Mara mbili, katika matoleo Na. 313 na
Na. 331, nimeandika makala yenye
maudhui ya aina hii ninayoandika leo.
Makala ya kwanza
niliandika: “Tusiendekeze usaliti huu”; na
kwenye makala ya pili nilihoji: “Nani ana
hakika Mtulia atatulia, hatahama tena?”
Nikasema yamekuwapo matukio mengi
ya wanasiasa kuvihama vyao na
kujiunga na vyama vingine vya siasa.
Wengi ni wale wanaotoka vyama vya
upinzani na kujiunga Chama Cha
Mapinduzi (CCM). Lakini wachache
wanatoka CCM na kwenda upinzani.
Wiki iliyopita Mbunge wa Ukonga, Mwita
Waitara (Chadema), ameungana na
wenzake kuhamia CCM – chama
kilichomkuza. Tukio hilo limenifanya

nirejee kwenye makala nilizozitaja.
Naheshimu na kutambua haki aliyonayo
Waitara na wenzake.
Hilo sina shaka nalo. Hasira zangu ni
kwenye matumizi mabaya ya fedha za
umma. Fedha za umma zinapotea kwa
sababu tu ya kukamilisha matamanio na
furaha ya watu. Uchaguzi mdogo
kwenye Jimbo kama la Ukonga
unagharimu zaidi ya Sh bilioni 1. Hii ni
pesa ya maana. Nitaeleza mbele ya
makala hii.
Ndugu zangu, natambua kuwa wapo
watu wengi wasiofurahishwa na hiki
kinachoendelea, lakini kwa sababu
zinazojulikana, wameamua kukaa kimya.
Mimi ni mfuasi wa CCM na zaidi ya yote
ni mfuasi wa nchi yangu – Tanzania. Hilo
naomba niliweke wazi.
Haya mambo tukiyafumbia macho kwa
sababu ya woga au unafiki, tutakuwa
hatuitendei haki nchi yetu. Tumeahidiwa
kuwa kabla ya Rais John Magufuli
kumaliza ngwe yake, tutakuwa na Katiba
mpya. Kwa hakika hiyo Katiba itakuwa
haijakamilika kama hatutakuwa

tumeweka breki ya kuzuia utapanyaji
huu wa fedha za umma unaosababishwa
na wanaohama vyama.
Tunaweza kutafuta maneno mengi
kulemba huu usaliti unaofanywa na
baadhi ya wanasiasa kwa wapigakura
wao na kwa walipakodi wote wa
Tanzania, lakini ukweli unabaki kuwa
kinachofanywa na hawa wanasiasa ni
dhuluma kwa nchi.
Mwalimu Nyerere katika
TUJISAHIHISHE anasema: “Makosa ni
makosa na dhuluma ni dhuluma, japo
watendao makosa hayo au dhuluma ile
ni wakubwa au ni wengi.”
Imekuwapo dhana kuwa mtu kujiunga au
kuhama chama cha siasa ni haki yake.
Sawa. Hata hivyo, haki ya mtu mmoja
haipaswi kupoka haki ya wengine. Sipati
shida hata kidogo kwa mwanachama
asiye mbunge au diwani kukihama
chama. Shaka yangu ipo kwa hawa
ambao tayari ni madiwani au wabunge,
tena wa kuchaguliwa.
Diwani au mbunge wa kuchaguliwa ni
mwakilishi wa wananchi. Uwakilishi wake

unahalalisha mkataba wake wa kazi kati
yake na wananchi au wapigakura katika
eneo lake. Diwani au mbunge
anapochaguliwa maana yake wananchi
wamemwamini. Wameutaka uwakilishi
wake. Wamewaacha wengine wakaona
yeye anawafaa kuwawakilisha.
Inapotokea diwani au mbunge akaamua
kuutupa au kuupuuza uamuzi wa
wananchi waliomwezesha kushika nafasi
hiyo, huyo diwani au mbunge anakuwa
ameasi.
Ndani ya CCM kuna watu wanaogopa
kuzungumza kwa sababu ya, ama hofu,
au unafiki tu. Wanadhani wakizungumza
watawaudhi wakubwa. Wanadhani
wakizungumza wataonekana ni
wapinzani.
Ni ukweli ulio wazi kuwa ndani ya CCM
wamo wafia CCM. Hawa wamekipenda
na kukitumikia chama bila kujali masika
wala kiangazi! Hata pale walipovaa sare
za chama hicho na kuzomewa mitaani,
hawakuikana imani yao. Wamekuwa
watiifu. Wana CCM wa aina hiyo wapo
tele!

