Siku kadhaa baada ya Rais John Magufuli kutengua uteuzi wa aliyekuwa Mkuu wa Wilaya ya Tarime, Glorious Luoga, mfanyabiashara maarufu, Peter Zakaria, ambaye yuko mahabusu ameibua mambo mapya yanayomhusu Luoga.

Zakaria ambaye amezungumza na Gazeti la JAMHURI kupitia kwa msemaji wa familia hiyo, Samuel Chomete, amesema amefurahishwa na uamuzi wa Rais Magufuli wa kumfuta kazi Luoga.

Januari 27, mwaka huu, Rais Magufuli alitengua uteuzi wa Luoga, kisha kumteua Charles Francis Kabeho, kuongoza Wilaya ya Tarime. Kabla ya uteuzi huo Kabeho alikuwa kiongozi wa mbio za Mwenge mwaka jana.

“Nimeonana na kuzungumza na Peter Zakaria aliyepo mahabusu. Ameniambia amefurahishwa sana na uamuzi wa Rais Magufuli kumfukuza kazi DC Luoga…ameniambia Luoga ndiye chanzo kikuu cha migogoro ya familia yake, kwa vile alikuwa anamdai fedha.

“Zakaria anamshukuru sana Rais Magufuli kuwaondolea Wana Tarime huyu mtu, alikuwa ni tatizo,” amesema msemaji wa familia ya Zakaria.

Msemaji huyo wa familia ambaye ni mtoto wa kaka wa Zakaria, amesema kazi ya kiongozi ni kupigania maendeleo ya wananchi.

“Zakaria anampongeza Mkuu mpya wa Wilaya ya Tarime, Francis Kabeho, kwa kuaminiwa na Mheshimiwa Rais Magufuli.

“Familia inamuomba sana Kabeho awasaidie Wana Tarime kupata maendeleo ya kweli. Atatue migogoro iliyoachwa na Luoga,” amesema Chomete.

Zakaria yupo Gereza la Musoma mkoani Mara akishikiliwa kutokana na tuhuma za kujaribu kuwaua kwa kuwapiga risasi maofisa Usalama wa Taifa, zogo hilo lilitokea mwaka jana katika ofisi yake mjini Tarime. Tuhuma nyingine inayomkabili Zakaria ni uhujumu uchumi.

Baadhi ya wananchi wanasema uongozi wa Luoga haukuakisi maendeleo ya wananchi wanyonge. Ikumbukwe kwamba Chama Cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Mara kimewahi kuwa na mgogoro na DC Luoga.

Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Mara, Samuel Kiboye (Namba Tatu) aliwahi kumtuhumu kuhusika na fedha za ujenzi wa Kiwanda cha Sukari (Tarime Sugar).

Tuhuma

Familia ya Zakaria inamtuhumu Luoga kwa kukataa kulipa deni la mashine ya kutengenezea mikate, inasemekana Luoga aliuziwa mashine hiyo na Zakaria lakini hakulipa.

“Zakaria alimuuzia Luoga mashine ya kutengeneza mikate, thamani yake ni Sh milioni 25. Lakini amekataa kumlipa.

“Mashine hiyo ilisafirishwa hadi Dodoma Area ‘D’ kwa gharama zetu. Hajatulipa hata fedha za mafuta ya gari tuliyotumia kuipeleka mashine yake Dodoma,” amesema Chomete.

Tuhuma nyingine zinahusu matumizi ya ukarabati wa Hospitali ya Tarime, kiasi cha Sh milioni 87, kilitolewa na baadhi ya wadau akiwemo Zakaria ili kuboresha Hospitali ya Wilaya ya Tarime mwaka 2016.

Familia ya Zakaria ina mtuhumu kiongozi huyo kufuja fedha hizo, hadi kufikia kumtishia Zakaria baada ya kuanza kuhoji zilipo.

“Aliniambia mimi nikamwambie Zakaria, ukiendelea kunifuatafuata nitakushughulikia hadi ufilisike. Wewe siyo tajiri kama akina Mengi na Mo.

“Zakaria ndiye alikuwa mwenyekiti wa kamati ya maboresho. Baada ya kukosekana kwa fedha hizo Zakaria alitoa Sh milioni 90 kufanikisha ukarabati huo,” Chomete ameliambia JAMHURI.

Anasema: “Zakaria alipeleka simenti (mifuko ya saruji). Alinunua hadi madawa akapeleka pale hospitalini ili kusaidia, nyaraka zote zipo,” anasema msemaji huyo wa familia ya Zakaria.

Mzee Chomete alipoulizwa na JAMHURI mazingira ya madai ya Luoga kufuja fedha hizo, alidai zilikuwa zikikusanywa nje ya utaratibu uliowekwa na kamati ya maboresho.

