Wadau wa habari nchini wameendelea kuipinga sheria inayomtambua mwandishi wa habari kuwa mtu ambaye amepata elimu ya stashahada.

Wakizungumza katika mkutano ulioratibiwa na Chama cha Waandishi wa Habari Mkoa wa Mwanza (MPC) hivi karibuni, wadau hao walidai kuwa pamoja na kuwa ni taaluma, lakini kazi ya uandishi wa habari inaweza kufanywa pia kupitia vipaji, wakitolea mifano katika kitengo cha utangazaji.

Walionyesha kushangazwa kwao na matakwa ya kielimu kwa waandishi wa habari wakati wabunge walikataa kuwekewa kiwango cha elimu wakati wa mjadala wa katiba mpya miaka kadhaa iliyopita.

Abubakar Karsan, Mkurugenzi wa Muungano wa Vyama vya Waandishi wa Habari Tanzania (UTPC), amesema sheria hiyo inapaswa kuondolewa kwa sababu ilitungwa kwa shinikizo la watu wenye masilahi binafsi na suala hilo.

“Ulikuwa mchakato mgumu sana. Wengine waliomba hadi fedha kwenye balozi hapa nchini ili kuwalipa wajumbe wakati wa mchakato wa kutungwa kwa sheria hii. Bado tunaiomba serikali kuiondoa au iwatambue waandishi mchundo wenye elimu ya cheti,” amesema Karsan.

Hata hivyo, baada ya kupitishwa kwa sheria hiyo, UTPC ilitangaza ufadhili kwa waandishi ambao wangependa kujiendeleza kielimu na waandishi 211 waliomba.

Kwa upande wake, Clara Matimo, mwandishi wa habari jijini Mwanza alihoji sababu ya wabunge kukataa mapendekezo ya wananchi kuwa na ukomo wa elimu na wakati huo huo kushinikiza waandishi wawe na kigezo hicho.

James Nhende, mmiliki wa Gazeti la Mzawa jijini hapa, ameshauri serikali isiwaadhibu wanahabari wenye elimu ngazi ya cheti.

“Sipingi vijana kusoma, wasome. Ila walio na vyeti wathaminiwe pia na kuachwa kazini,” amesema mzee Nhende.

Hata hivyo, Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Mawasiliano nchini (TCRA), James Kilaba, amewataka waandishi wa habari nchini kuizingatia sheria hiyo kwa sababu inafanya kazi.

Akizungumza katika mkutano huo, Kilaba alibainisha kuwa vituo vya redio, televisheni zikiwamo za mtandaoni, zinazokiuka maudhui ya utangazaji zitakabiliwa na adhabu kupitia sheria hiyo.

Kilaba amesema katika kipindi ha miaka minne iliyopita, kumekuwa na ongezeko la vyombo vinavyotoa huduma za maudhui mtandaoni, kwani kuna leseni 46 hadi mwezi uliopita.

Kilaba, anayeongoza taasisi yenye dhamana ya kisheria kusimamia mawasiliano ya simu, posta, utangazaji pamoja na mawasiliano kielektroniki, amewataka wamiliki wa vyombo hivyo vya habari kutii masharti ya leseni zao.

“Utengenezaji na urushaji wa maudhui unatakiwa kuzingatia misingi yote ya sheria. Maudhui yasilete uchochezi, kupotosha, uzushi na kukashifiana. Hili ni jukumu kubwa ambalo linatakiwa kusimamiwa kwa weledi, pamoja na kupata ushirikiano mkubwa kutoka kwa wadau,” amesema Kilaba. 

Hivi karibuni, TCRA ilitoa matangazo kupitia vyombo vya habari ikivionya vituo vya televisheni kuacha kuwatumia watu wasio na taaluma ya uandishi wa habari kama watangazaji.

Kwa mujibu wa Kifungu cha 19 (1) cha Sheria ya Vyombo vya Habari ya mwaka 2016, kufanya kazi ya uandishi wa habari pasipo kuthibitishwa kwa mujibu wa sheria ni kuvunja sheria.

Vivyo hivyo, Kanuni ya 17 (2) ya Kanuni za Vyombo vya Habari 2017, nayo inaeleza wazi kwamba: “Ili mtu athibitishwe kuwa mwandishi, pamoja na mambo mengine anatakiwa kuwa na Shahada (Digrii) au Stashahada (Diploma) ya Uandishi wa Habari; au inayohusiana na masuala ya vyombo vya habari, kutoka katika chuo kinachotoa elimu ya masuala hayo.

By Jamhuri