Na Mwandishi Wetu,JamhuriMedia, Tabora

Katika kuhakikisha mauaji ya watu wenye ualbino, watoto wachanga na vikongwe yanakomeshwa, Chama cha Waganga wa Tiba Asilia Mkoani hapa kimeazimia kuwasaka wenzao wanaopiga ramli chonganishi na kuomba kupelekewa viungo vya binadamu ili wawatengenezee dawa.

Ili kufanikisha mkakati huo chama hicho kimeamua kuungana na Jeshi la Polisi ili kuhakikisha wale wote watakaobainika au kutajwa kuhusika na vitendo hivyo wakamatwe mara moja na kufikishwa kwenye vyombo vya sheria.

Kauli hiyo imetolewa kwenye kikao kilichokutanisha Viongozi wa Chama cha Waganga wa Tiba asilia Mkoani hapa na viongozi wa Jeshi la Polisi.

Akizungumza katika kikao hicho Makamu Mwenyekiti wa Umoja huo Moshi Kisamvu amesema wamekuja na mkakati wa pamoja na Jeshi la Polisi ili kuhakikisha mauaji yoyote yanayotokana na ramli chonganishi yanakomeshwa.

Ametaja baadhi ya mikakati hiyo kuwa ni kuwasaka popote walipo waganga wote wanaolalamikiwa kujihusisha na vitendo hivyo, kufanya upelelezi wa kina dhidi yao ikiwemo kubaini makazi yao, atakayebainika kuhusika atachukuliwa hatua za kisheria.

Ameomba jamii kutoa taarifa za siri dhidi ya waganga wote wanaofanya vitendo hivyo na kuharibu sifa ya Waganga wa tibaasilia ambao wamekuwepo tangu enzi za mababu, kabla na baada ya Uhuru wakati huo kukiwa hakuna Hospitali.

Akizungumza katika kikao hicho Kamanda wa Polisi Mkoa hapa Richard Abwao amewataka Waganga wa tiba Asilia kuwakemea wenzao wanaochafua sifa ya chama hicho kwa kudanganya wananchi kuwa viungo vya binadamu vitawasaidia.

Kamanda amesema yeye anaamini tiba asilia wanazofanya zinahitaji vitu vingine lakini ila siyo miili ya binadamu.

Katibu wa Mkoa wa Umoja huo Jumanne Mpanda amesema kuanzia sasa waganga wote kabla hawajapata leseni za kutoa huduma hiyo wanapaswa kuthibitishwa na umoja huo ili wasajiliwe na chama hicho.

Ameongeza kuwa kutakuwa na semina ya waganga wote hivi karibuni ili waweze kuelekezwa utaratibu wa kuendesha shughuli zao kwa ufanisi zaidi bila ya kuvunja sheria za nchi.

Awali Mtemi wa Waganga wa Mkoa wa Tabora Habibu Ndutu amesema baadhi ya watu wanaojihusisha na shughuli hiyo sio waganga na hata ofisi zao hazijulikani zilipo, hivyo wakitambuliwa na umoja huo na kusajiliwa itakuwa rahisi kuwabaini.

Amesisitiza kuwa wamekuwa wakitoa maneno mazuri kwa wateja wao ili waaminiwe na kujipatia fedha za ulaghai, hili halikubaliki

By Jamhuri