Shambulio la kombora la Urusi kwenye mazoezi ya kijeshi katika eneo la mpaka la Sumy la Ukraine limewaua wanajeshi sita na kuwajeruhi zaidi ya wengine 10, imesema Wizara ya Ulinzi ya Kitaifa ya Ukraine.

Wizara ya ulinzi ya Urusi hapo awali ilitoa mkanda wa video unaoonyesha shambulio la kombora la Iskander kwenye kambi ya mafunzo ya kijeshi, na shirika la habari la serikali Tass lilisema hadi watu 70 wamefariki dunia.

Mkoa wa Sumy umekuwa chini ya mashambulizi ya mara kwa mara, na Ukraine ilizindua uvamizi wa miezi kadhaa wa sehemu ya eneo jirani la Kursk la Urusi kutoka huko.

Jeshi la Ukraine lilisema lengo la mashambulizi hayo lilikuwa ni kusaidia kuunda eneo salama kulinda Sumy, lakini baadhi wamelalamikia ukubwa wa hasara za kijeshi.

Video ya jeshi ya Urusi ambayo haijathibitishwa ilionyesha makumi ya wanajeshi wakitembea kwenye njia karibu na eneo lenye miti na kufuatiwa na mlipuko na moshi mwingi.

Utafiti uliofanywa na BBC Verify ulionyesha kuwa kambi hiyo ya mafunzo ililengwa kaskazini mwa eneo la Sumy, kusini mwa mpaka wa Urusi.

Ikulu ya Kremlin pia ilituma maelfu ya wanajeshi wa Korea Kaskazini katika eneo hilo kwa nia ya kuliteka tena eneo hilo.

Matumaini ya kukaribia kusitishwa kwa mapigano yanafifia, licha ya mazungumzo ya ngazi ya chini kati ya Ukraine na Urusi mjini Istanbul Ijumaa iliyopita.

Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani Marco Rubio alisema alitarajia Urusi kuwasilisha “masharti mapana ambayo yataturuhusu kuelekea usitishaji vita”, hata hivyo Volodymyr Zelensky wa Ukraine amesema Urusi “inajaribu tu kupata muda ili kuendeleza vita na uvamizi wake”.