Wakala mkuu wa mgombea wa urais kwa tiketi ya Azimio la Umoja kwenye kituo cha kuhakiki na kutangaza kura za urais cha Bomas, Saitabao Kanchory jana Jumamosi Agosti 13, 2022 alizuiliwa kuingia kwenye sehemu ya kuhesabia kura (auditorium) na polisi wanaolinda eneo hilo.

Tukio hilo liliibua mvutano uliodumu kwa dakika kadhaa kwenye ukumbi huo, huku watu wakihoji kama polisi hao hawakumtambua kuwa Kanchory ni mmoja wa mawakala mwenye haki ya kuwa eneo hilo.

Wakati purukushani hizo zikiendelea Kanchory amesema kuwa kituo hicho kimegeuzwa kama ni mahali ambapo uhalifu unatokea.

“Ninataka kuwatangazia Wakenya kwamba Bomas imegeuzwa kuwa eneo la uhalifu,” Kanchory alitangaza kabla ya kuzimwa kwa kipaza sauti.

Hata hivyo baada ya tukio hilo kutokea mawakala wametaka kubadilishwa kwa polisi hao wanaolinda amani kwenye eneo hilo.

Hali hiyo imetokea ni siku chache tangu Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) ya Kenya itangaze kuongeza ulinzi hasa kwenye eneo la kuhesabia kura baada ya ugomvi wa mara ya kwanza kutokea uliohusisha mawakala wa Azimio la Umoja wanaomsimamia Raila Odinga kuwashutumu mawakala wa Kenya Kwanza wanaomsimamia William Ruto, kuingilia mfumo wa kuhesabu kura

By Jamhuri