WADUNGUAJI HATARI KUMI ‘Shetani’ Chris Kyle (8)

Katika mfululizo wa makala hizi za kuangalia wadunguaji, leo tutamzungumzia mtu mwingine ambaye naye alikuwa mwanajeshi. 

Moja ya madhila aliyokutana nayo ni yeye pia kulengwa na wadunguaji wengine wa upande wa maadui zao.

Alikuwa ni mwanajeshi katika jeshi la Marekani na ameua kwa kuwadungua watu 150. Ni idadi kubwa sana na ndiyo maana ameingizwa kwenye orodha ya wadunguaji hatari duniani akishika nafasi ya nane.

Huyu ni Chris Kyle, aliyezaliwa Texas Aprili 8, 1974 na kufariki dunia Februari 2, 2013.

Alipangiwa kikosi cha askari hatari cha Navy SEAL akiwa mdunguaji. Habari zake zilifahamika kwa watu wengi kutokana na kitabu cha maisha yake alichokiandika na kukizindua mwaka 2012. Baadaye mwaka 2015 ilitengenezwa filamu kuhusu maisha yake ikaongozwa na mwongozaji maarufu wa filamu duniani, Clint Eastwood.

Katika filamu hiyo nafasi ya Kyle ilichezwa na Bradley Cooper. 

Idadi kamili ya watu aliowaua Kyle kwa kuwadungua akiwa vitani nchini Iraq bado ina ubishani lakini kuna uhakika wa vifo 159 kutokana na kazi yake hiyo.

Yeye mwenyewe alishawahi kusema kuwa pamoja na watu hao 150, pia amewadungua watu wengine zaidi ya 100 katika kazi yake. 

Alipata sifa baada ya kuvunja rekodi ya mdunguaji mwingine wa Marekani, Waldron.

Alishatunukiwa nishani za aina mbalimbali kutokana na umahiri katika kazi yake.

Katika moja ya kazi zake, Kyle alimbatiza mtu aliyepangiwa kumuua kwa jina la “Al-Shaitan Ramadi,” likimaanisha Shetani Ramadi, jina ambalo alikuja kupachikwa yeye mwenyewe baadaye.

Pamoja na kuua maadui, lakini Kyle pia alipangiwa kazi za kuwalinda maofisa wa Marekani waliokuwa katika maeneo ya kivita.

Yeye mwenyewe alinusurika katika matukio kadhaa ya kuuawa kwani alikuwa analengwa na kutafutwa sana na maadui.

Umaarufu wake ulitokana pia na kumdungua mtu katika umbali wa yadi 2,100. Alimdungua mdunguaji mwingine wa adui ambaye alijificha akivizia kuwadungua maofisa wa jeshi la Marekani nje kidogo ya mji wa Sadr mwaka 2008. Kyle mwenyewe aliwahi kusema kuwa alimdungua mdunguaji huyo kwa bahati tu, kwani alikuwa mbali sana.

Baada ya kukamilisha kazi yake katika vita ya Iraq, amewahi kunusurika kuuawa kwa risasi mara mbili na alihusika katika mashambulizi ya mabomu ya kutegwa ardhini mara sita. Alistaafu jeshini mwaka 2009. 

Mwaka 2013, Kyle aliuawa akiwa na rafiki yake, Chad Littlefield, katika loji ya Rough Creek karibu na Mlima Chalk huko Texas. 

Mtu aliyewaua, Eddie Ray Routh, pia aliwahi kuwa mwanajeshi lakini akaja kubainika kuwa na matatizo ya akili yaliyotokana na msongo wa mawazo. Hata hivyo alihukumiwa kifungo cha maisha.