Na Zulfa Mfinanga,Jamhurimedia, Arusha

Agizo la Rais la kuzitaka Taasisi za serikali kufanya kazi kidigitali linaendelea kutekelezwa ambapo leo wadau wa serikali Mtandao (eGA) wamekutana jijini Arusha kwa kikao cha siku tatu cha kujadili matumizi ya TEHAMA serikalini.

Kikazi kazi hicho cha nne kina lengo la kufanya tathmini ya jitihada za serikali mtandao, changamoto zake pamoja na kupitia mapendekezo 12 yaliyotolewa kwenye kikao cha tatu za serikali mtandao kilichafanyika mwaka jana.

Akifungua kikao hicho, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, George Simbachawene amezitaka Taasisi zote za serikali kuingia kwenye mfumo wa mtandao kwa kuwa jambo hilo ni la lazima.

Amesema suala hilo lipo kisheria (Na. 10 ya mwaka 2019) huku akiipongeza idara ya mahakama kwa kufanya vizuri katika kutekeleza agizo hilo.

“Serikali mtandao imeendelea kurahisisha huduma kwa wananchi kwa haraka, sahihi na kwa wakati, ndiyo maana tunatazitaka Taasisi zote ziingie kwenye mfumo huo” alisema Waziri Simbachawene.

Amesema hadi sasa jumla ya taasisi 119 zimeshaunganishwa na mfumo huo huku Taasisi 117 zikiwa tayari zimeshasajiliwa.

Amesema kuna haja ya kuweka ushindani katika Taasisi zote za serikali kwenye utoaji wa huduma kimtandao ili kuleta uwajibikaji na ufanisi wa huduma.

Mkurugenzi Mkuu wa Serikali Mtandao Mhandisi Benedict Ndomba amesema lengo la kuanzishwa kwa sheria hiyo ni kuwa miradi na mifumo ya serikali inayozingatia sheria pamoja na utunzaji wa taarifa za serikali.

“Mfumo huu utaleta mageuzi ya kimtandao nchini lakini pia utasaidia kubadilishana taarifa serikali pamoja na kutunza taarifa za serikali” amesema Mhandisi Ndomba.

Mkutano huo wa siku tatu umewakutanisha wadau zaidi ya elfu moja wakiwemo Wakuu wa Taasisi, Maafisa TEHAMA, Wakurugenzi wa Mipango, Utawala, na Wakuu wa Vitengo vya Mawasiliano Serikalini.

By Jamhuri