Septemba 3, mwaka huu, Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Fakihi Jundu, aliitisha mkutano na waandishi wa habari ofisini kwake Dar es Salaam na kutoa taarifa ifuatayo:

TAARIFA YA MAHAKAMA KWA VYOMBO VYA HABARI KUHUSU HABARI ILIYOANDIKWA NA GAZETI LA JAMHURI; LIKIWATUHUMU WAH; MAJAJI NA MAHAKIMU KUWALINDA WAFANYABIASHARA WA  DAWA ZA KULEVYA

Hivi karibuni imekuwa ni kawaida kusikia Majaji, Mahakimu au kesi mbalimbali zilizo mahakamani zikiendelea kusikilizwa, au maamuzi fulani yaliyotolewa na mahakama kulalamikiwa katika vyombo vya habari, na hatimaye watoe maamuzi husika au wasikilizaji wa kesi husika, ambazo nyingine huwa bado zinaendelea mahakamani kudhalilika na kuhukumika, na wakati mwingine, ushahidi kuharibika au kumshawishi Jaji au hakimu kutoa maamuzi kwa kufuata maoni ya magazeti, na ilhali maadili ya kazi za ujaji hayatoi mamlaka kwa walalamikiwa kujibu kwa kukanusha shutuma zilizo mbele yao kwa njia ya vyombo vya habari.

Ipo mifano mingi ya kuthibitisha kauli. Kwa minajili ya taarifa hii ninapenda kujikita kwenye habari iliyoripotiwa na Gazeti la JAMHURI la toleo la  Agosti 27-Septemba 2 yenye kichwa cha habari “Majaji wanaolinda wauza ‘unga’ wabainika”

 

Ndani ya taarifa hiyo, pamoja na mambo mengine, majina ya baadhi ya majaji na mahakimu yalitajwa na kuhusishwa na tuhuma mbalimbali zikiwamo za kuwalinda na kuwaachia watuhumiwa wa madawa ya kulevya kienyeji, kiupendeleo, na kwa kukiuka sheria. Taarifa hiyo, mwandishi anasema, ameamua kuwataja Majaji na Mahakimu kwa majina.

Tuhuma hizo dhidi ya Mahakama ni nzito na zenye lengo la kuichafua Mahakama ili wananchi wakose imani na Mahakama yao, tuhuma ambazo kwa uzito wake, ilimpasa mwandishi wa gazeti husika, kukutana na uongozi wa Mahakama ili aweze kupata ukweli wa taarifa mbalimbali alizoziandika.

Uongozi wa Mahakama una taratibu zake za namna ya kutoa taarifa, iwapo mtu yeyote anahitaji kuhusu namna suala fulani lilivyoendeshwa au katika kupata taarifa fulani zenye manufaa kwa nchi yetu.

 

Mahakama kwa mujibu wa ibara 107 A, ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania 1977, ndiyo yenye mamlaka ya kufasiri sheria na kutoa haki. Mahakama inaongozwa na Mhe. Jaji Mkuu ambaye ndiye kiongozi wa Muhimili wa Mahakama kwa mujibu wa ibara ya 118 (1), na kwa mujibu wa ibara 109 (2) Jaji Kiongozi anatajwa pia kuwa ndiye msaidizi maalum wa Mhe. Jaji Mkuu, pia wapo wahe. Majaji mbalimbali wa Mahakama Kuu, wakiongozwa na wah. Majaji Wafawidhi kulingana na kanda zao, pamoja na wasajili ambao pia wana mamlaka ya kutoa taarifa mbalimbali za mashauri yaliyo mahakamani, yanayoendelea na yale yaliyokwisha kusikilizwa.

 

Nimeona nianzie kwa kuzungumza hili kwa kuwa taarifa nyingi zinazozungumzwa dhidi ya mahakama si za kweli na hata waandishi wameshindwa kuja kupata ufafanuzi wa masuala mbalimbali kwa uongozi wa Mahakama. Mhe. Jaji Kiongozi, majaji wafawidhi wa kanda, Mtendaji Mkuu, Msajili Mkuu, na wasaidizi wake pamoja na Msajili wa Mahakama Kuu, wote hawa ni viongozi wa Mahakama, wenye mamlaka ya kutoa taarifa mbalimbali juu ya Mahakama ya Tanzania na katika maswali mbalimbali yanayohusu utendaji wa Mahakama.

 

Madhara ya uandishi wa namna hii ni sawa na ‘negligence and reckless reporting’, usiofuata mila na miiko ya uandishi wa masuala ya kimahakama, zaidi kuhusu masuala ya namna ya uendeshwaji wa kesi, maamuzi yaliyotolewa na Mahakama, kimuonekano hasi, yanaonekana katika rangi yake sawia kwamba, hauna nia njema katika ustawi wa amani ya nchini hii, ambayo inaendeshwa kwa misingi ya utawala wa sheria. Iwapo wananchi watakosa imani na Mahakama au vyombo vya dola, ni dhahiri kuwa watu watajichukulia sheria mkononi kwa kutohofia Mahakama au kutakuwepo na taratibu mbalimbali zisizofuata sheria na zilizo kinyume na haki za binadamu zenye lengo pia za kufuata zama za Pilato na Herode.

 

KESI ZILIZOLALAMIKIWA

Miongoni mwa kesi zilizolalamikiwa  ni pamoja na kesi No. 47 ya mwaka 2011, kati ya Jamhuri dhidi ya Fredy William Chonde. Kwanza kabisa, napenda niwafahamishe kwamba, kesi hii bado ipo Mahakama ya Rufani. Kuizungumza popote na kuitolea mfano katika magazeti haifai kisheria, kwa kuwa kufanya hivyo, kuna athari mbalimbali, mfano; kupotea kwa ushahidi au kutoa ushawishi kwa Wah. Majaji wanaosikiliza rufaa husika, baada ya washtakiwa kupewa dhamana na Mhe. Jaji Msuya, upande wa mashtaka haukuridhika na maamuzi ya Mhe. Jaji na ulikata rufaa kwenda Mahakama ya Rufani, rufaa ambayo bado haijasikilizwa.

 

Kwa kuwa kesi hii bado inaendelea, kwa njia ya rufaa ya kupinga dhamana, pamoja na kwa njia ya usikilizwaji wa kesi ya msingi, ambayo kwa kumbukumbu za Mahakama, imekuja jana tarehe 2 mwezi Septemba, 2013. Kwa ajili ya usikilizwaji wa awali yaani ‘Preliminary Hearing’ mbele ya Mhe. Jaji mwingine, kwa uzito huu kuzungumza kesi ya namna hii ni kinyume na maadili ya uandishi.

 

Ila tu, jambo moja ninalotaka kufafanua hapa ni kuwa, Ibara ya 107 A ya Katiba, inaipa mamlaka Mahakama kuwa ni chombo pekee cha kutafsiri sheria za nchi na kutoa haki, maamuzi yoyote atakayoyatoa yatawajibishwa kwa kukatiwa rufaa kwa upande wa pili iwapo haujaridhika na maamuzi husika. Mfano, sheria Na. 9 ya kudhibiti dawa za kulevya ya mwaka 1995, inazuia mtu yeyote aliyekamatwa na dawa za kulevya zenye thamani kuanzia Tshs milioni 10 asipewe dhamana, lakini pia sheria hiyo hiyo, katika kifungu Na. 27 (1) (b) kinamtaka Mkurugenzi wa Mashtaka kuambatanisha kiapo (certificate) na hati ya mashtaka kwa pamoja, kiapo ambacho ni lazima kithibitishwe na Kamishna wa  National Coordination of Drugs Control kinachoonesha thamani halisi ya dawa za kulevya alizokamatwa nazo mshtakiwa.

