Na Daniel Limbe,Jamhuri Media,Geita

UAMUZI wa Mabaraza ya madiwani kupanga gharama za mafunzo ya vitendo kwa wanafunzi wa vyuo vya Afya,umetajwa kuwa mzigo mzito kwa uendeshaji wa taasisi hizo kutokana na baadhi ya wanafunzi kushindwa kumudu gharama hizo.

Changamoto hiyo imekuwa ikivikumba vyuo vya afya vya kati baada ya kuwapeleka wanafunzi wao kwenye hospitali za wilaya kwaajili ya mafunzo kwa vitendo,ambapo hutakiwa kulipa gharama kubwa kinyume na mwongozo wa Wizara ya afya.

Akizungumza kwenye mahafali ya saba ya Chuo cha Sayansi za afya na teknolojia Chato,Mkurugenzi wa taasisi hiyo, Dkt. Joel Maduhu,amesema serikali inapaswa kuwasisitiza wakurugenzi wa halmashauri za wilaya kusimamia mwongozo wa gharama za matibabu kama ulivyoainishwa na wizara ya afya badala ya uamuzi wa vikao vya madiwani.

Licha ya kujivunia kwa matokeo mazuri ya wahitimu wa Chuo hicho,Dkt.Maduhu ameiomba serikali kuvisaidia vyuo hivyo ili viweze kutoa wahitimu wenye ujuzi mzuri utakao kuwa msaada kwa jamii hasa katika maeneo ya vijijini ambapo ujenzi wa zahanati na vituo vya afya unaendelea kufanyika licha ya upungufu mkubwa wa watumishi.

“Tumekuwa tukisumbuliwa sana kwa wanafunzi wetu kutakiwa kulipia kiasi kikubwa cha fedha kwa kila mwanafunzi anapokuwa kwenye mafunzo ya vitendo,kwa maelezo kuwa Baraza la madiwani limepitisha gharama hizo ambazo ni kinyume na mwongozo wa Wizara ya elimu” amesema Dkt. Maduhu.

Amesema kufanya hivyo ni kuzima ndoto za wanafunzi wanaotoka familia masikini kutokana na kushindwa kumudu gharama hizo, licha ya kuwa serikali bado inahitaji kupata watumishi wenye ubora wa hali ya juu ili kuwahudumia wananchi.

“Napendekeza ikiwezekana gharama za mafunzo kwa vitendo ziondolewe kabisa kwa sababu hazina tija,maana tunaweka vikwazo kwa wanafunzi wetu ambao siku za baadaye serikali itawahitaji ili wahudumie jamii ya watanzania” amesema.

Kwa mujibu wa gharama zilizoainishwa na mwongozo wa Wizara ya afya wa mwaka 2020, kwa idadi ya wanafunzi 1 hadi 25 wanapaswa kulipia kisasi cha sh. 250,000 na wanafunzi 25 hadi 50 wanapaswa kulipia sh. 500,000 kwa mwaka mmoja.

Kadhalika kwa wanafunzi kuanzia 50 hadi 100 wanapaswa kulipia sh. 750,000 na 100 na kuendelea hupaswa kulipia 1,500,000 kwa kipindi cha mwaka mzima.

Baadhi ya wahitimu wa kada za afya kwenye chuo hicho,Winfrida Vicent na Joseph Nyakuya,wamesema uwepo wa gharama kubwa za mafunzo kwa vitendo umekua ukiathiri ujifunzaji wao kutokana na baadhi ya wanafunzi kushindwa kumudu gharama hizo.

“Hizi gharama za mafunzo kwa vitendo zimekuwa mzigo mzito kwa wazazi wetu kutokana na baadhi yetu kutoka katika familia duni,licha ya wazazi kujibana ili watoto wao tupate elimu kwa manufaa yetu na jamii kwa ujumla” amesema Nyakuya.

“Tunaiomba serikali iongeze bajeti ya wizara ya afya ikiwa ni pamoja na kuajili watumishi wa kada hii hatua itakayosaidia kuongeza ubora wa huduma za afya kwa jamii sambamba na kupunguza vifo visivyokuwa vya lazima hasa vijijini” amesema Winfrida.

Amesema kuboreshwa kwa huduma za afya hasa ngazi ya zahanati na vituo vya afya itasaidia sana kunusuru maisha ya wananchi hasa kudhibiti vifo vya mama na mtoto ambavyo hutokea kutokana na kukosekana kwa huduma bora kwenye maeneo yao.

Kwa upande wake Mgeni rasmi katika mahafali hayo ambaye ni mjumbe wa halmashauri kuu ya Chama cha Mapinduzi(CCM) taifa, na mwenyekiti wa Chama hicho mkoa wa Geita,Mwl. Nichoraus Kasendamila, ameonyesha kushangazwa na vikwazo vya gharama za mafunzo kwa vitendo kwa wanafunzi wa kada za afya na kudai suala hilo lazima lipatiwe ufumbuzi wa haraka kwa sababu afya ni hitaji muhimu kwa kila mtanzania.

“Nimepokea Changamoto zote zilizosemwa hapa mimi kama kiongozi mkuu wa CCM mkoa wa Geita,Chama kinachoisimamia serikali iliyopo madarakani nakwenda kulifanyia kazi jambo hili,kwani vipo vyanzo vingi vya kukusanya mapato ya halmashauri kuliko kutoza gharama hizi kwa wanafunzi,nitaenda kupitia vyanzo vyote vya mapato halafu nitawashauri wafute hiki na wakusanya kile” amesema Kasendamila.

                    
Please follow and like us:
Pin Share