Ufisadi wa fedha za kilimo cha miwa na kiwanda cha sukari vilivyobuniwa na Mkuu wa Wilaya ya Tarime, Glorious Luoga, ndio uliomfanya Rais John Magufuli, amng’oe kwenye nafasi hiyo, JAMHURI limebaini.

Mradi huo ulibuniwa na Luoga kwa kigezo cha kuongeza kipato cha wananchi wa wilaya hiyo wasiokuwa na zao la biashara, kwani bila mradi wa kuwaingizia pato wanalazimika kulima na kuuza bangi.

Mradi ulihitaji ardhi ya kilimo na ujenzi wa kiwanda cha kusindika sukari. Vijiji vilivyohusishwa ni Bisarwi, Weigita, Mrito, Keisaka, Surubu, Kembwi, Nkerege, Nyamirambaro na Matongo; lakini vijiji pekee vilivyotoa ardhi ni vya Weigita, Bisarwi na Keisaka.

Hata hivyo, Rais Magufuli aliupiga “stop” mradi huo wakati alipokuwa kwenye ziara mkoani Mara mwishoni mwa mwaka jana. Alitaja sababu moja ya kuzuia mradi huo kuwa ni kukosekana kwa uthibitisho wa ardhi kwa matumizi ya wananchi endapo kiasi hicho angepewa mwekezaji wa kilimo cha miwa.

Kutokana na utata huo, Katibu Mkuu wa Wizara ya Madini, Profesa Simon Msanjila, mwishoni kwa mwaka jana aliunda timu ya watu sita kuchunguza matumizi ya fedha za mradi huo ambazo zimetoka kwenye Mfuko wa North Mara Community Trust.

Wajumbe wa kamati walitoka Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU), Ofisi ya Rais, Tume ya Madini na Wizara ya Madini.

Matokeo ya uchunguzi ambayo JAMHURI limeyapata kutoka Tarime yanaonyesha uhusika wa ofisi ya Mkuu wa Wilaya, iliyokuwa inaongozwa na Luoga kwenye upotevu wa mamilioni ya shilingi kwenye mradi huo.

Luoga aliwasilisha ombi la kupatiwa ufadhili wa vifaa na wataalamu wa upimaji kutoka mgodi wa North Mara Gold Mine Ltd na fedha kutoka Mfuko wa Maendeleo wa North Mara Community Trust Fund ili kutekeleza mradi huo.

Mfuko ulitoa Sh milioni 214 kwa masharti ya kupatiwa ardhi ya ukubwa wa hekta 840 ndani ya eneo la mradi kwa ajili ya kilimo cha miwa na kujenga nyumba za kupangisha wafanyakazi wa mradi.

“Mkuu wa Wilaya alikubaliana na sharti hilo na kuahidi kuwapatia ardhi hiyo. Pia aliahidi kuongea na mwekezaji ili atoe sehemu ya faida yake kuufadhili Mfuko. Mgodi ulitoa vifaa na wataalamu kwa siku 30 kufanikisha upimaji wa ardhi kwa gharama zake,” inasema ripoti.

Aprili 13, 2017 fedha zilihamishwa kutoka kwenye Mfuko kwenda wilayani. Kiasi kilichohamishwa ni dola 99,000 za Marekani ambazo kwa wakati huo zilikuwa sawa na Sh milioni 220.572. Zilitolewa kwenye Akaunti ya Mfuko Na. 30410003847 iliyoko katika Benki ya NMB kwenda akaunti ya Kampuni Tanzu ya biashara ya North Mara Commercial Business yenye akaunti Na. 33010002843 ambayo pia iko kwenye benki hiyo hiyo.

Aprili 20, 2017, Sh milioni 214 zilihamishwa kutoka akunti ya Kampuni Tanzu kwenda akaunti ya DAS Tarime Imprest Account Na. 30410008369 iliyoko katika Benki ya NMB.

JAMHURI limeelezwa kuwa uhamisho wa fedha hizo ulikuwa ni utekelezaji wa maazimio ya kikao cha Bodi ya Wadhamini wa Mfuko cha Machi 29, mwaka huo.

Fedha zilivyotafunwa

Matumizi ya fedha hizo yalifanywa na Ofisi ya Mkuu wa Wilaya chini ya usimamizi wa Katibu Tawala wa Wilaya (DAS) ya Tarime, John Mahinya Marwa. Hadi Oktoba, mwaka jana Sh milioni 213.61 zilikuwa zimekwishatumika kwa nyakati tofauti.

