Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia, Dar es Salaam

Ubomoaji nyumba zilizofidiwa katika Mradi wa Uendelezaji wa Bonde la Msimbazi unatarajiwa kuanza Aprili 12, 2024, na litawahusu waathirika 2,155 ambao tayari wamelipwa fidia.

ambaye ni Mratibu wa Miradi ya Ushirikiano na Benki ya Dunia TARURA amesema kwa mujibu wa makubaliano ya utekelezaji wa zoezi hilo, waathirika wa mradi ambao wameshakwishapokea malipo yao wanatakiwa kuhamisha mali zao na kupisha eneo la mradi ndani ya wiki sita baada ya kupokea fedha hizo kwenye akaunti zao.

“Waathirika tayari wameshalipwa fidia na tumewapa muda wa kuhama ambao ni makubaliano ya kimkataba yanayowataka kuhama ndani ya wiki sita mara tu baada ya fedha kuingia katika akaunti zao, muda huo sasa umepita hivyo wanatakiwa kuondoka ili kupisha utekelezaji wa mradi,” amesema Mhandisi Kanyenye.

Amesema kuwa wamechelewa kuanza zoezi hilo kwa ajili ya kuwapa muda waathirika ili wapate muda wa kubomoa wenyewe kwa hiari ili kuokoa baadhi ya mali zao.

Amesema kwamba kati ya waathirika 2,329 waliopo kwenye orodha ya daftari la kwanza la ulipaji fidia, kufikia Machi 21, 2024, tayari waathirika 2,151 walikuwa wamelipwa kiasi cha shilingi bilioni 52.6.

“Lakini pia kuna wale ambao hawakufikiwa katika uthamini wa awali kwa baadhi yao kugomea ama kutoonekana katika maeneo yao, idadi yao ni 466, hawa wameingizwa katika orodha ya daftari la pili ambalo limeshakamilika na litawasilishwa kwa Mthamini Mkuu wa Serikali kwa ajili ya kusainiwa tayari kwa kulipwa fidia,” amesema .

Mradi unatekelezwa kwa muda wa miaka sita kuanzia mwaka 2022-2028 kwa gharama shilingi bilioni 663 na lengo kuu la mradi ni kuimarisha ustahimilivu kwa kuweka mikakati ya kukabiliana na mafuriko na kuwa na matumizi bora ya ardhi katika eneo la chini la bonde la mto Msimbazi ikiwa ni pamoja na kurudisha uoto wa asili katika uwanda wa juu wa bonde la mto Msimbazi.

By Jamhuri