 

Sasa, kama sheria inasema ni lazima kwa upande wa mashtaka kuambatanisha kiapo, iwapo upande wa mashtaka utashindwa kuambatanisha kiapo tajwa, ni dhahiri kuwa kila jaji au hakimu anaweza kuwa na tafsiri tofauti ya maana ya ulazima wa kuambatanisha kiapo husika, Jaji mwingine anaweza akaona kama labda hati ya mashitaka imebaki kama  ‘a mere allegation’ yaani labda kweli au la! Mshtakiwa alikutwa na kiasi kilichotajwa kilichozidi shilingi milioni 10. Kisheria, ‘a mere allegation’ ni sawa na mzaha mzaha, ambao Mahakama haitautilia maanani, na itahitaji uthibitisho mzito kuweza kumshawishi Jaji au Hakimu kuweza kumtia hatiani mshtakiwa.

 

Maamuzi mbalimbali ya Mahakama Kuu na Mahakama ya Rufaa yaliyopita, yaani ‘precedent’ yamegawanyika katika tafsiri hii ya sheria, ambapo baadhi ya Wah. Majaji wamekuwa wakitoa dhamana kwa kesi zenye asili ya namna hii, na wengine wamekuwa wakikataa kutoa dhamana. Mfano katika kesi, Misc Criminal Application; No. 57 ya mwaka 2001 (Mahakama Kuu ya Tanzania) kati ya Jonathan Loliangwende Elia na wenzake wane, dhidi ya Jamhuri iliyokuwa mbele ya Mhe. Jaji Kileo, wakati huo akiwa Jaji wa Mahakama Kuu, suala la dhamana kwa washtakiwa liliibuka baada ya mwendesha mashtaka kushindwa kuambatanisha kiapo kuthibitisha thamani ya madawa yaliyokamatwa. Mhe. Jaji Kileo alisisitiza katika kesi hiyo kuwa ni lazima upande wa mashtaka kutoa ushahidi wa thamani ya madawa aliyokamatwa nayo mshtakiwa. Napenda kumnukuu Mhe. Jaji Kileo akisisitiza kuwa; “It requires the tendering of evidence to show that indeed the substance alleged has the value shown in the charge sheet, I say this bearing in mind that bail is a right of an accused person which should only be denied where there are cogent and compelling reasons to do so” mwisho wa kunukuu.

 

Kesi ya namna hii, sasa bado ipo inaendelea katika Mahakama ya Rufaa, na maamuzi yake yatasaidia kutoa tafsiri fasaha ya kifungu Na. 27(a)(b) cha sheria ya kuzuia madawa ya kulevya sura ya 95.

 

Kama alivyowahi kuzungumza pia Mhe. Jaji Mushi, (Mstaafu) katika kesi Misc. Economic Application No. 15 ya mwaka 2011, kati ya DPP dhidi ya Freddy William Chonde na wenzake, akiwa anakubali kuongezwa kwa muda wa kukata rufaa wa kesi tajwa, ili kupata ufafanuzi halisi wa kisheria katika Mahakama ya Rufaa, kuhusu kama kuna ulazima wa Mkurugenzi wa Mashtaka kwa mujibu wa kifungu Na. 27 cha sheria tajwa, kuwasilisha hati ya kuthibitisha thamani ya madawa yaliyokamatwa pamoja na hati ya mashtaka, ikiwa imethibitishwa na Kamishna wa Tume ya Kuthibiti Dawa za Kulevya, ‘Commissioner for the National Coordination of Drugs Control’ Mhe. Jaji Mushi alisema, nami napenda nimnukuu.

“…Those two issues are very important to be decided by the Court of Appeal, even as to clear the legal position on this important aspect of criminal law. Currently, the High Court is “divided” on the issues referred above. To let this legal position to go on as it is currently, without the intervention of the Court of Appeal, it will not be “healthy” in the administration of criminal justice, by both the High Court itself, or the subordinate courts thereto either” mwisho wa kunukuu.

 

Nami pia kwa mantiki hiyo, ninatunza maoni yangu kuhusu tafsiri ipi iliyo makini kisheria ya kifungu chenye mgongano nilichokitaja hapo juu hadi pale mahakama ya rufaa itakapotoa tafsiri fasaha ya suala hili.

 

Ni makosa kuzungumzia suala ambalo bado liko katika hatua ya kusikilizwa mbele ya Mahakama kwani kufanya hivyo ni kinyume na sheria.

Kesi nyingine iliyolalamikiwa ni PI Na. 26 ya mwaka 2011 iliyokuwa mbele ya Mhe. Jaji Faudh. Ambapo mwandishi anadai kuwa Mahakama ilimwachia mshtakiwa. Kwa mujibu wa kumbukumbu za Mahakama ni kuwa si kweli kwamba Jaji Faudh alimwachia mshtakiwa kwa matakwa yake binafsi au kutumia kivuli cha Mahakama. Naomba, kila mmoja wetu afahamu na tusiwapotoshe wananchi, tuwaelimishe kuwa; Iwapo upande wa mashtaka/Jamhuri (DPP) ukiwasilisha maombi ya kuondoa shtaka au kufuta mashtaka, yaani ‘Nolle Prosequi’ chini ya kifungu Na. 91 cha Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai sura ya 20 (CPA) kwa kesi yoyote mahakamani, iliyo katika hatua yoyote isipokuwa tu kama ikiwa katika hatua ya utetezi.

 

Mahakama haina mamlaka ya kupinga maombi hayo ya Mkurugenzi wa Mashtaka au Mwendesha Mashtaka anayefanya kazi kwa maelekezo ya Mkurugenzi wa Mashtaka kutoondolewa au kufutwa kwa kesi yoyote.

 

Mkurugenzi wa Mashtaka hapaswi hata kutoa sababu kwanini anaondoa shtaka fulani mahakamani, hilo ni jukumu lake na mtu yeyote hapaswi kuuliza kwa mujibu wa sheria.

Katika kesi; Jamhuri dhidi ya Suleman Salehe Ally, kesi ya mwaka 1985 TLR 96(HC) Mhe. Jaji Ramadhani, akiwa Jaji Mkuu wa Zanzibar wakati huo, alitoa kanuni mbalimbali kuhusu kuondolewa au kufutwa kwa mashtaka na Mwendesha Mashtaka, yaani ‘Nolle Prosequi’ chini ya kifungu Na. 81 (a) cha Sheria ya Zanzibar ya Criminal Procedure Decree, sura ya 14.

 

Mhe. Jaji Mkuu Ramadhani katika kesi tajwa amesema, naomba nimnukuu.

“The Attorney General is the only public prosecutor with the priviledge position, whereby he can withdraw charges without assigning any reasons, and the courts must readily comply with his move…” mwisho wa kunukuu.

 

Kwa Tanzania Bara, mwendesha mashtaka ni Mkurugenzi wa Mashtaka, atakapoamua kuondoa kesi, Majaji na Mahakimu hatupaswi kuhoji, tunapaswa kukubali maombi husika, kwa kumwachia mshtakiwa kwa mujibu wa sheria tajwa. Jaji au Hakimu yeyote likiwasilishwa kwake ombi la namna hiyo, anakuwa amefungwa mikono kisheria, hana mamlaka tena kuendelea na kesi husika. Hivyo kumlaumu Mhe. Jaji yeyote kwa hilo ni kumtwisha mzigo usiokuwa wa kwake.

