Wafungwa wanavyoteswa Shinyanga

Na Mwandishi Wetu, Shinyanga

Vitendo vya ukiukwaji wa haki za binadamu katika magereza nchini vinaendelea licha ya Tanzania kuwa miongoni mwa mataifa mbalimbali duniani yaliyokubaliana kukomesha vitendo hivyo.

Mbali na matamko ya kisera ambayo Tanzania imeridhia kwenye ngazi ya kikanda na kimataifa juu ya kuheshimu haki za binadamu, Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzani ya mwaka 1977 Ibara ya 12-24 pia inasema wazi kuwa kila mtu  anastahili heshima ya kutambuliwa na kuthaminiwa utu wake ikiwa ni pamoja na kulindwa na kupata haki mbele ya sheria.

Kupitia Ibara hiyo ya Katiba, ilianzishwa Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora kwa Ibara ya  29 kipengele cha 1 kama ilivyofanyiwa marekebisho kwa sheria Namba 3 ya mwaka 2000 kwa lengo la kuendeleza na kulinda haki zote za binadamu, ili kuhakikisha kunakuwepo na demokrasia , utawala wa sheria na utawala bora.

Pamoja na kuwepo kwa sheria hizo lakini wafungwa na mahabusu katika magereza nchini Tanzania wanakabiliwa na changamoto mbalimbali ambazo zinakwenda kinyume na haki za binadamu.

Katika gereza la Mkoa wa Shinyanga kuna viashiria vingi vya ukiukwaji wa haki za binadamu licha ya kuwa sera, sheria na matamko mbalimbali ya ndani na nje ya nchi yameeleza wazi juu ya kulindwa na kuheshimiwa kwa haki za wafungwa.

Uchunguzi wa gazeti la JAMHURI, umebaini kwamba wafungwa katika gereza hilo wanaishi katika mazingira yasiyo salama kwa afya zao. Gereza lina idadi ndogo ya matundu ya vyoo ikilinganishwa na idadi ya wafungwa waliopo na vifaa vya usafi. Aidha, vyombo vya chakula siyo salama wakati huduma ya afya ni duni hali inayofanya wafungwa waishi maisha ya taabu na dhiki.

Kumrekebisha mfungwa tabia na hatimaye aweze kurudi katika tabia njema inayokubalika katika jamii ni moja ya kazi ya magereza wala sio sehemu ya kumpotezea heshima na utu wake kama anavyosimulia Abdi Ali (sio jina lake halisi) aliye tumikia adhabu ya kifungo cha miezi sita iliyopita gerezani.

“Ukiingia hapa ujue ukitoka lazima utoke na maradhi ya ngozi, kwa sababu usafi ni duni sana, mazingira ya kulala, kuoga na haja kubwa si salama, bafu la kuogea ndio hapo hapo sehemu ya haja ndogo, ndio hapo hapo pa kupigia mswaki na sisi tupo mamia ya watu,” amesema Ali.

Katika mkutano wa Umoja wa Mataifa juu ya haki za binadamu ujulikano kama Universal Declaration of Human Rights wa mwaka 1948 ambao Tanzania ilishiriki, lilipitishwa azimio la kulinda na kuheshimu haki za binadamu kwamba; kila mtu ana haki ya kuishi na kupatiwa huduma zinazostahiki ikiwemo chakula bora, mavazi safi, malazi bora huduma bora ya matibabu pamoja huduma za kijamii zinazostahili.

Uchunguzi wa JAMHURI, katika gereza la Mkoa wa Shinyanga, umebaini suala la malazi ambalo pia ni changamoto katika magereza nchini ambapo godoro moja hutumiwa na watu wanne hali inayowafanya kulala kwa kubanana kupita kiasi, kama anavyoeleza Yono Makoye aliyewahi kukaa mahabusu katika gereza hilo.

“Kule godoro moja wanalala watu wanne, yaani ukilala upande mmoja hakuna kujigeuza upande wa pili hadi pakuche, ni shida sana wakati wa kulala, ukiitwa mfungwa huna namna unakubali yote” amesema Makoye.

