Tunapozungumzia uhuru wa habari tunakuwa na maana mbili. Kwanza, uhuru wa vyombo vya habari kutoa habari zilivyo bila kutishwa au kusumbuliwa. Pili, uhuru wa wananchi kupewa habari zilivyo bila vikwazo au kufichwa.
Kwa upande wa vyombo vya habari, vimetajwa kuwa ni Mhimili wa Nne wa Dola (ingawa si rasmi) baada ya Serikali, Bunge na Mahakama.
Kwa Tanzania, uhuru wa habari kidogo unatia wasiwasi. Hii ni kwa sababu sheria zinazokandamiza uhuru wa vyombo vya habari bado zipo ingawa Tume ya Nyalali ilipendekeza zaidi ya miaka 20 iliyopita zifutwe. Kwa hivyo, mapambano ya vyombo vya habari kutafuta uhuru kamili wa vyombo hivyo yanaendelea.
Kwa upande wa suala la wananchi kupewa taarifa za habari na vyombo vya habari miaka hii, waandishi wa habari vijana wamekuwa tatizo kubwa, wanawanyima wananchi habari katika kutafuta maslahi yao binafsi.
Ukitaka kusema ukweli katika Tanzania ya leo vijana wamezuka kuwa tatizo kubwa katika kila sekta ya maisha. Kwa mfano, walimu wengi vijana ni mzigo shuleni, hasa kwa walimu wakuu. Wanapojiunga na shule fulani wanajifanya wanajua zaidi kuliko walimu waliowakuta ikiwa ni pamoja na Mwalimu Mkuu. Wanataka yafuatwe yao tu. Nasikia huwaambii kitu!
Kuna habari kwamba walimu vijana wakiambiwa kwenda kwenye semina; cha kwanza wanachotaka kujua si semina itahusu nini bali watapata posho kiasi gani?
Sitaki kuleta picha kwamba walimu wote vijana ni wabaya. Si suala la kuoza samaki mmoja na wote huoza. Wapo walimu vijana wazuri sana lakini wanahesabika. Isitoshe lengo langu si kuzungumzia walimu vijana. Nawazungumzia waandishi wa habari vijana.
Mwaka 2011 niliendesha semina ya uraia kwa walimu wa Halmashauri ya Manispaa ya Kinondoni. Waandishi wa habari wakapata habari mapema ya kuwapo kwa semina hiyo, wakaja jumla yao 12. Tuliwapa soda waandishi wote pale Shule ya Msingi Mwananyamala “B”. Baada ya shughuli za ufunguzi wa semina nikapewa ujumbe kuwa nilikuwa naitwa na waandishi wa habari nikaenda kuwaona.
Wakanitaka niwape nauli ili wawe na nafasi nzuri ya kutoa taarifa kwa wananchi. Nikawaambia sikuwa na nauli ya kuwapa, kwa hiyo walioripoti habari hizo ni gazeti moja na TV moja tu. Vyombo hivyo vya habari ndivyo vilivyoleta waandishi wa habari vijana waadilifu.
Aprili 25, mwaka huu, kulikuwa na semina ya uraia Shule ya Msingi Kinondoni, ambayo mgeni rasmi alikuwa alikuwa Naibu Meya wa Halmashauri ya Manispaa ya Kinondoni. Kutokana na ninavyoendesha semina hizi kwa kujitolea bila kuzitoza shule chochote katika kutambua kuwa shule hazina fedha, Naibu Meya alizungumza maneno mazuri juu yangu.
Katika semina ile kulikuwa na waandishi wa habari wanne, niliwapa nafasi ya kujitambulisha kwa walimu na kwa wageni rasmi, pia tuliwapa soda. Mwisho wa semina nikapewa ujumbe kwamba waandishi wa habari walikuwa wanataka kuniona. Nikawafuata.
Wakanipongeza kwa maneno mazuri ambayo Naibu Meya alikuwa amezungumza juu yangu. Wakataka niwape nauli ili wakatoe habari hizo kwenye vyombo vyao vya habari.
Sikuwa na nauli yoyote ya kuwapa kwa sababu semina haikulipiwa; wakaenda zao. Wakawanyima wananchi uhuru wa kupata habari hizo. Hawakutoa taarifa yoyote.
Hivi ndivyo waandishi wa habari vijana wanavyojidhalilisha na wanavyodhalilisha vyombo vyao vya habari.