya kazi hiyo, kwa hiyo ni wazo zuri ambalo tumelipokea,” amesema Dk. Ndumbaro.

Waziri huyo amezungumzia pia kuwapo kwa madai ya kuchezewa mfumo wa mnada wa vitalu kwa njia ya kielektroniki.

“Hili jambo na sisi tumelisikia sana. Kwenye mnada huu tukasema ebu tuweke mbele zaidi kulifanyia kazi. Tukaomba wenzetu wa e-Government waje. Ule mnada umekwenda kwa muda wa siku saba. Katika muda huo wa siku saba watu wa e-Government wame-monitor na wamesema hakuna kuingilia mfumo na wametuandikia ripoti kabisa. Wangetuambia watu wa wizara tu tungesema (shaka), lakini watu wa e-Government ndio wana mamlaka ya kukagua na kudhibiti hii mitandao – wameridhika na ubora, wameridhishwa kwamba haukuingiliwa. Kama kuna ushauri tofauti tunaupokea,” amesema Dk. Ndumbaro.

Wakati waziri akisema hayo, JAMHURI limepokea taarifa kutoka kwa wadau walioshiriki mnada huo wakisema mfumo uliingiliwa ili kuwanufaisha wachache.

Wanatoa mfano kuwa baadhi ya waendesha mfumo walikuwa wakitoa siri kwa ‘watu wao’ zilizohusu kiwango  kilichowekwa na washindani.

“Kwa mfano, ulipoweka kiasi cha dola 200,000 siri hiyo ilipelekwa kwa mtu wao na kutakiwa aweke dola 201,000. Ulipotaka kurudi na kuweka kwa mfano dola 250,000 system unakuta tayari haikubali kwa sababu imeshaingiliwa.

“Matokeo yake serikali imekosa pesa nyingi sana. Fikiria mtu anayeweka dola 200,000 anakataliwa na anachukuliwa aliyeweka dola 170,000. Tumemsikia waziri lakini ajue ukweli kuwa mfumo wote umechezewa sana,” kimesema chanzo chetu.

Wanaolalamika wanasema mchezo mbaya ulikuwa kwenye vitalu vilivyo Kaskazini.

“Tunashauri mnada wa vitalu vilivyo Umasaini urudiwe kwa sababu kule kuna wanyama wasiopatikana vitalu vingine nchini, lakini vimeuzwa kwenye mnada kwa fedha kidogo sana. Nakuhakikishia vikirudiwa kila kitalu kinaweza kununuliwa kwa dola 250,000 hadi 270,000. Vimeuzwa bei ya chini kwa sababu system ilikuwa tempered. Tunajua watu wana masilahi yao. Kuna vigogo wa TAWA wana ubia na baadhi ya walioshinda zabuni baada ya kuingilia mfumo wa mnada,” imeelezwa na vyanzo vyetu vya habari.

Aidha, kuna malalamiko kuwa kwenye mnada ilitangazwa kuwa wanaoshinda vitalu wanapewa siku 10 za kufanya malipo, lakini baadaye utaratibu huo umekiukwa na kuwapa muda hadi Oktoba, mwaka huu.