Wafanyabiashara Kinondoni walia miundombinu mibovu ya Masoko

Na Mussa Augustine,JamhuriMedia

Wafanyabishara wa Masoko ya Kigogo,Magomeni na Makumbusho katika Manispaa ya Kinondoni Mkoani Dar es salaam wameiomba Serikali kuwatatulia kero zinazowakabili ikiwemo uchakavu wa Miundombinu ya Maji taka,pamoja na huduma zingine Muhimu kama vile kukosa sehemu ya Kuhifadhi taka pamoja na Umeme .

Wakizungumza kwa nyakati tofauti baada ya Mwenyekiti wa Chama Cha Wafanyabiashara Wilaya ya Kinondoni Abdalah Mwakilima alipotembelea Masoko hayo nakuzungumza na Wafanyabiashara hao ambapo wamebainisha kwamba wanashindwa kufanya biashara vizuri kutokana na baadhi ya maeneo ya Masoko hayo kukosekana miundombinu rafiki pamoja na huduma zingine muhimu.

Baadhi ya wafanyabiashara katika soko la Magomeni ambao ni Mussa Kunambi mchuuzi wa Nyanya, mbogamboga ameomba waruhusiwe kufanyabiashara kwenye maeneo ya chini kutokana na kukosa wateja sababu ya kupangwa kufanya biashara gorofa ya juu hali inayopelekea kupata hasara na bidhaa zao kuoza ..

Kwa upande wake mfanyabiashara wa bidhaa za mitumba Abass Ramadhani amelalamika kwa kusema wanafanya biashara katika mazingira hatarishi kwani chemba za maji machafu zilizo wazi zikitiririsha maji yanayonuka na nyingine zikitoa uchafu unaotoka juu ya gorofa huku wakikumbana na wizi wa mali zao hasa nyakati za usiku kwani tangu wapangiwe eneo hilo ni takribani miezi mitatu wanafuatilia Halmashauri na kuishia kupigwa kalenda..

“Kiukweli tunafanya bishara ya mitumba katika mazingira magumu yakukosekana Kwa umeme,TANESCO wamewahi kuja hapa nakupima lakini hakuna majibu mpaka Sasa hatujaletewa umeme , hatuna amani na mali zetu zinaibiwa “amesema kwa uchungu Abbas Ramadhani

Kwa upande wap Wafanyabiashara wa Soko la Makumbusho Peragia Mushi, Yusuphu Omary wameukataa uongozi wa soko uliokuwepo Kwa madai mbalimbali ikiwemo wanaendeshwa kwa mabavu na vitisho atakayekwenda kushtaki anaambiwa simu polisi na wametapeliwa fedha kwa kudanganya wafunguliwe accounti za benki wapewe mikopo pia eneo la barabara vimejengwa vizimba na kuzuia magari kuingia na kutoka.

Hata hivyo kutokana na Uongozi uliopita kushindwa kutimiza wajibu wao ipasavyo hali iliyo mlazimu Mwenyekiti wa Chama Cha Wafanyabiashara Wilaya ya Kinondoni Abdalah Mwakilima kuteua viongozi wengine wa muda ambao watahudumu mpaka pale utakapoitishwa uchaguzi wa viongozi wa kudumu.

Hata hivyo Abdalah amewahakikishia Wafanyabiashara hao kuwa kero zote zinazowakumba atazifikisha sehemu husika ili kupatiwa ufumbuzi huku akiwataka kuendelea kuchapa kazi kwa bidii nakuunga mkono dhamira ya Rais Dkt Samia ambaye anataka Wafanyabiashara wadogo wafanye biashara katika mazingira mazuri nakukuza biashara zao.

Abdalah amesema kwamba ataendelea kufika kwenye masoko hayo mara kwa mara ili kuhakikisha kero zinazowakumba Wafanyabiashara hao zinaondolewa nakuwafanya wafurahie kufanya biashara zao katika mazingira safi na salama.

“Ndugu zangu Mheshimiwa Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni Godwin Gondwe pamoja na Mkurugenzi wa Halmashauri yetu wanafahamu kwamba tuna kikao hapa ,hivyo naomba mnieleze kero zinazowakumba ili niwapelekee waweze kuzitafutia ufumbuzi,nawaomba sana tushirikiane na viongozi wetu ” amesema Adhalah mbele ya kikao na Wafanyabiashara hao.