Lakini ni kweli kuwa wapo ambao CCM
ilipopata msukosuko kidogo tu
walikikimbia chama hicho na kwenda
upande wa pili. Wapo ambao
walipokatwa majina wakachukia na
kuamua kuhama. Kwenye kundi hili
wamo kina Waitara, Mtulia na kadhalika.
Leo watu hawa wanarejea CCM na
kupewa heshima ya kupeperusha
bendera ya chama kwenye uchaguzi.
Wale wafia chama wanabaki kuwa na
kazi ya kuwanadi. Machoni wanaweza
kuonekana wamefurahi, lakini mioyoni
wanaumia. Wana chuki. Athari za haya
haziwezi kuonekana leo.
Hawa wanaorejea CCM wanatoa sababu
zinazofanana. Wanasifu utendaji kazi wa
Rais John Magufuli. Nani asiyejua
utendaji kazi wa kiongozi huyu? Mbona
sisi kwa miaka zaidi ya 20 tunaujua na
tumeendelea kuwa watiifu kwake? Wao
walikuwa nchi gani hata wasijue namna
alivyofanya kazi za kutukuka akiwa
Ujenzi, Ardhi, Uvuvi na kurejea Ujenzi?
Walikuwa wapi wakati Rais Benjamin
Mkapa akimtaja kama askari wake wa

mwavuli?
Tume ya Taifa ya Uchaguzi ilisema
uchaguzi, mathalani kama ule wa
Kinondoni ambako kulikuwa na vituo
zaidi ya 600; uligharimu Sh bilioni 1. (Sh
1,000,000,000). Fedha hizi ni mbali na
zile zinazotumiwa na vyama.
Bei ya dawati moja zuri kabisa ni Sh
100,000. Hii ina maana kuwa Sh bilioni 1
zingeweza kutengeneza madawati
10,000. Idadi hii ya madawati
ingetosheleza watoto 30,000. Idadi hiyo
ya wanafunzi ni kama shule 20. Kwa
maneno mengine ni kuwa endapo fedha
hizo zingeelekezwa kwenye madawati,
watoto 30,000 wangeondolewa adha ya
kuketi chini. Hiyo ni kwa jimbo moja
pekee. Je, kuna majimbo mangapi
yaliyotumika kupoteza fedha kwa namna
hii?
Ndugu zangu, dhuluma inayofanywa na
mtu mmoja matokeo yake yanabebwa na
walipakodi wote wa Tanzania. Tunaweza
kushangilia kwa sababu sisi ni CCM na
tunaona tunaukomoa Upinzani, lakini
tujue wanaoumia ni makabwela wote wa

nchi yetu.
Hatuwezi kuwa taifa la watu kuhama
vyama na baadaye kutumia fedha za
umma kuendesha uchaguzi. Sharti
tukatae kwa hoja na kwa sauti moja
matumizi haya mabaya na haramu ya
fedha za umma. Kinachofanywa na
wanasiasa ni matumizi mabaya ya fedha
za umma. Matumizi haya tunaweza
kuyakubali wakati wa kuziba pengo la
mbunge au diwani aliyefariki dunia, lakini
si kwa mwanasiasa aliyejilaghai au
aliyelaghaiwa na kuamua kukihama
chama kwa faida zake mwenyewe.
Kuna shule zisizo na madawati. Tunazo
shule zenye uhaba wa walimu. Kuna
shule nyingi nchini zisizokuwa na vitabu
vya ziada wala kiada. Kuna kata na
majimbo ambayo wananchi wake
hawayajui maji ya bomba wala ya
visima. Huko kwenye kata kuna zahanati
zisizo na ‘Panadol’.
Katikati ya mazingira haya ya dhiki
kunajitokeza madiwani na wabunge
wanaovihama vyama vyao ili uitishwe
uchaguzi mwingine wenye kutumia