Tanzania imeshiriki pia mkutano wa kimataifa ujulikanao kama UN Standards Minimum Rule uliokuwa na lengo la kuhakikisha kuwa wafungwa wanapata haki za kibinadamu ikiwemo huduma zote za kijamii kwa kiwango kinachoridhisha, ikiwemo hakiya kuabudu pamoja na haki ya kuwasiliana.

Kama hiyo haitoshi, sheria ya magereza ya mwaka 1967 sehemu ya 76 iko bayana kuhusu haki za wafungwa kupatiwa mavazi stahiki, kulala kila mmoja peke yake, pamoja na kupatiwa matibabu bora kama itakavyoamriwa na daktari wa gereza.

Kupata uhalisia wa haya yote katika uchunguzi wa JAMHURI, ulilazimu baadhi ya familia za wafungwa kutafutwa wazungumze ili kujua iwapo wamepokea malalamiko yoyote kutoka kwa ndugu zao. Wapo waliokiri kweli kwamba hali sio nzuri kiasi cha kuwalazimu ndugu kuwapelekea baadhi ya mahitaji ambayo walistahili kupatiwa gerezani; ikiwemo chakula, sabuni, mafuta ya kupaka, dawa ya meno, nyembe pamoja na blanketi.

Mmoja wa ndugu ambaye hadi sasa tayari ameshatumikia miezi minne ya kifungo cha miaka 30 gerezani amesema licha ya kuwa suala la chakula ni jukumu la magereza, lakini analazimika kumpelekea nduguye chakula kila mwisho wa wiki kwani chakula gerezani sio kizuri.

“Kila nikija lazima nimpikie chakula nimletee, kama sikupika basi naleta dagaa wabichi anakuwa anatengenezewa na wapishi maana anadai chakula sio kizuri kabisa, na ninashukuru kwa sababu wanaruhusu tulete chakula au mboga ili apikiwe” amesema ndugu huyo na kuongeza.

“Lakini pia hata baadhi ya vifaa kama mablanketi kwa ajili ya kujikinga na baridi usiku, nyembe, sabuni, mafuta ya kupaka, dawa ya meno na vitu kama hivyo huwa naleta maana ya hapa anadai hakuna”

(Emis Kisena sio jina lake halisi) amesema alipatwa na mshtuko mara alipotembelea gerezani na kumwona mwanaye akiwa ametokwa na upele na ukurutu mwili mzima, ambapo alimwuliza kulikoni, akajibu chanzo ni mazingira machafu na ukosefu wa vifaa vya usafi kama vile sabuni.

“Ikifika siku ya kwenda kumuona mwanangu lazima nihakikishe kuwa sikosi mahitaji muhimu kama sabuni, kabla ya mwanangu kufungwa nilijua ndugu wanaenda magereza kusalimia ndugu zao kumbe wanakwenda kwa sababu nyingi, usipompelekea atakavyokuagiza ujue hakuna wa kumpatia,” amesema mama huyo

Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga ambaye pia ni Mwenyekiti wa Kamati ya Ulinzi na Usalama, Zainab Telack alipotakiwa kuthibitisha iwapo anafahamu juu ya changamoto hizo na maoni yake, aliomba apewe muda ili aweze kujiandaa kwa ajili ya kujibu hoja hizo. Hata hivyo hadi uchunguzi huu unatoka hapakuwa na majibu yoyote kutoka kwa kiongozi huyo.

Mtandao wa Utetezi wa Haki za Binadamu Tanzania kupitia Mratibu wake wa Kitaifa, Onesmo Ole Ngurumwa umezungumzia hali ya wafungwa gerezani na kukiri hali ya wafungwa na mahabusu katika magereza nchini sio ya kuridhisha.

Ole Ngurumwa ameliambia JAMHURI kwa mujibu wa viwango vya kimataifa gereza halipaswi kuwa sehemu ya kutweza utu wa binadamu, bali mfungwa na mahabusu wakiwa gerezani wanawajibika kwa kukosa haki moja tu ambayo ni uhuru wa kutembea.

