SHARE

 *Dakar, Senegal* 

Mkutano wa Kimataifa wa Asasi ya Kimataifa ya Uwazi na Uwajibikaji _*(EITI – Extractive Industry Transparency Initiative)*_ uliofanyika Jijini Dakar nchini Senegal kuanzia tarehe 13 -14 Juni 2023 umejadili fursa mbalimbali kwenye Sekta ya Madini ikiwemo namna nchi zenye utajiri wa madini mkakati zinavyoweza kuzalisha madini hayo kwa kuzingatia vigezo vya Uwazi na Uwajibikaji ili kuhakikisha kuwa madini hayo yanawanufaisha wananchi wa maeneo yanapozalishwa na kuchangia katika kuinua uchumi wa mataifa husika.

Akichangia hoja katika mkutano huo, Naibu Waziri wa Madini Dkt. Steven Kiruswa alisema Tanzania ina aina nyingi za Madini mkakati yakiwemo *_Nikeli, Graphite (Kinywe), Rare Earth Elements, Cobalt, Lithium, Manganese, Vanadium, Niobium, Titanium, Tin, na Copper (Shaba)._* 

Aliongeza kuwa, madini hayo yanahitajika kwa wingi duniani kwa sasa na hivyo kinachohitajika zaidi ni ushirikiano (Partnerships) kati ya Serikali na wawekezaji mahiri kwenye masuala ya utafiti wa kina, uchimbaji wa kisasa, na uchakataji wa bidhaa za ndani na kuyaongeza thamani madini ndani ya nchi suala ambalo litaongeza tija na kutoa fursa za ajira kwa wazawa na kukuza biashara ya bidhaa za madini yaliyoongezwa thamani kwa walaji wa masoko ya ndani na nje ya nchi. 

Aidha, katika mkutano huo, mada mbalimbali zilijadiliwa kwa siku mbili ikiwa ni pamoja na masuala ya vipaumbele katika Uwajibikaji na Uwekaji wazi kumbukumbu za uzalishaji na biashara ya Rasilimali Madini, Mafuta na Gesi Asilia katika kipindi cha miaka kumi ijayo; uwekaji wazi Mikataba kati ya Serikali na wawekezaji; uwekaji wazi takwimu za wenye hisa katika kampuni za uwekezaji; sambamba na kujadili mbinu za kukabiliana na rushwa na ufisadi katika Sekta za Madini, mafuta na Gesi Asilia.

By Jamhuri