Baraza la Taifa la Hifadhi ya Mazingira (NEMC) limewaonya watu wanaokuka chakula kwa mama lishe ambao wanatumia karatasi za plastiki kufunika vyakula vyao kuwa wanakabiliwa na hatari ya kupata ugonjwa wa saratani.

Aidha, NEMC pia imetoa onyo kwa watu wanaopenda kutumia nguo za ndani zilizotumika (mitumba) kuwa nao wanakabiliwa na hatari ya kuambukizwa magonjwa mbalimbali ikiwamo saratani na magonjwa ya ngozi.

Ofisa Mazingira wa NEMC, Jarome Kayombo, ameliambia JAMHURI kuwa karatasi za plastiki ni hatari kwa afya za binadamu zinapotumika kufunikia chakula, hasa kinapokuwa cha moto.

Kayombo amesema jambo baya ni kuwa chembechembe za plastiki kutoka katika karatasi hizo huyeyushwa na joto na kuingia kwenye chakula na hatimaye kwenye mwili wa mtu anayekila chakula hicho.

“Tatizo ni kuwa chembechembe hizi huingia mwilini taratibu sana, hivyo inachukua muda mrefu sana kwa mwathirika kugundua tatizo lake,” amebainisha Kayombo.

Amesema wametumia muda mwingi kuielimisha jamii kuhusu madhara ya karatasi za plastiki kwa binadamu, mifugo na mazingira ili watu wabadilishe tabia.

Kayombo amesema kulingana na kemikali zinazotumika kutengeneza karatasi hizo, madhara kwa mtumiaji yanaweza kuonekana baada ya  miaka 50 hadi 500.

Mifuko mbadala

Kayombo amewaonya watu wanaotumia mifuko ya plastiki myeupe wakiamini kuwa imeruhusiwa kutumika.

Amesema serikali imepiga marufuku matumizi ya mifuko ya plastiki ya aina zote nchini na anayetaka kuruhusiwa kutumia bidhaa za plastiki kwa ajili ya vifungashio anapaswa kuomba kibali serikalini.

Alitoa mfano wa Kampuni ya Bakhresa ambayo imeomba na kuruhusiwa kutumia vifungashio vya plastiki kwa ajili ya maziwa, mikate na bidhaa nyingine.

Hata hivyo, Zuhura Hamisi, anayefanya biashara ya mama lishe katika eneo la Vinguguti Machinjioni, amesema wanalazimika kutumia karatasi za plastiki katika kazi zao kwa sababu zinasaidia kuivisha chakula vizuri.

“Tunanunua karatasi hizi za plastiki katika maduka wanayouza vifungashio na tunazitumia wakati wa kupika na wakati wa kuhifadhi ili kutunza joto la chakula,” amesema.

Nguo za ndani

Akizungumza na JAMHURI, Ofisa Uhusiano wa Shirika la Viwango Tanzania (TBS),Roida Kayuni, ameonya kuwa matumizi ya nguo za ndani za mitumba ni hatari sana kiafya kama ilivyo kwa vipodozi ambavyo havikidhi viwango vya ubora.

Amesema matumizi ya nguo hizo husababisha maambukizi ya maradhi mbalimbali, ikiwemo saratani na magonjwa ya ngozi.

Amesema inasikitisha kuona kuwa licha ya elimu ambayo wamekuwa wakiitoa kwa jamii kuhusiana na madhara ya kutumia nguo za ndani za mitumba na vipodozi vyenye kemikali hatari bado watu wengine katika jamii wanaendelea kuzitumia bidhaa hizo.

By Jamhuri