 

Labda niwaulize ninyi, mfano ninyi ni majaji, suala la namna hii limekuja mbele yenu, je, mngekataa kufuata sheria au mngefuata taratibu halali zilizowekwa kisheria?

Hapa kweli tutamlaumu Jaji kwa kuondoa kesi? Hii ni haki? Je, tunamtendea haki Jaji husika aliyechapishwa jina lake katika ukurasa wa mbele wa gazeti lenye kichwa cha habari, “Majaji wanaolinda wauza unga wabainika, gazeti hili sasa limeamua kuwataja kwa majina. Hivi hii ni sawa?

 

Kesi Na. 238 ya mwaka 2010, kati ya Dhoulkefly Awadh Abdallah. Kesi hii inakuja kwa ajili ya kusikilizwa tarehe 30 mwezi huu katika Mahakama Kuu, nadhani si busara pia kuizungumza kwenye magazeti, na kwamba suala la kwanini Mwendesha Mashtaka kamwachia mmoja wa washtakiwa, si mzigo wa Mahakama, nilishazungumza kuhusu nguvu za Mkurugenzi wa Mashtaka, iwapo ataona hana haja ya kuendelea na kesi au kumuondoa mmoja wa washtakiwa anaweza kufanya hivyo, na Mahakama haina uwezo wa kumzuia, iwapo anaona ushahidi fulani ni hafifu au mshtakiwa fulani hafai kujumuishwa katika kesi.

 

Kesi nyingine iliyolalamikiwa, ambayo kwa bahati mbaya hatukupata kumbukumbu zake kwa haraka, kwa kuwa mwandishi ameonesha kuwa maamuzi yaliyotolewa katika Mahakama ya Kinondoni na Hakimu Msongo, ambaye hakuwahi kufanya kazi katika Mahakama ya Kinondoni.

 

Kitu kimoja ninachopaswa kusisitiza hapa ni kuwa, sheria ya ushahidi yaani ‘the Evidence Act’ sura ya 6. Katika kifungu Na. 110 kinazungumza mamlaka ya kuthibitisha shtaka, ambapo mzigo wa uthibitishwaji wa makosa ya jinai upo kwa Mkurugenzi wa Mashtaka. Iwapo kutakuwa na wasiwasi wowote katika ushahidi, wasiwasi huo utakuwa ni manufaa kwa mshtakiwa, upande wa mashtaka ni lazima uthibitishe shtaka pasi na wasiwasi wowote, labda ni kweli au la. Mfano iwapo mshtakiwa alikamatwa na mzigo wa sukari wa kg 100, basi upande wa mashtaka unapaswa kuhakikisha kuwa kilo 100 zote, zimefikishwa mahakamani na kutolewa ushahidi.

Iwapo upande wa mashtaka, utashindwa kufanya hivyo, itakuwa ni hatari kwa Mahakama kumfungua mtu yeyote kwa namna hiyo kwani itakuwa ni kinyume cha sheria.

 

Mahakama haitafanya kazi ya uonevu au kumpendelea mtu yeyote, na kila anayeleta shauri lake mahakamani basi ni lazima ajipange kulitetea suala lake alilolileta kwa kuthibitisha madai yake, vinginevyo Mahakama si Pilato wala haitajiridhisha katika zama za Pilato na Herode, kwa kuamua kufunga watu pasipo na ushahidi uliojitokeza.

 

Kesi nyingine, ni ile ya jinai iliyokuwa mbele ya Mhe. Luhwago, Jamhuri dhidi ya Kwarku Sarfo. Kumbukumbu za Mahakama zinaonesha kwamba, kesi hii ilikuwa ni ya muda mrefu, na Mahakama iliondoa kwa kuwa upande wa mashtaka ulishindwa kuendelea na usikilizwaji wa shtaka dhidi ya mshtakiwa, pia lilishapita mbele ya Mahakimu mbalimbali kabla ya kupangiwa Bwana Luhwago. Mahakama haiwezi kukaa na kesi milele zisizokwisha, ni jukumu kwa wenzetu kuhakikisha kwamba, kesi  za msingi zinawakilishwa  ipasavyo pasipo kudharau na kwamba “Justice delayed is Justice denied”… Ni jukumu la Mahakama ni kusimamia kanuni hizi za haki za binadamu kuhakikisha kwamba kanuni hizi hazivunjwi na mtu yeyote.

 

Katika nchi zinazoongozwa na utawala wa sheria Tanzania, mamlaka ya kusikiliza tuhuma dhidi ya watu na kutolea maamuzi ni ya Mahakama. Kama nilivyosema hapo awali. Ibara ya 13(6) (a) (b) ya Katiba, maamuzi yoyote yanayoathiri haki au wajibu wa mtu hayawezi kufanyika bila ya yeye kusikilizwa, pia ni marufuku kwa mtu aliyeshtakiwa kwa kosa la jinai kutendewa kama mtu mwenye kosa hilo mpaka itakapothibitika kuwa anayo hatia ya kutenda kosa hilo.

 

Watu wote ni sawa mbele ya sheria, na wanayo haki, bila kubaguliwa na kulindwa na kupata haki sawa mbele ya sheria, hivyo Mahakama itabaki katikati (neutral) bila kuegemea upande wowote na itatenda haki hata kama haki husika itawaumiza watu wengi. Mfano; iwapo mtu mmoja amewashtaki watu 100, na ikaonekana  ana haki, Mahakama itampatia haki hiyo pasipo kujali kwamba maamuzi hayo yamewaumiza watu wengi.

 

Mahakama inaongozwa na Katiba ya nchi, sheria mbalimbali na kanuni katika kutenda haki kwa wanachi wetu na sio maneno ya kutaka kuwafurahisha watu fulani, kwani kufanya hivyo itakuwa ni kwenda kinyume na matakwa ya sheria. Kamwe Mahakama haitafanya kazi za harakati ‘activist’ au za kisiasa zenye lengo la kuwanufaisha wanasiasa na wanaharakati au mtu yoyote. Tutafuata taratibu za kisheria.   Na yeyote ambaye ataona hakutendewa haki, basi ni jukumu lake kukata rufaa katika Mahakama ya juu zaidi, au yeyote anayeona kuwa hakimu au jaji fulani anakwenda kinyume na maadili, sheria ya utawala ya Mahakama yaani, ‘The Judicial Administration Act 2011′ inatoa mwanya kwa mtu yeyote kutoa malalamiko yake au kumshtaki hakimu au Jaji husika aliyekwenda kinyume na maadili, wapo majaji na mahakimu kadhaa wameshawajibishwa na baadhi kufukuzwa kazi. Hii ndiyo njia pekee halali na si vinginevyo.

 

Tuhuma hizi nzito dhidi ya majaji na mahakimu zilizotolewa na gazeti hilo la JAMHURI na za namna kama hiyo za kukejeli Mahakama, zimekuwa zikisambazwa kwa umma mara kwa mara. Kwa kufanya hivyo ni wazi kwamba majaji na mahakimu waliotajwa pamoja na Idara nzima ya Mahakama wamehukumiwa hata kabla tuhuma hizo hazijathibitika kinyume na Ibara ya 13 ya katiba.

 

Ni  wazi kabisa kwamba imani ya watu katika chombo hiki muhimu cha kutoa haki inaweza kushuka. Mfano, mwaka jana, gazeti hili la JAMHURI katika makala yake ya tarehe 14 Agosti hadi 20 mwaka 2012, iliwahi toa makala, yenye kichwa cha habari “Majaji’ vihiyo’ watajwa”, ikishutumu baadhi ya majaji kupewa mikataba kinyume na sheria, nikiwemo mimi mwenyewe, madai ambayo gazeti husika lilishindwa kudhibitisha kwa kutoa mikataba waliyoitaja.

