Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia,Dodoma
Wagombea 58 kutoka vyama 17 vya siasa vyenye usajili kamili wameteuliwa na Tume ya Taifa ya Uchaguzi kuwania nafasi wazi ya Ubunge kwenye Jimbo la Mbarali lililopo Halmashauri ya Wilaya ya Mbarali na kata sita za Tazanzania Bara.
Tarehe 05 Agosti, 2023 Tume ilitangaza uchaguzi mdogo wa Jimbo la Mbarali na kata sita za Tanzania Bara na uteuzi wa wagombea umefanyika tarehe 19 Agosti, 2023, kampeni zimeanza tarehe 20 Agosti 2023 na zinatarajiwa kuhitimishwa tarehe 18 Septemba, 2023 ambapo uchaguzi utafanyika tarehe 19 Septemba, 2023.
Fomu za uteuzi wa wagombea zilitolewa kuanzia tarehe 13 hadi 19 Agosti, 2023 ambapo jumla ya wagombea 70 walichukua fomu.
Kati ya wagombea 70 waliochukua fomu, wanawake walikuwa 21 na wanaume walikuwa 49. Kati ya wagombea 58 walioteuliwa wanawake ni 14 na wanaume ni 44.
Wagombea hao wametoka kwenye vyama 17 ambavyo ni; CCM, AAFP, ACT – WAZALENDO, TLP, NRA, SAU, ADA – TADEA, ADC, CCK, CUF, DEMOKRASIA MAKINI, DP, NCCR – MAGEUZI, NLD, UDP, UMD na UPDP.
Kata zitakazofanya uchaguzi mdogo ni; Nala iliyopo Halmashauri ya Jiji la Dodoma, mkoani Dodoma, Mwaniko iliyopo Halmashauri ya Wilaya ya Misungwi, mkoani Mwanza, Old Moshi Magharibi iliyopo Halmashauri ya Wilaya ya Moshi na Marangu Kitowo iliyopo Halmashauri ya Wilaya ya Rombo, mkoani Kilimanjaro, Mtyangimbole iliyopo Halmashauri ya Wilaya ya Madaba na Mfaranyaki iliyopo Halmashauri ya Manispaa ya Songea, mkoani Ruvuma.