Na Isri Mohamed, JamhuriMedia, Pwani

Waandishi wa habari wawili waliokuwa wakitokea Dar es Salaam kuelekea Lindi wamefariki baada ya gari walilokuwa wamepanda kugongwa na gari aina ya Canter.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kipolisi Rufiji, Protas Mutayoba, amethibitisha kutokea kwa ajali hiyo iliyotokea katika eneo la Nyamwage wilayani Rufiji mkoani Pwani usiku wa kuamkia leo.

Kamanda amewataja marehemu kuwa ni Abdallah Nanda wa Channel Ten na Josephine Kibiriti wa Sahara Media Group.

Kamanda Mutayoba amesema kuwa waandishi hao walikuwa wakitokea Dar es Salaam kuelekea Lindi kwenye mafunzo wakiwa na gari ndogo ambapo waligongwa na gari kubwa aina ya Canter na baada ya ajali hiyo dereva wa gari hilo alikimbia.

Amesema kwenye gari ndogo ya waandishi walikuwemo watu watatu, wawili wanawake na mmoja mwanaume, ambapo wawili wamefariki papo hapo na mmoja ni majeruhi amekimbizwa hospitali na mguu wake mmoja ukiwa umeshavunjika.

Kamanda Mutayoba amesema eneo lilipotokea ajali hiyo lina miundombinu mizuri na halina changamoto yoyote na juhudi za kumsaka dereva aliyesababisha ajali hiyo zinaendelea na maiti zimehifadhiwa katika kituo cha afya Ikwiriri.

Aidha Kamanda Mutayoba ametoa onyo na msisitizo kwa madereva na watumiaji wa barabara kufuata sheria za usalama barabarani.