 

TUEPUKE KUELEKEZA SIASA/HARAKATI KATIKA IDARA YA MAHAKAMA

Moyo wa nchi yoyote inayotawaliwa na utawala wa sheria ni Mahakama. Mahakama ni kimbilio la wote na ni mlinzi na mtoaji mkuu wa haki. Hili linafanikiwa pale Mahakama inapoheshimiwa na kuaminiwa kama chombo huru kisichofungamana na makundi yoyote ya kisiasa, kijamii, kiuchumi na kiutamaduni.

 

Kwa kuzingatia umuhimu wa hilo, Katiba imekataza bayana kwa maofisa wa Mahakama kuwa na uhusiano na vyama vya kisiasa au kujiingiza katika shughuli za harakati. Kiapo cha  ujaji na uhakimu kinawataka majaji katika kufanya kazi zao kuwa huru na kutoa maamuzi bila kuathiriwa na upendeleo, huba wala chuki. Zaidi ya hilo, katiba imeweka ibara zinazolinda uhuru wa Mahakama na kuondoa uwezekano wowote wa kuingiliwa na chombo chochote.

 

Pamoja na uhuru mkubwa Mahakama tuliopewa katika kufanya maamuzi, maamuzi hayo ni lazima yawe ya haki, Mahakama haijawekwa kuwa juu ya sheria. Maamuzi ya Mahakama yanapaswa kuwa kwa mujibu wa sheria, pale jaji au hakimu anapokosea kuna taratibu maalum za kumrekebisha na hata kumvua  kofia ya ujaji au uhakimu. Hamna uhalali wowote kwa wanasiasa, wanaharakati au mtu yeyote kutumia vyombo vya habari kuichafua Mahakama na maofisa wa Mahakama.

 

Vita hii ya madawa ya kulevya, ili iweze kufaulu, ni muhimu kuwa na ushirikiano na vyombo vyote husika, lakini kuandika habari kwa lengo la kuwakatisha tamaa wengine si sawa, nasisitiza.

 

Mfano, hivi karibuni wadau wa haki jinai, tulikutana chini ya uenyekiti wangu, tumekuwa tukishirikiana kwa karibu.

Mtu yeyote hata kama unaguswa kiasi gani, hupaswi kuzungumzia kesi zinazoendelea mahakamani. Walioweka kanuni hizi wanajua kuwa inaweza kuathiri uamuzi wa Mahakama.

 

Ni vizuri Watanzania tukajihadhari na kuingiza siasa katika Mahakama. Tuache Mahakama ziendelee kuwa huru maana ni kimbilio letu sote.

Kama kuna mapungufu katika Idara ya Mahakama (na of course hayawezi kukosekana), tutumie taratibu zinazokubalika kisheria ambazo tumejiwekea sisi wenyewe.

 

HATUA TUTAKAZOCHUKUA

Wanahabari wanapotaka kuandika habari za Mahakama, wahakikishe wanazingatia maadili ya uandishi wa habari za Mahakama kuhusiana na masuala ya kuripoti kesi mbalimbali zilizo mahakamani, zinazoendelea au zile zilizokwisha. Kuna taratibu za uandishi wa makala kuhusu Mahakama, ambapo mwandishi anapaswa kuwa makini kwa namna anavyoandika.

 

Vinginevyo mwandishi anaweza kujikuta akijiingiza katika kosa la jinai la kudharau Mahakama, ambapo Mahakama itaamua kama utetezi wake una uzito au la, mzigo wa ushahidi utaamini kwake kudhibitisha kauli zake alizoandika.

Mfano; katika kesi ya Shamwana na wenzake vs The People (1985) LRC (CRIM) P. 120; John and others Vs DPP and others (1986) LRC (Consti and administer) P.508. Andres S/o Mathias Vs Regina (1954) 21 EACA 285 na R Vs Malik (1986) 1 ALL ER 582.

 

Kesi zote tajwa  kama zilivyoamuliwa, zinaonesha namna gani wanahabari wanaweza kusababisha kuharibu kesi kwa kumfanya Jaji kutoa maamuzi ya upendeleo, na pia inaweza kupelekea mwandishi husika kuchukuliwa hatua za kudharau Mahakama ‘contempt of court’.  Pia kama alivyowahi kuzungumza Mhe. Jaji Mkuu wakati huo (marehemu) Mhe. Jaji Nyalali katika kesi; Criminal Appeal No; 191 ya mwaka 1994. Wakili msomi,  Dk. Lamwai, katika kesi iliyokuwa mbele ya Mhe. *****

Kati ya Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP) na Mehboub Ekbar Haji na wenzake; kuwa namnukuu “The radio commentary had the effect of influencing the public to believe, before the conclusion of the trial, that the three accused persons were guilty of the offence charged”.

 

Maoni hayo ya Mhe. Wakili msomi, yaliishawishi Mahakama ya Rufani kukubali kuwa, maoni (comments) zilizotolewa wakati kesi ikiendelea, kushawishi wananchi (General public) kuamini kuwa, kabla ya kutolewa kwa maamuzi ya mwisho ya Mahakama, washtakiwa wana hatia kwa kosa waliloshtakiwa nalo hata bila kusikilizwa.

 

Katika hali ya namna hiyo kwa vyombo vya habari kuzungumza masuala yaliyo mahakamani, yanayoendelea kusikilizwa, katika kesi ya Mehboub Ekbar Haji (Supra), Jaji Mkuu (Marehemu Nyalali) aliagiza kufutwa mashtaka dhidi ya washtakiwa na kuachiwa huru washtakiwa, ili kuweka wazi kwa haki ionekane kutendeka, na kwamba kwa kituo cha habari kilichotoa maoni juu ya mwenendo wa kesi tajwa, maoni yaliyoonekana kuwatia hatiani washtakiwa kabla ya kusikilizwa, Jaji Nyalali, aliagiza. Nanukuu “Appropriate measures are to be taken to restore the presumption of innocence in the mind of the general public’ mwisho wa kunukuu.

 

Vile vile, Jaji mmoja wa Mahakama Kuu ambaye kwa sasa ni mstaafu, aliwahi kukemea tabia ya kuzungumza masuala yaliyo mahakamani, kwa kupitia maamuzi yake ambayo nina yanukuu hapa chini.

 

“If the trial proceeds and the accused persons are acquitted, members of the public who will be fed with the commentary will be persuaded to belive, erroneously, that the government was right that the accused and a court have struck a deal. If convicted, the accused and the public will be led to believe, again erroneously, that the court has been cowed and the government has got what it wanted; a conviction. In either case justice will not be seen to have been done.

 

Hata kama kesi imekwisha uandishi wa kishabiki haufai, uandishi wa kishabiki unaweza kusababisha ‘contempt of court’ kama nilivyosema hapo awali, wa kutaka kudhalilisha majaji au mahakimu, au kuhakikisha kuwa utawala wa Mahakama au uongozi, hauingiliwi au kuzuiliwa na mtu au chombo chochote.

 

Adha ya kuidhalilisha Mahakama kwa namna hii, inaelezwa zaidi katika kesi ya Prof. Wangari Muta Muthai na wenzake Criminal Application No. 53 ya 1981, ambapo Mahakama Kuu Kenya ilimtia hatiani Prof. Wangari na wenzake, kwa kutoa kauli alipokuwa akihojiwa kuwa,  ninanukuu. “What shocked me most of all was the court’s acceptance of the divorce on the ground of adultery. That charge was never proved in court, and I will say without fear that there can only be two reasons for the court to have said that I committed adultery: corruption or incompetence”.

