Hali si shwari ndani ya Chuo Kikuu cha Teofilo Kisanji (TEKU), baada ya uongozi wa Chama cha Wahadhiri wa Chuo hicho (TEKUASA) na wanachama wake kutangaza mgomo wa kutotunga mitihani ya kufunga mhula, inayotarajiwa kufanyika Julai mosi, waka huu.

Wametaja sababu za mgomo huo kuwa ni kero ya menejimenti ya chuo kutowapa majibu ya matatizo yao.

 

Mgomo huo umetangazwa na Kaimu Mwenyekiti wa TEKUASA, Amani Simbeye, katika mkutano na waandishi wa habari kwenye ukumbi wa chuo na kuhudhuriwa na zaidi ya wahadhiri 30, wiki iliyopita.

 

Simbeye amesema kuna changamoto nyingi za elimu inayotolewa chuoni hapo ambazo menejimenti inahusika moja kwa moja, hivyo kuhatarisha mustakabali wa elimu nchini, hususan inayotolewa chuoni hapo na kuongeza kuwa hakuna ushirikishwaji wa uamuzi unaohusu taaluma.

 

Ametaja baadhi ya sababu za kugoma kutunga mitihani ya kufunga muhula hadi pale zitakapopatiwa ufumbuzi kuwa ni pamoja na uongozi wa chuo hicho kutowashirikisha wahadhiri katika kushughulikia taaluma inayotolewa chuoni hapo.

 

Amesema menejimenti hiyo ilijadili na kubadili muda wa masomo bila wahadhiri kuhusishwa, ambapo wamebadilisha kutoka somo moja kufundishwa kwa miezi minne hadi kufundishwa kwa wiki mbili, hali waliyodai kuwa walimu watashindwa kukamilisha mada inavyotakiwa pamoja na kuandaa mitihani ya mwisho ya kuwapima wanafunzi.

 

Pia amesema menejimenti bila kuwashirikisha wahadhiri ilifanya uamuzi wa kuwafukuza chuo wanafunzi wa madhehebu ya Wasabato baada ya kushindwa kufanya mitihani wiki iliyopita, hivyo kukiuka sheria za Vyuo Vikuu na Elimu ya Juu.

 

Changamoto nyingine ni pamoja na menejimenti kuwafukuza chuo baadhi ya wanafunzi, ambao walikamatwa kwa kosa la kughushi hati za malipo ya ada benki lakini baadaye walirudishwa bila wakufunzi kupewa taarifa.

 

Kaimu Mwenyekiti huyo ameongeza kuwa menejimenti iliwafukuza wahadhiri watatu kwa madai kuwa walishiriki kuwahamasisha wanafunzi kufanya mgomo na kufuatilia kesi dhidi ya menejimenti, lakini wakashindwa kutoa vielelezo kuhusu madai hayo wanayowatuhumu wakufunzi waliowafukuza.

 

Ameongeza kuwa kutokana na Sheria za Vyuo Vikuu, mhadhiri anapandishwa daraja kutokana na  kusoma zaidi au kwa kufanya machapisho, lakini sheria hiyo imekiukwa baada ya menejimenti ya TEKU kushindwa kuwapandisha madaraja baadhi ya wahadhiri na wengine kushushwa bila kuwapo kwa taarifa za msingi.

 

Amesema pia menejimenti hiyo inasitisha mishahara ya watumishi na wengine wakicheleweshewa bila sababu zozote, ambapo pia uwepo wa wahadhiri ambao taaluma yao zina mashaka na kutokuwa na uwezo wa kufundisha baadhi ya masomo lakini wao wamewapa hadi vitengo.

 

Aidha, ameongeza kuwa utaratibu wa vyuo vikuu kila idara inatakiwa kuwa na mkuu wa idara husika, lakini kwa TEKU hali ni tofauti kutokana na kuwapo kwa idara bila kuwapo kwa wasimamizi kama kitengo cha kusimamia ubora wa elimu inayotolewa chuoni hapo.