Kiongozi huyo amesema, kwa kushirikiana na washirika wake kama vile Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu, Tume ya Haki za Binadamu pamoja na Chama cha Wanasheria Tanganyika, mtandao huo umekuwa ukiwatembelea wafungwa katika magereza mbalimbali nchini  na kutoa mapendekezo yao kuhusu nini kifanyike ili kuboresha maisha ya wafungwa; kama vile upanuzi wa majengo:

“Magereza yanapaswa kuwa si sehemu ya kutweza utu wa binadamu, mtu anapofungwa anakuwa amekosa haki yake moja tu ya kutembea au kujumuika na familia, lakini haki zake nyingine kama kula vizuri,kulala vizuri, kusoma magazeti, kuabudu ni lazima apate” amesema Olengurumwa na kuogeza kuwa

“Mazingira yanapokuwa mabaya ni kwenda kinyume na sheria zetu, kwenda kinyume na Katiba pamoja na makubaliano ya kimataifa, sisi  pamoja na wanachama wetu huwa tunatembelea magereza zetu na kutoa mapendekezo ya nini kifanyike ili kuboresha mazingira hayo”

Uduni wa hali ya wafungwa na mahabusu nchini umetiliwa mkazo zaidi bungeni wakati wa uwasilishaji maoni ya kambi rasmi ya upinzani ya makadirio ya mapato na matumizi kwa mwaka wa fedha 2017/2018 kwa Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi; ambapo msemaji wake, Mbunge wa Arusha Mjini, Godbless Lema amesema hali ni mbaya.

Akichambua taarifa ya utekelezaji wa majukumu ya Wizara kwa mwaka wa fedha 2016/2017 na mwelekeo wa bajeti kwa mwaka wa fedha 2017/2018, Mheshimiwa Lema alisema kuwa bajeti yote ya fedha za maendelo kwa ajili ya jeshi la magereza iliidhinishiwa Shilingi Bilioni 3  lakini fedha zilizotolewa ni Sh milioni 190, jambo linaonesha kuwa ufinyu wa bajeti ni moja ya sababu inayochangia changamoto lukuki  katika magereza nchini.

Wizara ya Mambo ya Ndani kwa kipindi cha mwaka wa fedha 2017/2018 iliidhinishiwa jumla ya Sh bilioni 930, lakini ni shilingi bilioni 3 tu zilitengwa kwa ajili ya upanuzi na ujenzi wa magereza mpya kila wilaya ili kuhakikisha haki za binadamu zinatekelezwa.

Katibu Mtendaji wa Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora, Mary Massay, licha ya kukiri kuwa hajafika katika magereza ya Shinyanga lakini amekanusha vikali kuwepo kwa ukiukwaji wa haki za wafungwa na mahabusu katika gereza hilo na kuongeza kuwa hata ripoti yao (ambayo hakuifafanua inahusu nini na ni ya mwaka gani) amesema inafurahisha.

“Mi naomba usome ripoti yetu itakusaidia kujibu maswali yote hayo, hayo unayosema havipo kabisa, hii ripoti ukiisoma utafurahia, nimetembelea baadhi ya magereza bahati mbaya huko Shinyanga sijafika, lakini hakuna huo ukiukwaji wa haki za binadamu unaousema” amesema Massay.

Kamishna wa magereza nchini Dk Juma Malewa amekanusha kuwepo vitendo vya ukiukwaji wa haki za binadamu katika magereza yote nchini huku akikiri kuwepo kwa msongamano ambao alisema ni suala mtambuka kwa kuwa unahusisha taasisi mbalimbali.

Ripoti ya Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu ya kuanzia mwezi Januari hadi June mwaka 2017 imeonesha hali ya haki za binadamu Tanzania ni mbaya katika nyanja mbalimbali ikilinganishwa na kipindi kama hicho mwaka 2016.