“Kila aliyetoa fedha kwa  mkuu wa wilaya alikuwa anamwandikia mwenyekiti wa shughuli hiyo kumfahamisha kwamba wamempa fedha DC,” anafafanua.

Luoga ajibu mapigo

Akizungumza na Gazeti la JAMHURI kuhusu tuhuma hizo, Luoga amekanusha na kuziita uzushi mtupu.

“Watu bwana… watu husema ondoka usemwe! Tujifunze hata kusema mazuri mtu aliyoyafanya. Hayo wanayosema ni uzushi tu.

“Hiyo mashine ya kutengeneza mikate siyo ya milioni 25 kama walivyokwambia. Hiyo mashine mimi ndiye niliyemuagiza Zakaria aninunulie kutoka China.

“Alininunulia na kuniletea. Mashine ilikuwa ya Sh milioni 11.7 hivi. Ilikaa kwake baadaye nikaikomboa kwa kuuza gari la mke wangu.

“Yeye mwenyewe Zakaria alitafuta mnunuzi wa hilo gari, akampata. Nakumbuka gari hilo lilinunuliwa na Chomete, mpaka leo hii wanalo gari hilo hapo Tarime,” amesema Luoga.

Hata hivyo mzee Chomete amekiri gari hilo ya Luoga ilinunuliwa na mtoto wake aitwaye, Michael Chomete.

“Gari hilo lilikuwa linamilikiwa na mke wangu, nililiuza kwa Sh milioni 4.5. Zakaria alikuwa anamtumia kijana wake anaitwa Raja anakaa India,” Luoga ameliambia JAMHURI.

Kuhusu tuhuma za kufuja Sh milioni 87 za kamati ya maboresho ya Hospitali ya Wilaya ya Tarime, Luoga amesema tuhuma hizo hazina ukweli.

Ingawa amekiri kuunda yeye mwenyewe kamati hiyo, lakini amesema hakuna fedha yoyote aliyokwapua.

“Hospitali ya Tarime nimeikuta inanuka. Ilikuwa chafu nikaona niunde kamati tuifanyie maboresho, tukafanikiwa hadi waziri mkuu akanipongeza, akasema mbona ni kama mpya!

“Mdau aliyetoa fedha nyingi kwenye kamati ya maboresho ni Acacia Mining. Alitoa Sh milioni 220 tena kwa mkataba na kwa awamu.

“Acacia walikuwa wanakuja kuangalia ujenzi kisha wanatoa fedha. Fedha zote zilikuwa zikiingizwa kwenye akaunti ya kamati na imefanyiwa uchunguzi hadi Takukuru, hawakubaini wizi wala udanganyifu wowote.

“Sasa mimi nilichukuaje hizo fedha?” anahoji Luoga huku akisema anashangaa kama tuhuma hizo zinatolewa na Zakaria mwenyewe.

Amesema kama anadaiwa fedha wakafungue kesi mahakamni, si magazetini. “Kwa ufupi, hayo ni majungu na naomba usitumike,” amesema Luoga.

Luoga alikwenda mbali zaidi na kusema: “Zakaria ana matatizo yumo ndani. Watu wanasema kukamatwa kwake mimi nimehusika.

“Zakaria alikuwa rafiki yangu, rafiki yangu na ataendelea kuwa rafiki yangu,” amesema Luoga.

Takukuru wanena

JAMHURI limezungumza na Kamanda wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), Mkoa wa Mara, Alex Kuhanda, juu ya tuhuma za ubadhirifu katika kamati hiyo ya maboresho wilayani Tarime.

Anasema Takukuru walishafanya na kukamilisha uchunguzi wao juu ya tuhuma za upotevu wa Sh milioni 300 katika kamati hiyo iliyoundwa na Luoga.

“Suala la upotevu wa Sh milioni 87 siwezi kulisemea. Sisi tulishakamilisha uchunguzi wetu wa tuhuma za Sh milioni 300.

“Kwa sasa suala hilo lipo ngazi za juu, tunasubiri maelekezo,” amesema Kamanda Kuhanda.

Alipoulizwa mlengwa wa tuhuma za ubadhirifu huo wa Sh milioni 300 na mazingira yake, Kuhanda alicheka kwanza kisha akakataa kumtaja, akidai ataharibu.

“Aaah (kicheko) nisingependa kusema nani mhusika. Kama nilivyokuambia suala hili lipo ngazi za juu.

“Nikisema naweza kuharibu. Nisingependa niingilie maamuzi,” amesema Kuhanda.

Kuhusu mazingira ya upotevu wa kiasi hicho cha fedha, Kuhanda ameema: “Hizi fedha kwa namna zote mbili, zilikusanywa nje ya utaratibu na zikatumika nje ya utaratibu kwenye kamati hiyo ya maboresho.”

Please follow and like us:
Pin Share