 

Kauli hiyo ya Profesa Wangari aliitoa wakati kesi imekwisha, na Mahakama ilimtia hatiani kwa kulipa faini na wenzake.

Namna hii ya kuidhalilisha Mahakama, haihitaji kuwepo na kesi inayoendelea kuzikilizwa. Hata kesi zilizokwisha kuna taratibu zake za namna ya kuripoti na si kwa kumlaumu moja kwa moja Jaji kama amekula rushwa au hana uwezo wa kufanya kazi.

Hivyo basi, ni muhimu tukashirikiana, ili kuepuka ukiukwaji huu wa sheria. Wakati wote mtakapohitaji taarifa kuhusu suala fulani, ni vizuri mkapata ufafanuzi zaidi kwa viongozi wa Mahakama.

 

AHSANTENI KWA KUNISIKILIZA

IMETOLEWA NA MH. FAKIHI AR JUNDU

JAJI KIONGOZI

3rd, Sept. 2013.


 

 

 

  • Habari zinazolalamikiwa na Jaji Fakihi ni:
  • Majaji wanaolinda wauza ‘unga’ wabainika

 

 

Na Waandishi Wetu, Dar na Zanzibar

Mahakama kupitia baadhi ya majaji na mahakimu wasio waadilifu imebainika kuwa kikwazo kikubwa katika vita dhidi ya dawa za kulevya nchini, uchunguzi wa JAMHURI umebaini.

 

Pamoja na Mahakama, Ofisi ya Mwendesha Mashitaka wa Serikali (DPP), nayo imelaumiwa kwa kufuta kesi katika mazingira ambayo hata mtu ambaye hakusoma sheria, anaweza kuyatilia shaka.

 

Wakati vyombo hivi vikikwamisha vita hii, lawama zimekuwa zikielekezwa kwa polisi na vyombo vingine vya usalama, ambavyo watendaji kazi wake wanafanya kazi usiku na mchana.

 

Juhudi zote zinazofanywa na vyombo vya ulinzi na usalama zinagonga mwamba mahakamani kwa msaada wa ofisi hiyo ya DPP.

Wakati kesi nyingine zikifutwa, nyingine hazisikilizwi, kiasi cha kusababisha zirundikane mahakamani tangu mwaka 2005. Kesi chache zinazohusu watuhumiwa wakubwa wa kuuza ‘unga’ zinamalizwa haraka kwa utaratibu wa ofisi ya DPP kuwasilisha nia ya kutoendelea na mashtaka mahakamani (nolle prosequi) au wasimamizi hao wa utoaji haki kutoa hukumu zinazoacha wengi vinywa wazi na kuwakatisha tamaa polisi.

 

Katika hali ya kushangaza, majaji na mahakimu wamekuwa wakikiuka wazi Sheria ya Kuzuia Dawa za Kulevya Na, 9 ya Mwaka 1995 inayozuia mtu yeyote aliyekamatwa na dawa zenye thamani kuanzia Sh milioni 10 asipewe dhamana, lakini hilo halizingatiwi. JAMHURI haikubahatika kufahamu bayana nini kinawapofusha majaji na mahakimu wakati ‘mapapa’ wanapofikishwa mahakamani kwa tuhuma za kuuza ‘unga’, lakini ni wazi kuwa kuna mtandao mkubwa wa kulindwa kwa watuhumiwa hao wenye ukwasi mkubwa.

 

Wakati polisi wanafanya kazi ya hatari usiku muda wote, wakipambana na wauaji, wahongaji na watu wanaouza dawa za kulevya, kesi za mapapa zinamalizwa kienyeji mahakamani. Moja ya kesi inayotia shaka ni Na. 47 ya Mwaka 2011. Kesi hii ilifunguliwa dhidi ya watuhumiwa Fredy William Chonde, Kambi Zuberi Seif; ambao ni Watanzania na Abdulghan Peer Bux na Shaaban Malik ambao ni raia wa Pakistani.

 

Hawa walikamatwa eneo la Mbezi Beach, Dar es Salaam wakiwa na kilo 175 za heroin, ambako kesi dhidi yao ilifunguliwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu jijini humo. Wakati kesi inaendelea Kisutu, mawakili wa vigogo hawa walikwenda Mahakama Kuu wakafungua shauri la kuomba wapewe dhamana chini ya Jaji Pendo Msuya, wakitambua kuwa sheria inazuia.

 

Bila kuchukua jalada wala kuwasiliana na Mahakama ya Kisutu, huku Jaji Msuya akijua fika kuwa kilo 175 ambazo thamani yake ni zaidi ya Sh bilioni tano, na watuhumiwa hawapaswi kupewa dhamana; yeye kwa mamlaka aliyonayo kama Jaji aliamua kuwapa dhamana watuhumiwa hawa. Baada ya kupata dhamana, Wapakistani walirejeshewa pasipoti zao na wakakimbia nchi. Hawajakamatwa hadi leo.

 

“Cha kusikitisha kesi iliendelea bila kujua kuwa watuhumiwa wamekwishapewa dhamana na hadi Aprili 8, mwaka huu 2013 kesi hiyo ilitajwa… baadaye Mahakama ikapewa taarifa kuwa watuhumiwa walishapewa dhamana na Mahakama Kuu ndiyo maana hawaonekani mahakamani. Tulishangaa sana,” kilisema chanzo chetu kutoka Mahakama ya Kisutu.

 

Kesi nyingine iliyomalizwa kienyeji ni ya Mwinyi Rashid Mkoko. Vyanzo vya JAMHURI vinaonesha kuwa huyu na familia karibu yote wanatuhumiwa kufanya biashara ya dawa za kulevya. Ndugu zake waliokamatwa kwa nyakati tofauti na baba yao, ambako mmoja alidhulumiana, na ‘mzigo’ na wauza unga, hali iliyofanya wamuue kwa kumpiga risasi.

 

Katika familia hii, Rashid Ismail Mkoko ndiye aliyeuawa na wauza unga wenzake eneo la Ilala, Dar es Salaam. Huyu alipata kukamatwa kuhusiana na dawa za kulevya, ila pia kwa kosa la mauaji. Shuhuda wa tukio la Rashid Ismail Mkoko anasimulia kama ifuatavyo:

 

“Huyu ndiye wa kesi ile ambayo kijana aliyemtuma mzigo Pakistan pipi zilipasukia tumboni akafia gesti kule Tabata, Dar es Salaam. Mmoja wa ndugu wa kijana huyu aliyefariki, alimpigia simu akamwambia ‘si unajua alikuwa na mzigo wako ndiyo umemuua? Sasa mbona umetususa? Hata maji ya kunywa hutupatii msibani?’

“Mkoko akamwambia nitakuja jioni. Na kweli jioni iliyofuata akampigia simu kuwa anakwenda hapo nyumbani msibani. Alipofika akampigia simu, akamwambia njoo tuonane. Huyu ndugu wa kijana aliyefariki akatoka nje, akaenda kwenye gari kuonana na Mkoko. “Alipofika Mkoko akamuuliza ndiye wewe uliyenipigia simu jana, yule ndugu wa marehemu akajibu ‘ndiyo’, basi Mkoko alichofanya akatoa bastola akampiga risasi ya usoni yule kijana…akafariki papo hapo, Mkoko akaondoka.