Mchanganuo wa matumizi hayo unaonyesha kuwa; mosi, Aprili 21, 2017 Sh milioni 32 ziliidhinishwa kwa ajili ya kulipia gharama za usafiri na posho za kujikimu kwa viongozi na watendaji wa serikali wilayani Tarime kwenda Dodoma na Dar es Salaam kuonana na Waziri wa Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI).

Pili, Aprili 24, 2017 Sh milioni 100 ziliidhinishwa kwa ajili ya kukodisha vifaa vya upimaji na wataalamu wa kutumia vifaa hivyo.

Tatu, Aprili 29, 2017 Sh milioni 42.5 ziliidhinishwa kwa ajili ya kulipa posho kwa wataalamu, watendaji wa vijiji na vibarua.

Nne, Mei 2, 2017 Sh milioni 2.11 ziliidhinishwa kwa ajili ya kununulia mafuta kwa magari yaliyokuwa yakitumika kwenye kazi ya upimaji.

Tano, Mei 12, 2017 Sh milioni 20 ziliidhinishwa kwa ajili ya kulipa posho kwa wataalamu; na mwisho, Mei 23, 2017 Sh milioni 17 ziliidhinishwa kwa ajili ya kulipa posho za wataalamu. Sh 390,000 ndizo pekee zilizokuwa zimesalia kwenye akaunti ya DAS Tarime Imprest hadi Oktoba, mwaka jana.

Taarifa ya uchunguzi imebaini kuwa matumizi ya vifaa na wataalamu wa upimaji, mgodi wa North Mara ulitoa bure vifaa vyote na wataalamu wa upimaji kwa siku 30 kuanzia Aprili 28 hadi Mei 28, 2017. Pia posho zote za wataalamu waliotoka mgodini zililipwa na mgodi.

Ripoti ya uchunguzi inaonyesha kuwa Katibu Tawala wa Wilaya ya Tarime, John Mahinya Marwa, alikuwa akiidhinisha matumizi ya fedha zaidi ya kiwango cha Sh milioni 2 alichoidhinishiwa na Afisa Masuhuli ambaye ni Katibu Tawala wa Mkoa wa Mara.

Katika orodha za malipo ya wataalamu, baadhi ya malipo yameonekana kutosainiwa na wahusika na badala yake baadhi ya wataalamu kusaini kwa niaba bila kuwapo uthibitisho wa kuomba kuchukuliwa fedha au fedha hizo kuwasilishwa kwa mhusika.

Sh milioni 4.5 zililipwa kwa wataalamu wa mwekezaji kutoka Uganda wakati mwekezaji huyo alikuwa na wajibu wa kuwalipa watu wake na hakuna uthibitisho wa wao kukiri kupokea fedha hizo.

Wilaya ilitumia Sh milioni 32 kugharimia posho za viongozi wa kiserikali na kisiasa (Mkuu wa Wilaya ya Tarime, Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Tarime, madiwani, viongozi wa vijiji na watumishi wa halmashauri) ambao walisafiri kwenda Dodoma na Dar es Salaam kufuatilia suala la kilimo cha miwa na ujenzi wa kiwanda cha sukari kati ya Aprili 23 – 30, 2017 na Mei 11 – 22, mwaka huo. Ripoti inasema matumizi haya yalikuwa kinyume cha makubaliano ya maombi ya fedha kutoka kwenye Mfuko.

Mnamo Aprili 24, 2017 Katibu Tawala wa Wilaya ya Tarime aliidhinisha Sh milioni 100 ambazo zilikabidhiwa taslimu kwa Baraba Albert ili akakodishe vifaa vya kupimia.

“Uidhinishaji huo uliofanywa na Katibu Tawala wa Wilaya ya Tarime, John Mahinya Marwa, ulikuwa kinyume cha taratibu za fedha za umma na taratibu za ununuzi wa umma. Hata hivyo, hadi wakati wa uchunguzi huu hapakuwa na uthibitisho wowote uliowasilishwa kuonyesha vifaa hivyo vilikodishwa.

“Imethibitika kuwa vifaa vilivyotumika kwenye upimaji pamoja na wataalamu wake vilitolewa na mgodi [North Mara] bila malipo. Kutokana na ushahidi uliopatikana uchunguzi unaamini kuwa fedha hizo zimefujwa. Ushahidi umethibitisha kuwa kuanzia Aprili 25, 2017 hadi Mei 02, 2017 Baraba Albert alikuwa na ruhusa ya kwenda kwenye matibabu katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili.

“Mafuta ya Sh milioni 2.11 yaliyonunuliwa kwa matumizi ya upimaji hayakuingizwa kwenye leja za stoo ili kudhibiti matumizi yake kama utaratibu unavyoelekeza.

