Vyombo vya usalama nchini Uganda vimewaonya wananchi wa Uganda walioko nje ya nchi ambao wanatoa matamko ya kuvunja amani, utulivu na haki binafsi za mtu yoyote hususan viongozi, watashughulikiwa ipasavyo watakapo rejea nchini.

Onyo hilo limetolewa kufuatia kukamatwa kwa mtoto wa Mkuu wa Chuo cha Makerere wa zamani, ambaye polisi wanamtuhumu kwa kutumia lugha ya matusi wakati wa maandamano yaliyofanywa na wahamiaji wa Uganda nchini Marekani, yaliyokuwa yanashinikiza kuachiwa kutoka kizuizini jeshini Mbunge Robert Kyagulanyi wa jimbo la Kyadondo Mashariki.

Kato Kajubi, ambaye ni mtoto wa Marehemu Profesa William Ssenteza Kajubi, alikamatwa alipowasili uwanja wa ndege wa kimataifa wa Entebbe wiki iliyopita na kuendelea kuwekwa kizuizini hadi Jumatatu ambapo alipewa dhamana alipofikishwa polisi.

Vicent Ssekatte, msemaji wa Kitengo cha uchunguzi wa makosa ya jinai, amesema wapelelezi bado wanachambua lugha chafu iliyotumiwa na Kajubi.

“Amepewa dhamana na amesalimisha pasi yake ya kusafiria polisi na atapewa pasi hiyo baada ya uchunguzi kumalizika,” Ssekatte amesema Ijumaa.

Hii ina maanisha kuwa Kajubi hataweza kusafiri nje ya nchi siku za karibuni ili kuwasaidia familia yake, ambapo wakati mwengine polisi huchukuwa miezi kadhaa kabla ya kukamilisha uchunguzi.

Please follow and like us:
Pin Share