“Polisi walimkamata wakamfikisha mahakamani. Mahakama ikamwachia kwa mizengwe. Ila Mungu si Athumani, ikatokea naye akadhulumu wauza unga wenzake huko Ilala, nao wakamuwinda wakampiga risasi akafa mwaka juzi.

 

“Huyu alikuwa muuza dawa za kulevya mkubwa. Mdogo wake Mwinyi Rashid Mkoko, naye anauza dawa. Tulimkamata na heroin gramu 250 zenye thamani ya Sh milioni 11, ikafunguliwa kesi Temeke Na. PI 26 chini ya Hakimu Mkwawa, lakini ajabu wakati kesi inaendelea kutajwa Temeke hadi leo, huyu Mwinyi Mahakama Kuu imekwishamwachia huru bila vielelezo vyovyote,” kilisema chanzo chetu kutoka mahakamani.

 

Uchunguzi wa JAMHURI umeonesha kuwa awali mawakili wa Mwinyi waliwasilisha ombi la dhamana kwa Jaji Munisi, ambaye aliwaelekeza mawakili wa Serikali kuwa badala ya kumshtaki Mwinyi kwa kukutwa na dawa za kulevya, waiondoe kesi mahakamani na kuifungua upya kama kesi ya kusafirisha dawa za kulevya. Kwa kawaida tuhuma za aina hiyo huwa hazina dhamana.

 

Mawakili walivyopata mwanya huo, wanajua jinsi walivyozungumza na wanasheria wa Serikali. Kesi hiyo badala ya kuiondoa kama alivyoelekeza Jaji Munisi wakaihamishia kwa Jaji Dk. Fauz Twalib, ambaye katika hukumu yake ya Julai 30, 2012 alikiri kuwa mbele yake halikufikishwa jalada la kesi hiyo na wala hakuwa na mamlaka ya kuisikiliza kwani yeye si hakimu, ila akasema kwa kuwa Mahakama ya Temeke haina mamlaka ya kusikiliza kezi za dawa za kulevya kama cocaine, basi akatoa fursa ya kumsikiliza mtuhumiwa.

 

“Kwa kasi ya aina yake, siku hiyo hiyo ya Julai 30, 2012 baada ya Jaji Dk. Fauz kutoa hukumu hiyo ya ajabu, mawakili wa Serikali ambao ni upande wa mashitaka wakawasilisha nolle chini ya Section 91 ya CPA (Sheria ya Mwenendo wa Mashitaka), hivyo Mwanasheria wa Serikali Mpembo kwa niaba ya DPP akawasilisha hati hiyo, na Jaji Fauz akaifuta kesi dhidi ya Mwinyi.

 

“Kisichoeleweka na kufahamika ni nini kilitokea na nini kiliendelea siku hiyo hiyo kutoa hukumu, na siku hiyo hiyo Mpembo akawasilisha nolle na kesi ikafutwa siku hiyo hiyo. Hapa kuna maswali mengi. Mwinyi amekimbilia Zanzibar. Yupo anaponda raha, kesi bado ipo Temeke na hakuna kinachoendelea,” kimesema chanzo chetu.

Baba yao Mwinyi na Rashid, naye kwa nyakati tofauti anadaiwa kukamatwa na polisi akituhumiwa kujihusisha na biashara ya dawa za kulevya. Mtoto wake mwingine, Abubakar Mkoko, yeye alitolewa dawa za kulevya tumboni, lakini Mahakama ikampiga faini ya Sh milioni 1 na kumwachia huru.

 

Kesi nyingine inayowakosesha usingizi polisi ni ile ya Dhoulkefly Awadh Abdallah Na. 238 ya Mwaka 2010. Kesi hii ilimhusisha Abdallah na mkewe Asha Seif Kiluvya. Asha ndiye aliyekamatwa na dawa za kulevya. Hata hivyo, katika mazingira ya kutatanisha, ofisi ya DPP ilipeleka nolle prosequi mahakamani Asha akaachiwa huru, na sasa anashitakiwa Abdallah ambaye hakukutwa na kitu chochote.

 

Kioja kinginge kilifanywa na Hakimu Mkazi wa Mahakama ya Kinondoni anayetajwa kwa jina la Msongo. Kesi hii ilianza mwaka 2005 na kumalizika mwaka 2008. Mshitakiwa alikuwa Yusufu Hassan Yossye, mkazi wa Kinondoni A, Mtaa wa Togo, aliyekutwa na gramu 1,244 za heroin ambazo alikamatwa nazo katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere, Dar es Salaam. Aliwekwa chini ya ulinzi kwa lengo la kumfanya atoe ‘pipi’ kwa njia ya haja kubwa. Katika hukumu ambayo inatia shaka Hakimu Msongo aliandika hivi:

 

“Katika ushahidi wote uliotolewa, hakuna ubishi kuwa ni kweli amekutwa na dawa za kulevya. Pia ushahidi unaonesha kuwa mshitakiwa alitoa madawa hayo kwa njia ya haja kubwa. Hata hivyo, upande wa mashitaka umeshindwa kueleza ni dalili zipi zilipelekea (zilisababisha) kushukiwa kuwa mshitakiwa ana madawa ya kulevya. Na pia hawakushirikishwa watu au wataalamu wa afya ya binadamu.

 

“Upande wa mashitaka katika ushahidi wao umeonesha walipishana kutoa idadi [ya pipi alizotoa kwa haja kubwa]. Kutokana na hilo, ushahidi hautoshelezi na mshitakiwa namwachia chini ya Kifungu cha 235 cha CPA (Kanuni ya Mwenendo wa Mashitaka) katika mashitaka yote mawili.” Hukumu hii ilitolewa na Hakimu Msongo Mei 2, 2008. Yossye alikuwa akishitakiwa kwa kukutwa na dawa; na pia kwa kuwaambia polisi uongo kuwa hakuwa na dawa, lakini baadaye akazitoa kwa njia ya haja kubwa.

Katika Mahakama ya Kisutu, mwanamke mwingine aliyetambuliwa kwa jina la Pilly, alikamatwa Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere akiwa na zawadi ya kinyago ambacho ndani yake kilikutwa na dawa za kulevya, lakini Mahakama ya Kisutu wakati inatoa taarifa ilimwachia huru Pilly kwa maelezo kuwa wakati polisi wanamkamata, hakuwapo mwanamke, hivyo ni kosa mhalifu mwanamke kukamatwa na polisi mwanaume. Akaachiwa huru!

 

Kesi nyingine ni ya Kwaku Sarfo, raia wa Ghana, alikamatwa Uwanja wa Ndege wa Julius Nyerere mnamo Novemba 14, 2010. Thamani ya dawa ilikuwa Sh milioni 390. Kesi ilipelekwa Mahakama ya Hakimu Mkazi Samora kwa Hakimu Mkazi Luago.

 

“Tulishangaa, kwamba kwanza Mahakama hii haina mamlaka ya kusikiliza kesi hii, lakini pia baada ya kupita siku 60; bila mamlaka kisheria, Hakimu Luago akaifuta. Hakimu huyu ni kero. Amehamishiwa Lindi akagoma kwenda. Hatujui anapewa jeuri na nani. Tungeomba Rais Kikwete na mhimili wa Mahakama waingilie kati suala hili vinginevyo nchi inateketea,” kimesema chanzo chetu.

 

Uchunguzi umebaini kuwa kati ya kesi 423 zilizofikishwa Mahakama Kuu kati ya mwaka 2005 na 2013 hadi leo kesi iliyokwisha ni moja tu ya Shaaban Mintanga, ambayo nayo imeisha kutokana na mashahidi muhimu kufariki dunia kabla kesi haijasikilizwa. Kati ya mashahidi waliofariki dunia ni Mkemia Mkuu, Dk. Ernest Mashimba, aliyefariki Septemba 2010.

