Na Cresensia Kapinga, JamhuriMedia, Songea

Walimu wa Kiswahili na wadau hapa chini wametakiwa kuona umuhimu wa lugha ya kiswahili katika kuimarisha utamaduni na elimu jambo ambalo litachangia jamii kukuza lugha ya kiswahili, uzalendo na uelewa wa historia ya nchi yao na si vinginevyo.

Hayo yamesemwa jana na Waziri wa Utamaduni,Sanaa na Michezo Dkt. Damas Ndumbaro wakati akifungua mafunzo ya siku moja ya matumizi ya kiswahili fasaha na sanifu kwa walimu wa kiswahili na wadau yaliyofanyika katika ukumbi wa mikutano wa Shule ya Sekondari ya Wasichana ya Songea Girls iliyopo katika Manispaa ya Songea mkoani Ruvuma.

Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo Dkt. Damas Ndumbaro akihutubia walimu wa kiswahili na wadau kwenye mafunzo ya matumizi sanifu na fasaha ya kiswahili yaliyofanyika Jana katika ukumbi wa mikutano wa shule ya Sekondari ya Wasichana Songea Girls iliyopo katika Manispaa ya Songea mkoani Ruvuma.

Alisema kuwa katika kuelekea maadhimisho ya Tamasha la tatu ya utamaduni kitaifa ambayo yanafanyika mkoani Ruvuma na mgeni rasmi katika maadhimisho hayo atakuwa Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt.Samia Suluhu Hassan ,Wizara ya utamaduni,sanaa na Michezo kwa kushirikiana na Baraza la Kiswahili la Taifa (Bakita)wameona umuhimu kwa wanajamii kujifunza na kutumia kiswahili fasaha ili kudumisha utamaduni na kuimarisha mawasiliano.

Waziri Dkt. Ndumbaro alisema kuwa mafunzo hayo yenye lengo la kukumbushana matumizi ya kiswahili fasaha na sanifu kwa tija ya jamii na Taifa kwa ujumla hivyo inawapasa kutafakari jukumu lao wakiwa kama walimu wa kiswahili katika kufundisha na kuendeleza ufasaha na usanifu wa lugha ya kiswahili kwa kizazi kilichopo na kijacho.

“Ndugu washiriki kama vile jua lichomozavyo upande wa Mashariki na kuangaza nuru yake hadi upande wa Magharibi, ndivyo hali ya kiswahili ilivyo hivi sasa, kiswahili kimeendelea kuchanja mbuga na kuingia katika anga za kimataifa na hivyo Tanzania kama kinara wa Kiswahili fasaha na sanifu hata hivyo kiswahili hicho kinajengwa nyumbani, shuleni na kwenye jamii kwa ujumla wake.”alisema Waziri Dkt. Ndumbaro.

Aidha Waziri wa utamaduni,Sanaa na Michezo Dkt.Ndumbaro amewasisitiza walimu wa kiswahili na wadau kutumia fursa hiyo ya mafunzo kujifunza na kubadilishana mawazo ili kukuza lugha ya kiswahili na kuongezeka uelewa na upokeaji wa maarifa katika jamii, kuboresha ujuzi wa walimu na kuhamasisha matumizi bora ya lugha ya kiswahili.

Katibu mtendaji Baraza la kiswahili la Taifa Bakita Consolata Mushi akimkaribisha mgeni rasmi Waziri wa Utamaduni Sanaa na Michezo Dkt Damasi Ndumbaro aweze kuzungumza na walimu wa kiswahili na wadau.

Kwa upande wake katibu mtendaji baraza la kiswahili la Taifa (Bakita) Consolata Mushi alisema kuwa lengo la mafunzo hayo ni kuwakumbusha matumizi ya kiswahili fasaha na sanifu kwa sababu wanaamini walimu wa kiswahili na wadau ndio wanaotengeneza kiswahili ndani ya jamii, walimu wanalo jukumu kubwa katika katika kufundisha wanafunzi lakini wadau wengine wanajukumu kubwa kuanzia kwenye familia na kwenye jamii.

“Tumekuja hapa katika kuelekea siku ya maadhimisho ya Tatu ya utamaduni wa Taifa na tukaona tusitoke bure hapa Songea bila kuacha kitu na miongoni mwa mambo tuliyoyapanga ni kuhakikisha kwamba tunawaelimisha,tunawakumbusha namna ya kuzingatia ufasahaa na usanifu kwa lugha ya kiswahili. “Alisema Consolata.

Naye Mkurugenzi wa Idara ya maendeleo ya utamaduni, Wizara ya utamaduni ,Sanaa na Michezo Bonifas Kadili alisema kuwa wamewaletea mafunzo hayo wanasongea kwa kuwa wanatambua mchango mkubwa katika ukuaji na ukuzaji wa lugha hadhimu ya kiswahili na hii ni fursa kwa wanasongea kupata ajira kwa sababu kiswahili kinatoa ajira lakini kiswahili ni bidhaa hivyo wanasongea wanahitajika kutumia bidhaa hii katika kujinufaisha na wakati huo wanaikuza lugha hadhimu ya kiswahili Ruvuma, Tanzania na Duniani kwa ujumla.

Mwalimu Thobias Mkongwa Mwalimu wa Shule ya Sekondari Subira iliyopo Manispaa ya Songea alisema kuwa kutokana na mitaala mingi sana inabadilika kuhusiana na kiswahili kupitia mafunzo hayo itawawezesha kwenda kuwajenga vizuri wanafunzi waweze kuendana na wakati nayatawezesha kiswahili kiweze kuzungumzika kile kiswahili kilichokuwa sahihi na sio kiswahili kile cha mtaani.

Baadhi ya walimu wa kiswahili na wadau wakimsikiliza mgeni rasmi Waziri wa Utamaduni Michez, Sanaa na Michezo Dkt Damasi Ndumbaro kwenye mafunzo ya siku moja ya matumizi ya kiswahili fasahana sanifu.
Please follow and like us:
Pin Share