Na Daniel Limbe, JamhuriMedia, Biharamulo

Imeelezwa kuwa baadhi ya wakazi wa wilaya ya Biharamulo mkoani Kagera wanalazimika kufuata maji safi na salama kwenye wilaya jirani ya Ngara huku wakinunua ndoo moja yenye ujazo wa lita 20 kwa shilingi 2,000 kutokana na maeneo yao kutokuwa na huduma hiyo.

Hatua hiyo inatajwa kukwamisha maendeleo ya kuinua uchumi wa kaya na taifa kwa ujumla,baada ya wakazi hao kutembea umbali mrefu kwenda kupata huduma hiyo sambamba na kutumia gharama kubwa kununua maji hayo.

Mkurugenzi wa Mamlaka ya Maji mjini Biharamulo(Buwsa), Siraj Abdul, akijibu maswali na malalamiko ya madiwani

Malalamiko hayo yametolewa na Diwani wa Kata ya Nyakahula,Apolinary Mugalura, kwenye kikao cha Baraza la madiwani wa halmashauri hiyo,huku akiitupia lawama mamlaka ya maji mjini Biharamulo(Buwsa) kushindwa kutatua adha hiyo kwa wananchi wake.

Amesema baadhi ya wakazi wa kata yake,hutembea umbali mrefu kwenda kata jirani ya Benako iliyopo wilaya ya Ngara kwaajili ya kupata huduma ya maji safi na salama na kwamba hali hiyo imekuwa ikikwamisha jitihada za wananchi kujikwamua kiuchumi.

“Kwenye Kata ninayofanya uwakilishi ya Nyakahula wananchi wangu wanakabiliwa na changamoto kubwa sana ya ukosefu wa maji safi na salama‚Ķtuliamini baada ya kuingizwa kata yetu kwenye mradi wa mamlaka ya maji mjini Biharamulo huenda kero kwa wananchi ingekuwa imefika mwisho lakini mpaka sasa wanataabika”

Baadhi ya madiwani wa halmashauri ya wilaya ya Bibaramulo wakiwa kwenye kikao chao leo.

“Nimekuwa nikipokea malalamiko mengi kwa wananchi wangu wakitaka kujua adha hiyo itakwisha lini‚Ķhata hivyo wanatumia gharama kubwa za kununua maji safi na salama kwa shilingi 1,500 hadi 2,000 kwa ndoo moja yenye ujazo wa lita 20, pesa ambayo ingeweza kusaidia maendeleo mengine ya kijamii ikiwemo kuinua uchumi wa kaya wilaya na taifa kwa ujumla” amesema Mugalura

Mkurugenzi mamlaka ya maji mjini Biharamulo(Buwsa) Siraj Abdul, amekiri kuwepo kwa changamoto ya uhaba wa maji kwenye kata hiyo huku akiahidi kushughulikia changamoto hiyo na kwamba wananchi wavute subra kwa kuwa serikali imeshalitambua hilo.

Diwani wa kata ya Nyakahula,Apolinary Mugalura,baada ya kuwasilisha malalamiko ya wananchi wake.

Mwenyekiti wa halmashauri hiyo,Leo Rushahu, ameitaka mamlaka hiyo ya maji Biharamulo, kufika maeneo ambayo yanalalamikiwa na wananchi ili kuona namna wanavyoweza kutatua changamoto zinazo wakabili.

Hatua hiyo itasaidia kuinua uchumi wa kaya kutokana na wananchi hao kutumia muda mwingi kutafuta maji na kushindwa kwenda kufanya shughuli za uzalishaji mali.

Mkurugenzi wa halmashauri ya Biharamulo,Inocent Mukandara, akitoa ufafanuzi kwa madiwani.