 

Kamanda wa Kikosi Maalumu cha Kuzuia Dawa za Kulevya, Godfrey Nzowa, alikiri matukio hayo kuwapo na akasema: “Mimi mamlaka yangu ni kukamata, na kuwafikisha mahakamani. Sasa huko kama mmekuta hali iko hivyo, ambayo ni kweli kimsingi inasikitisha na kukatisha tamaa, inabidi muwaulize huko mahakamani au kwa DPP wao ndiyo waeleze nini kinatokea.”

 

JAMHURI haikufanikiwa kuzungumza na Msajili wa Mahakama Kuu kwani mara zote kila mwandishi wetu alipofika aliambiwa yuko kwenye vikao kwa wiki nzima, na hata alipoacha ujumbe wa maandishi haukujibiwa.

 

Baada ya juhudi za kumpata Msajili wa Mahakama Kuu kugonga mwamba, JAMHURI iliwasiliana na Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera na Uratibu wa Bunge), William Lukuvi, ambaye Kamisheni ya Dawa za Kulevya iko chini yake. Yeye alisema ni kweli tatizo hilo lipo, na kwamba kuna mengi zaidi ya hayo.

 

“Mimi nasema sheria zinapaswa kubadilishwa, na Serikali tayari imeanza mchakato. Mtu akipatikana na pipi za dawa za kulevya zikatolewa tumboni mwake, nataka sheria irahisishwe na kuwezesha ashitakiwe na kufungwa maisha ndani ya siku saba.

 

“Hali ilivyo sasa ambapo unapaswa kuhifadhi ushahidi kwa miaka hadi 10 ukiendesha kesi moja, ushahidi unapoteza ubora. Wakati mwingine mtuhumiwa anashindwa kesi anatozwa faini ya Sh 500,000. Hatuwezi kupambana na dawa za kulevya tukashinda vita hii kwa utaratibu huo.

 

“Sasa Serikali imejipanga, ipo kwenye mchakato wa kuanzisha mahakama maalum ya kudhibiti dawa za kulevya na kwa kweli katika hili tunataka mchakato uwe mfupi kadiri inavyowezekana. Ndani ya muda mfupi kadiri inavyowezekana tupitishe sheria hii ili sheria iwe kali itoe adhabu itakayowazuia wengine kufanya biashara hii,” alisema Lukuvi.

 

Hivi karibuni, Tanzania imeanza kuzungukwa na sura ya kuwa Taifa la wauza dawa za kulevya baada ya Watanzania wengi kukamatwa ndani na nje ya nchi wakiwa na dawa hizo. Taarifa za uhakika zilizoifikia JAMHURI zinasema Rais Jakaya Kikwete ametoa maelekezo ya dhati kuhakikisha linafanyika jambo kubwa litakalowezesha kukamata mtandao wa wauza dawa za kulevya na kumaliza tatizo hili nchini.

 

Kwa mwezi mmoja sasa, JAMHURI imekuwa ikichapisha orodha ya wauza unga ‘dagaa’ na ‘mapapa’ hapa nchini, ambako hadi sasa gazeti hili limekwishatangaza hadharani majina ya wauza unga 504 katika matoleo manne yaliyotangulia.

 

Bosi wa Masogange anaswa na unga

*Anaswa na kilo 50 Nairobi, zinafanana na za wanamuziki

*‘Unga’ wagonganisha majaji, mahakamani watafutana

 

Na Waandishi Wetu, Dar & Nairobi

Wakati Mahakama Kuu ikituhumiwa kuharibu mwenendo wa kesi za dawa za kulevya nchini kwa kutoa hukumu zinazopingana na sheria zilizotungwa na Bunge, mtu anayetuhumiwa kuwa ndiye aliyewapatia mzigo wa kilo 180 za dawa za kulevya wanamziki – Agnes Jerald (Masogange) na Melisa Edward waliokamatwa Afrika Kusini Julai 5, naye amekamatwa na unga.

 

Masogange na Edward walikamatwa katika Uwanja wa Oliver Thambo wakiwa na mabegi tisa yanayofanana ndani yake yakiwa yamebeba dawa za kulevya aina ya methamphetamine, na kwa taarifa za kiuchunguzi ilizozipata JAMHURI, mtu aliyetambulika kwa jina la Rumishaeli Mamkuu Shoo anayedaiwa kuwa bosi wa akina Masogange amekamatwa Nairobi, Kenya.

 

“Amekamatwa jana (Alhamisi, Agosti 29) jijini Nairobi akiwa na dawa aina ya methamphetamine kilo 50,” chanzo cha uhakika kiliijulisha JAMHURI. “Pamoja naye, amekamatwa akiwa na mtu mwingine anayeitwa January Gabriel Liundi wakiwa na gari aina ya RAV 4 nyeusi Na T 410 CLF.” Chanzo kingine kilisema dawa walizokamatwa nazo ni ephedrine ambazo hutumika kutengeneza methamphetamine.

 

Uchunguzi unaonesha kuwa kabla ya Shoo kukamatwa, mama yake alikuwa anahaha makao makuu ya polisi na Mkoa wa Kipolisi Ilala, akiomba Shoo asiangukie mikononi mwa Kamanda Godfrey Nzowa wa Kitengo cha Kuzuia Dawa za Kulevya.

 

“Yule mama alikuwa analia anasema Nzowa akimkamata atamweka ndani,” kilisema chanzo chetu.

JAMHURI ilipowasiliana na Nzowa, alikiri kusikia taarifa hizo ila akasema atazizungumzia zaidi baada ya kupata taarifa rasmi kutoka Jeshi la Polisi Nairobi. “Nimezisikia, na ni kweli tulimkamata Julai 7 baada ya kuwa wale mabiti (Masogange na Edward) wamemtaja, hatukumkuta na mzigo ila tukamweka chini ya uangalizi, na sasa kabla hajaja kuripoti, nimepata taarifa kuwa amekamatwa na dawa hizo Nairobi. Nitawajulisha nikipata taarifa kamili,” alisema Nzowa.

 

Wakati bosi wa Masogange akinaswa, JAMHURI imepata hukumu mbili zinazoonesha Mahakama inavyopingana wazi nchini kuhusiana na kesi za dawa za kulevya.

Hukumu iliyotolewa na Jaji Upendo Msuya ndiyo inayoumiza vichwa wanasheria na Serikali kwa ujumla, kwani imekinzana wazi na sheria ya nchi kwa kutumia sababu dhaifu za kisheria. Katika kesi iliyowahusisha Watanzania wawili na Wapakistani wawili – Fredy William Chonde, Kambi Zuberi Seif, Abdul Ghan Peer Bux na Chambaz Malik, Jaji Upendo Msuya alitoa dhamana kwa kosa lisilodhaminika.

 

Jaji Msuya katika kesi hii ya mwaka 2011, alisema alitumia Ibara ya 148 (5) (a) (iii) kuwaachia watuhumiwa hao waliokuwa na jumla ya kilo 179 za heroin iliyokadiriwa kuwa na thamani ya Sh 6,265,000,000 kwa maelezo kuwa Kamishna wa Kamisheni ya Kuzuia Dawa za Kulevya nchini hakuambatanisha cheti cha thamani iliyothibitishwa ya mzigo uliokamatwa.

 

Hawa walikamatwa Februari 2011 katika Mtaa wa Jogoo, Mbezi Beach uliopo Wilaya ya Kinondoni, Dar es Salaam.

