Ukosefu wa vyoo katika baadhi ya shule za msingi na sekondari Wilaya ya Moshi umechangia kwa baadhi ya wanafunzi kujisaidia vichakani na wengine kwenye vyoo vya wananchi wanaoishi karibu na shule hizo.

Hatua hiyo imetokana na baadhi ya miundombinu ya vyoo kwenye shule hizo kuwa chakavu na kutishia usalama wa wanafunzi kutokana na vyoo hivyo kuwa katika mazingira hatarishi.

JAMHURI limetembelea baadhi ya shule hizo na kushuhudia baadhi ya vyoo vikiwa vimefungwa kutokana na kuwa katika hali mbaya iliyosababishwa na majengo yake pamoja na matundu kujengwa miaka mingi iliyopita.

Katika Shule ya Msingi Mkolowony iliyopo Kata ya Mamba Kusini, JAMHURI limeshuhudia vyoo hivyo vikiwa vimefungwa kwa kuwekewa miti yenye miba kuzuia wanafunzi kuingia kutokana na kuwa katika mazingira hatarishi.

Baadhi ya walimu wa shule hiyo waliozungumza kwa sharti la kutotajwa majina yao, wamesema hali hiyo imesababisha wanafunzi kujisaidia vichakani na baadhi yao wakijisaidia kwenye vyoo vya wananchi wanaoishi jirani na shule hiyo.

“Nadhani mwenyewe umejionea hali ilivyo, kwa kweli hali ni mbaya, lakini sisi si wasemaji, mtafute mwalimu mkuu yeye ndiye mwenye shule na anaweza akakupa taarifa nzuri,” amesema mwalimu mmoja.

JAMHURI limegundua zaidi ya wanafunzi 300 wa shule hiyo wanataabika kupata sehemu ya kujisaidia kutokana na kufungwa kwa vyoo hivyo, hali ambayo inaweza kusababisha mlipuko wa magonjwa yakiwamo ya kipindupindu.

Mbali na tatizo la matundu ya vyoo, shule nyingi za msingi katika wilaya hiyo zinakabiliwa na tatizo kubwa la uchakavu wa majengo pamoja ja uhaba wa walimu ambapo baadhi zina walimu wawili wanaofundisha kuanzia shule ya awali hadi darasa la saba.

Katika Shule ya Msingi Mrienyi, iliyopo Kata ya Mamba Kusini, JAMHURI limeshuhudia shule hiyo ikiwa na walimu wawili tu ambao wamekuwa wakipokezana kufundisha wanafunzi kuanzia wale wa shule ya awali mpaka darasa la saba.

Ofisa Elimu Msingi Wilaya ya Moshi, Deusdedit Bimbalirwa, amezungumza na JAMHURI na kukiri kuwepo kwa changamoto ya miundombinu katika shule za msingi, ikiwamo hali mbaya ya vyoo, uchakavu wa majengo pamoja na uhaba wa walimu.

 Amesema tayari wameshachukua hatua kukabiliana na changamoto hizo ikiwamo kuainisha ukubwa wa tatizo na kuandaa bajeti ambayo tayari wameshaiwasilisha ofisi ya mkurugenzi wa halmashauri hiyo kwa ajili ya utekelezaji.

“Kwa kweli hizo changamoto zipo na tumeshaziona na kwa sasa tumeanza kuzifanyia kazi na changamoto kubwa ni hiyo ya matundu ya vyoo kwa baadhi ya shule zetu za msingi,” amesema.

Amesema halmashauri kwa kushirikiana na wadua ikiwamo Hifadhi ya Taifa ya Mlima Kilimanjaro (KINAPA) na Taasisi moja isiyo ya kiserikali ya FT Kilimanjaro, wamekuwa wakijitahidi kuboresha miundombinu ya shule hizo.

Kuhusu uhaba wa walimu kwa baadhi ya shule hizo, ofisa elimu huyo amesema suluhisho pekee la kukabiliana na tatizo hilo ni serikali kuajiri walimu wapya na watakaokidhi mahitaji.

 Takwimu za Machi 31, mwaka jana zinaonyesha kuwa kulikuwa na mahitaji ya walimu 2,329 na waliokuwepo kwa wakati huo ni 2,011 ikiwa ni pungufu ya walimu 318 na ofisa elimu huyo anasema idadi hiyo itakuwa imeongezeka kwa mwaka huu.

Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Moshi, Michael Kilawila, ameliambia JAMHURI kuwa zinahitajika Sh bilioni moja kutatua changamoto za miundombinu ya vyoo kwa shule za msingi na sekondari katika halmashauri yake.

Amesema vyoo vingi vimebomoka kutokana na kujengwa kwa mfumo wa zamani, ambavyo kwa mujibu wa mwongozo mpya wa serikali, vyoo hivyo havistahili kuwepo kwa sasa.

Please follow and like us:
Pin Share