Wanajeshi 25 waliotiwa hatiani kwa kumkimbia adui wakati wa mapigano na kundi la waasi la M23 mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo wamehukumiwa kifo kwenye kesi iliyofanyika jana huko Kivu Kaskazini.
Kwa mujibu wa mawakili wao, kesi hiyo iliwajumuisha watuhumiwa 31, wakiwemo wanajeshi 27 na wanne kati ya wake zao.
Kesi hiyo iliendeshwa kwenye mahakama ya kijeshi ya Butembo, karibu na mstari wa mbele wa mapambano.
Miongoni mwa mashitaka waliyoshitakiwa nayo yalikuwa ni kuharibu silaha za kivita, kukaidi amri halali na wizi, ambapo wanajeshi 25, wakiwemo makapteni wawili, walihukumiwa kifo.
Waliosalia, wakiwemo wake zao, waliachiwa huru kwa kukosekana ushahidi. Kundi la M23 limetwaa udhibiti wa miji kadhaa muhimu , ukiwemo mji wa kimkakati wa Kanyabayonga, unaounganisha miji miwili ya kibiashara ya Butembo na Beni.