Pia alisema katika hati ya mashitaka, walalamikaji hawakuweka umri wa walalamikiwa, hivyo akakubaliana na hoja za mawakili wa walalamikaji Michael Mwambeta na Yasin Memba akawapa dhamana na kuagiza warejeshewe hati zao za kusafiria. Siku hiyo hiyo, Wapakistani walikimbia nchi na Watanzania wawili inaelezwa kuwa nao kuna nyakati walikimbilia Afrika Kusini.

 

Sura ya 27 (1) (a) ya Sheria ya Kuzuia Dawa za Kulevya, inatamka bayana kuwa mtu aliyekutwa na heroin au cocaine na dawa za kulevya nyingine zilizoorodheshwa hapaswi kupewa dhamana, lakini Jaji Msuya alisema kukosekana kwa hati ya Kamishna wa Tume ya Kudhibiti Dawa za Kulevya yenye kuonesha thamani, inaweza ikawa ishara ya watu hawa kubambikiwa kesi, hivyo akaamuru waachiwe huru.

 

Upande wa mashitaka ukiongozwa na mawakili wa Serikali Mangowi na Mfikwa, ulisema kuwa sheria inataka watuhumiwa kufikishwa mahakamani ndani ya saa 24 na hivyo uchunguzi ulikuwa bado unaendelea, na wakaomba kuwa hivyo vyote vinavyodaiwa kuwa vinapungua wangeviwasilisha wakati wa hatua ya awali ya kusikiliza kesi, lakini Jaji Msuya akasema hakubaliani nao kwani hilo likiruhusiwa linaweza kuruhusu raia wema kubambikiwa kesi.

 

Wakati Jaji Msuya akitoa hukumu ya aina hiyo, Jaji mwenzake Kipenka Mussa, alipingana wazi na Jaji Msuya katika kesi dhidi ya Ramadhani Athumani Mohamed, Ally Mohamed Abdallah, Issa Abdallahman Soud na Rashid Mohamed Flashman, iliyotolewa Septemba 9, 2011.

 

Watuhumiwa hawa ambao wako rumande hadi sasa, walikutwa na kilo tatu za cocaine zenye thamani ya Sh milioni 202,500,000. Mahakama ya Hakimu Mkazi Tanga, ilikuwa imewapatia dhamana kwa kutumia kigezo cha hukumu iliyotolewa na Jaji Msuya awali, kwa mazingira yale yale kuwa washitakiwa walipofikishwa mahakamani dawa walizokamatwa nazo hazikuwa na hati ya kuthibitisha thamani ya dawa hizo kutoka kwa Kamishna wa Tume ya Dawa za Kulevya Nchini.

 

Mkurugenzi wa Mashitaka (DPP) alikata rufani kwenye Mahakama Kuu Kanda ya Tanga kupinga dhamana hiyo, kwa maelezo kuwa kosa la kukutwa na dawa za kulevya kwa mujibu wa sheria iliyotajwa hapo juu halina dhamana, lakini pia kwa maelezo kuwa Mahakama ya Hakimu Mkazi haina mamlaka ya kutoa dhamana kwa kesi ambazo haina uwezo wa kuzisikiliza na hazidhaminiki.

 

Akitoa hukumu yake, Jaji Mussa alisema kwa masikitiko analazimika kupingana na hukumu ya Jaji mwenzake Msuya, ambayo ilitafsiri sheria bila kuangalia nia ya wabunge wakati wanatunga sheria hiyo. Alisema pia kwa mazingira ya watuhumiwa kutakiwa kufikishwa mahakamani ndani ya saa 24 na ukubwa wa Tanzania, kusema kuwa ndani ya muda huo Kamishna awe ametoa hati ya thamani ya dawa za kulevya nchi nzima ni kujidanganya.

 

Jaji Mussa alisema nia ya msingi ilikuwa ni kutoa adhabu kali itakayozuia watu kufanya biashara ya dawa za kulevya zenye madhara makubwa kwa Taifa na kizazi chote kwa ujumla, hivyo akafunga dhamana ya watuhumiwa hao na kuagiza sheria hiyo irekebishwe kufuta kifungu cha kutaka hati ya thamani kutolewa, kwani kinasaidia wahalifu kuendelea kufanya biashara hii.

 

Hadi sasa Mahakama haijatoa chapisho maalum kubainisha ni hukumu ipi iko sahihi kati ya ile ya Jaji Msuya na hii ya Jaji Mussa, hali inayowafanya mahakimu na watumishi wa Mahakama kuchagua hukumu ya kutumia wanayoona inawafaa kulingana na matakwa yao au ya kisheria.

Pamoja na mgongano huo mahakamani, Ofisi ya Mwendesha Mashitaka wa Serikali (DPP), nayo imelaumiwa kwa kufuta kesi katika mazingira ambayo hata mtu ambaye hakusoma sheria, anaweza kuyatilia shaka.

 

Wakati vyombo hivi vikikwamisha vita hii, lawama zimekuwa zikielekezwa kwa polisi na vyombo vingine vya usalama, ambavyo watendaji kazi wake wanafanya kazi usiku na mchana. Juhudi zote zinazofanywa na vyombo vya ulinzi na usalama zinagonga mwamba mahakamani kwa msaada wa ofisi hiyo ya DPP. Wakati kesi nyingine zikifutwa, nyingine hazisikilizwi, kiasi cha kusababisha zirundikane mahakamani tangu mwaka 2005. Kesi chache zinazohusu watuhumiwa wakubwa wa kuuza ‘unga’ zinamalizwa haraka kwa utaratibu wa ofisi ya DPP kuwasilisha nia ya kutoendelea na mashtaka mahakamani (nolle prosequi) au wasimamizi hao wa utoaji haki kutoa hukumu zinazoacha wengi vinywa wazi na kuwakatisha tamaa polisi.

 

Katika hali ya kushangaza, majaji na mahakimu wamekuwa wakikiuka wazi Sheria ya Kuzuia Dawa za Kulevya Na, 9 ya Mwaka 1995 inayozuia mtu yeyote aliyekamatwa na dawa zenye thamani kuanzia Sh milioni 10 asipewe dhamana, lakini hilo halizingatiwi.

 

JAMHURI haikubahatika kufahamu bayana nini kinawapofusha majaji na mahakimu wakati ‘mapapa’ wanapofikishwa mahakamani kwa tuhuma za kuuza unga, lakini ni wazi kuwa kuna mtandao mkubwa wa kulindwa kwa watuhumiwa hao wenye ukwasi mkubwa.

Wakati polisi wanafanya kazi ya hatari usiku muda wote, wakipambana na wauaji, wahongaji na watu wanaouza dawa za kulevya, kesi za mapapa zinamalizwa kienyeji mahakamani.

 

Habari za kuaminika zilizoifikia JAMHURI zinaeleza kuwa kesi nyingi sasa zimepangiwa majaji zianze kusikilizwa baada ya JAMHURI kulipua kadhia hii na Serikali inajiandaa kuunda Mahakama Maalum ya Kesi za Dawa za Kulevya. Hili atalitangaza Rais Jakaya Kikwete muda wowote akirejea nchini kutoka safarini Ulaya.

 

Kwa mwezi mmoja sasa, JAMHURI imekuwa ikichapisha orodha ya wauza unga ‘dagaa’ na ‘mapapa’ hapa nchini, ambako hadi sasa gazeti hili limekwishatangaza hadharani majina 504 ya wauza unga katika matoleo manne yaliyotangulia.

 

2035 Total Views 1 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!