“Sh milioni 7.89 za malipo ya Aprili 21, 2017 zilizopokewa na Joseph Mulazi hazina uthibitisho wowote wa kupokewa na walengwa. Baraba Albert ambaye ni miongoni mwa watu ambao fedha zao zilichukuliwa kwa niaba (Sh 1,000,000) alikuwa na ruhusa ya matibabu ya siku saba kuanzia Aprili 25, 2017 [hivyo kuna kila dalili kuwa Baraba Albert jina lake lilitumiwa bila yeye kukabidhiwa hizi fedha] na wataalamu walilipwa na mgodi na;

“Sh 1,000,000 zililipwa kwa Rhoida Nyondo kama malipo ya posho ya siku 10 kwa ajili ya upimaji ulioanzia Mei 11, 2017 na kwa wakati huo huo akiwa amelipwa posho ya kujikimu ya Sh milioni 1.32 kwa ajili ya safari ya kwenda Dodoma kuanzia Mei 11 – 22, 2017,” inasema taarifa na kuongeza kuwa Sh milioni 79.5 zililipwa kama posho kwa wataalamu, viongozi wa halmashauri, vibarua na wasaidizi. Malipo yaliyothibitika kuwa halali Sh milioni 35.42 na hivyo kufanya malipo yasiyo halali kufikia Sh milioni 44.08.

Kiasi kingine cha Sh milioni 4 kililipwa kwa wataalamu kutoka mgodini, ingawa wataalamu hao walikanusha kulipwa fedha hizo kwani walilipwa na mwajiri wao.

Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Tarime wa wakati huo, Luoga, alilipwa Sh milioni 2 kama posho ya kujikimu katika malipo ya Mei 12, 2017 kwa ajili ya kazi ya upimaji, ilhali hakuwahi kufika eneo la upimaji wa ardhi wakati wa upimaji.

Ripoti hiyo imebaini pia Luoga alilipwa tena posho ya kujikimu ya Sh milioni 1.32 kwa ajili ya safari ya kwenda Dodoma kuanzia Mei 11 – 22, 2017.

“Mkuu wa Wilaya ya Tarime na Katibu Tawala wa Wilaya ya Tarime hawakusimamia ipasavyo matumizi ya Sh milioni 214 na kusababisha matumizi mabaya ya fedha hizo.

“Katibu Tawala wa Wilaya ya Tarime [John Mahinya Marwa] alilipwa posho ya kujikimu Sh 1,440,000 kama posho ya kujikimu ilhali hakuwahi kufika kwenye eneo la upimaji; na

“Kiasi cha Sh 1,000,000.00 kililipwa kwa Abas Shemzigwa kama posho ilhali hakuwahi kufika eneo la upimaji na yeye alihusika kwenye kufanya malipo tu. Kwa hiyo, kati ya Sh milioni 214 zilizotolewa na Mfuko; Sh milioni 144.080 zilitumika isivyo halali,” inasema taarifa hiyo.

Kamati maalumu ya uchunguzi imependekeza mambo kadhaa. Miongoni mwa mambo hayo ni ukaguzi katika miradi yote iliyotekelezwa katika vijiji vyote vinavyozunguka Mgodi wa North Mara ili kuhakiki thamani halisi ya fedha na kubaini miradi iliyotekelezwa na mgodi huo kwa kutumia fedha za mrabaha wa asilimia moja za vijiji.

Imependekezwa uendeshaji wa Mfuko ufanyiwe mabadililiko kwa kubadili uongozi.

Watumishi wote waliohusika kufanya ufujaji na ubadhirifu wa fedha za umma (Sh milioni 214) wachukuliwe hatua za kisheria; pia wote waliohusika kufanya ufujaji na ubadhirifu wa fedha za Mfuko wachukuliwe hatua za kisheria.

 Katibu Tawala wa Wilaya ya Tarime, John Marwa, ameulizwa na JAMHURI kuhusu malipo hayo yanayodaiwa kufanywa kinyume cha taratibu, lakini amekataa kutoa ufafanuzi akisema hawezi kuzungumza.

“Siwezi kusema chochote, siwezi kusema chochote kuhusu hilo. Sasa hivi siwezi kuzungumza lolote. Kwani ripoti imenitaja nimekula hizo pesa au nimefanyaje?” amehoji.

Hata baada ya kuambiwa kuwa malipo aliyofanya yanadaiwa kutofuata sheria na taratibu, akahoji: “Utaratibu upi? Hiyo tungumze kesho, sasa hivi siwezi.”

Wakati anazungumza na JAMHURI tulikuwa tunakwenda mitamboni baada ya kumtafuta kwa muda mrefu bila mafanikio. Hata hivyo, gazeti hili litaendelea kumtafuta ili kupata ufafanuzi wake.

Please follow and like us:
Pin Share