Uzuri wa ng’ombe wa maziwa ni pale akishazaa na kuanza kutoa maziwa kwa wingi. Karibu sawa na hivyo, uzuri wa mwanafunzi machoni pa waajiri ni pale anapohitimu vyema masomo yake na kuwa tayari kwa kazi.

Watanzania wengi tumekuzwa katika mazingira ya kawaida – yenye changamoto nyingi huku wazazi na walezi wakihangaika kuhakikisha mahitaji yanapatikana. Kwa hiyo kwa waliozingatia walikotoka, nguvu iliyowekwa nyuma yao na matarajio ya wazazi au walezi, walifanya bidii sana shuleni.

Walijua kwamba ni muhimu kusoma na kutafiti kwa bidii, kwani hatimaye elimu ilikuwa na malengo ya kumkomboa mwanafunzi na kumwezesha kujitegemea ama kwa kuajiriwa au kujiajiri mwenyewe.

Tanzania yetu ina ushirikiano mzuri na nchi nyingi – tajiri na masikini. Na kwa hilo, tunamshukuru Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere.

Ushirikiano huo umezaa hamasa ya washirika wetu kuwapokea vijana wetu katika ngazi mbalimbali, kwa masomo ambayo baadhi ya nchi wahisani/washirika hugharamia na mengine serikali yetu hulipia.

Wapo wengine pia ambao kwa wazazi au walezi kuwa na uwezo wanalipiwa kama ilivyo kwa taasisi au jamii zilizoingia mfukoni kupeleka watoto wao ng’ambo kubukua.

Mwishoni mwa wiki iliyopita, London ilikuwa imejaa waajiri kutoka Tanzania. Walikuwa Watanzania pamoja na raia wa mataifa mengine, lakini wote walikuja kwa lengo la kuchota wahitimu kuwaajiri.

Ilikuwa kazi nzuri kwenye Hoteli ya Hilton hapa, ambako wahitimu wa sasa, waliohitimu kitambo na wanaokaribia kuhitimu walifika na vyeti vyao au maelezo kuhusu maendeleo yao na kufikiriwa na waajiri hao.

Kampuni zilikuwa nyingi hapa – kuanzia benki zetu tulizozoea kuhifadhi, kupitishia au kukopa visenti hadi zile za utalii, madini, hoteli, mawasiliano, miundombinu, ndege na kadhalika.

Ulikuwa wakati mzuri, kwa kampuni kufungua masikio na wanafunzi/wahitimu kufungua midomo na mikoba kuonyesha walicho nacho, baada ya wawakilishi wa kampuni zile kueleza walichokuwa wanataka.

Haikuwa na mushkeli kwa vile baada ya utangulizi, maelezo ya hapa na pale, na chai nzito tu, kulikuwa na kugawanyika kila mmoja akienda kule alikoona kunamfaa.

Hii hufanyika hapa London mara kwa mara, na wanaporudi nyumbani wawakilishi wa kampuni huweka makabrasha yao kusubiri wahitimu warudi nyumbani, wakiendelea na mawasiliano nao kila mara kwa njia za mtandao na hata simu.

Usisikitike wewe unayesoma au kuhitimu Dar, Malampaka, Tukuyu, Ugweno, Ngarenaro au Kirumba, kwa sababu huku ni mbali. Wewe unaweza kufunga safari hadi kwenye makao makuu ya mkoa wako na kuwasiliana na wakala wa hao jamaa, au unaweza kufunga safari hadi ilipo kampuni na kama una sifa hakuna shaka watakuchukua.

Lakini kitu kimoja ndugu zangu lazima tukubali; tumeingia Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) kwenye ushindani mkubwa, lazima tujioneshe sisi ni akina nani.

Licha ya kukipenda Kiswahili, kukienzi na kutaka iwe lugha ya kufundishia kuanzia chekechea hadi chuo kikuu, bado Kiingereza kinapewa kipaumbele na tukicheza tutapigwa bao, kama kwa bahati bado hatujapigwa.

Ukiacha ubora wa elimu ya wahitimu inayofuatwa na waajiri hapa London, kingine ni Kiingereza, mtiririko wa ung’eng’e na uwezo wa kunasa na kuelewa mara moja wanachozungumza Wazungu.

Waajiri wanataka watu wa namna hii, kwa sababu moja ya njia muhimu za kuvunja kuta na kuanzisha uhusiano ni lugha. Biashara bila kuwa na lugha nzuri ya kuelewana haiendi na Mzungu asipokuelewa au usipomwelewa vizuri anakuacha anapeleka fedha kwingine.

Nimalizie kwa kusema kwamba mmoja aliyepata kazi na anatarajia kuja huko baada ya Juni wala hakuja hapa kusoma, huwa anaosha magari na kupata pauni kadhaa kwa kila gari. Kwa vile anataka pesa, amewekeza kwenye Kimombo hadi jamaa wa kampuni moja huko wamempenda kwa sababu atawafaa hata kwa ‘customer service’.

Tafakari, fungua kitabu, soma na jifunze kuzungumza vizuri. Alamsiki.

By Jamhuri