mamilioni ya shilingi. Hii ni dhuluma.
Nimepata kusema, na naomba nirejee
kusema kuwa kama diwani au mbunge
anaamua kukihama chama, basi ahame,
lakini kusiwe na gharama za kuziba
pengo hilo. Kwenye uchaguzi kuna
mshindi wa kwanza, wa pili na kadhalika.
Sioni ni kwanini anapojiuzulu mshindi wa
kwanza, yule wa pili asizibe hiyo nafasi.
Hili linaweza lisiwe na tafsiri kwenye
msamiati wa demokrasia, lakini nadhani
hata kama lina mushkeli, basi tutafute
njia nyingine nzuri ya nafasi hiyo
kujazwa bila kuwa na uchaguzi mdogo.
Hapa ndipo tunapoweza kuona faida za
kuwa na uwakilishi wa uwiano wa vyama
kwa maana ya kuwa na nafasi ya chama
na si ya mtu (mshindi wa udiwani au
ubunge). Kwenye uwakilishi wa uwiano
wa viti kinachoangaliwa ni idadi ya viti
kwa chama, na kwa maana hiyo diwani
au mbunge anapopoteza sifa za
kuendelea na wadhifa wake, basi chama
kinatoa mwanachama mwingine kuziba
nafasi hiyo.
Hii ni njia nzuri kwa sababu inawezekana

wananchi wanapomchagua diwani au
mbunge, hawamchagui kwa sababu ya
sura, ukwasi, hali au mvuto wake.
Yawezekana wakamchagua kwa
kufurahishwa au kuridhishwa na sera za
chama anachotoka huyo mgombea.
Kama kura zinatokana na mvuto wa sera
za chama, ni vema kwa chama hicho
kumteua mwakilishi wa kuwakilisha sera
na mitazamo ya chama kilichopendwa
na wapigakura wengi. Huko tuendako
hatuna budi kulitazama hili. Lina faida
nyingi. Tuwe na madiwani na wabunge
kwa uwiano wa uwakilishi wa vyama.
Naamini tukifanya hivyo, huu usaliti wa
kuhama-hama vyama utapungua au
kukoma kabisa. Hatutapoteza fedha za
Watanzania kwa uchaguzi wa marudio.
Kwa kufanya hivyo tutakuwa na
wanasiasa serious, na siyo hawa
wanaokimbizwa na hali ya maisha.
Nimesema ni haki ya mtu kukihama
chama fulani na kujiunga na chama
kingine, lakini sidhani kama ni haki
kuwabebesha wananchi mizigo ya
uchaguzi mdogo, kwa sababu tu diwani

au mbunge ametumia akili binafsi kufikia
matamanio yake ya maisha.
Tuwe na utaratibu wa anayekihama
chama ahame yeye mwenyewe. Nafasi
ijazwe, ama na chama alichokihama au
aliyemfuata kwenye kura.
Kwa Sh bilioni 1 ambazo huenda
zikatumika kwenye uchaguzi mdogo
Ukonga, ina maana watoto 30,000 nchini
watakuwa wamekoseshwa madawati.
Sioni kwanini tukio baya kama hili lisiwe
kwenye orodha ya ‘dhambi’. Fedha hizi
zingepelekwa kwenye visima, kwa kila
kisima kugharimu Sh milioni 20;
tungepata visima 50 vya maji. Mtu
anayeamua ‘kufukia’ visima 50 si wa
kumwacha hivi hivi bila kumshitaki kwa
Mungu.
Tukiamini kuwa fedha zinazotumika
kwenye uchaguzi ni fedha za umma, na
kwamba zinatakiwa kuboresha maisha
ya wananchi maskini, basi bila shaka
tutaungana kulaani ukasuku huu wa
kisiasa.

Please follow and like us:
Pin Share