 

Kutokana na madai hayo, wahadhiri hao kwa sauti moja walikubaliana kutotunga mitihani hiyo ya kufunga mhula hadi hapo menejimenti itakapotoa majibu juu ya changamoto hizo na namna ya kuzitatua likiwamo suala la ushirikishwaji katika uamuzi.

 

Mhadhiri Rose Sekile amesema wamekubaliana kufanya hivyo kutokana na menejimenti kuwavunja ari ya ufundishaji na kusababisha elimu kuendelea kudorora licha ya wao kuiandikia barua menejimenti pamoja na Bodi ya Chuo kuhusiana na malalamiko yao, ambayo hayajajibiwa na kuhusu kutokuwa na imani na baadhi ya wajumbe wa bodi.

 

Hata hivyo, Kaimu Makamu Mkuu wa Chuo, Dk. Daniel Mosses, alipotakiwa kuzungumzia kuwapo kwa mgogoro huo chuoni hapo, alisema yeye si msemaji wa chuo na anayetakiwa kuongelea hayo ni Makamu Mkuu wa Chuo ambaye yuko safarini.

 

Alipobanwa zaidi alisema atayafanyia uchunguzi madai ya wahadhiri na kuyafikisha kwa Makamu Mkuu wa Chuo aweze kuyaongelea. Hata hivyo, Kaimu Makamu Mkuu wa Chuo, Dk. Mosses, ameibuka na  kukanusha mgomo huo.

 

Akisoma tamko la kukanusha uwepo wa mgomo huo, Dk. Mosses amesema mitihani itafanyika kama ilivyopangwa kuanzia Julai mosi hadi Julai 11, Mwaka huu.

 

Kaimu Mwenyekiti wa TEKUASA, Sembeye, alipopigiwa simu kuhusiana na uamuzi wa menejimenti amesema msimamo wao uko pale pale. Amesema bado majadiliano kati ya menejimenti na uongozi wa wahadhiri unaendelea ili kufikia mwafaka na hatimaye mitihani hiyo ifanyike.

 

Pia alipoulizwa endapo mwafaka hautafikiwa na kama kuna njia mbadala ya kuhakikisha mitihani inaandaliwa na kufanyika, Kaimu Makamu Mkuu wa Chuo amesema anaamani kuwa mwafaka utafikiwa.

 

Hata hivyo, baada ya  menejimenti ya chuo hicho kuitisha mkutano na waandishi wa habari, ilichukua zaidi ya saa tatu kujitokeza kwa wanahabari hao ambapo awali malumbano makali yalikuwa yakisikika kati ya Kaimu Mkuu wa Chuo, Mshauri wa Wanafunzi na viongozi wawili wa Chama cha Wahadhiri waliokuwa ofisini kwa Makamu Mkuu wa Chuo.

 

Aidha, malumbano hayo yalionekana ni kitendo cha menejimenti hiyo kuitisha mkutano wa wanahabari huku wakitaka viongozi wa chama hicho wawepo jambo ambalo lilionekana kupingwa na kuchukua muda mrefu bila kuafikiana, hivyo kuulazimu uongozi wa chuo kusoma tamko lao lenye maneno mawili tu kwamba mazungumzo yanaendelea na mitihani iko pale pale.

 

Kwa upande wake, Kaimu Mwenyekiti wa TEKUASA, Amani Simbeye, alipopigiwa simu kuulizwa juu ya msimamo wao kuhusu utungaji wa mitihani na tamko la uongozi wa chuo, amesema msimamo uliotolewa na uongozi wa chuo hawaujui na wala hauwahusu.

 

Ameongeza kuwa vikao vya mazungumzo vilifanyika ambapo walikubaliana kwanza mwafaka ufikiwe ndipo waitishe mkutano na vyombo vya habari, lakini wao kama chuo wamelazimisha na kudai kuwa mwafaka umepatikana na mazungumzo yanaendelea.

 

“Nikuambie mwandishi, sisi msimamo wetu uko pale pale na kungekuwa na tofauti yoyote tungeitisha mkutano wa waandishi ili tubadilishe msimamo, na kimsingi kuna mambo tulikubaliana kabla ya wao kutoa tamko lakini wanataka kutulazimisha,” amesema Simbeye.

By Jamhuri