Wananchi wametakiwa kuchukua tahadhari juu ya mlipuko wa janga la Ebola ambao unaripotiwa kutokea nchi jirani ya Uganda huku wakitakiwa kuondokana na safari zisizo za lazima ili kuepukana na ugonjwa huo.

Hayo yamesemwa jijini Arusha na Rais wa Chama cha Madaktari Tanzania (MAT),Dkt.Shadrack Mwaibambe wakati akizungumza katika mkutano wa 54 wa chama hicho unaofanyika jijini Arusha.

Mwaibambe amesema kuwa ,kutokana na kuwepo kwa mlipuko huo jamii inatakiwa kuelimishwa mapema kuchukua tahadhari ikiwemo kuepukana na safari zisizo za lazima kwenda nchini Uganda.

Daktari wa afya ya kinywa mkoa wa  Arusha,Dkt. Omar Chande akizungumza katika mkutano huo jijini Arusha.

“Kumekuwepo na muingiliano mkubwa sana wa wananchi kwenda nchi jirani kwa ajili ya shughuli mbalimbali kwani Uganda hapo sio mbali ni kilometa mia mbili kutoka mpaka wa Tanzania ,hivyo ni lazima kila mmoja wetu atoe elimu ya kutosha ili wananchi waweze kuchukua tahadhari mapema “amesema .

Mwaibambe amesema kuwa,kutokana na kuripotiwa kwa ugonjwa huo nchini Uganda ni muhimu serikali ikachukua tahadhari mapema ili ugonjwa huo usiingie nchini kwetu na kuweza kuleta madhara .

“Kutokana na ugonjwa huo ni vizuri tahadhari ikachukuliwa kwenye viwanja vya ndege kwa kuwakagua watu wanaoingia na watakaogundulika kuwa na ugonjwa huo wawekwe garanteeni ili ugonjwa usiingie nchini kwetu na kwa kufanya hivyo tutaweza kudhibiti kwa kiwango kikubwa sana.”amesema Dk Mwaibambe .

Amesema kuwa ,katika mkutano huo watajadili agenda ya umuhimu wa kupata chanjo ya pili ya uviko 19 kwa wale watu ambao hawakupata awamu ya kwanza ili waweze kupata awamu ya pili sambamba na kujadili namna ya kuchukua hatua katika kudhibiti ugonjwa wa Ebola .

Kwa upande wake Rais mstaafu wa chama cha madaktari Tanzania,Dkt. Elisha Osati amesema kuwa, kutokana na kuwepo kwa mlipuko wa ugonjwa wa Ebola ulioripotiwa nchini Uganda ni wajibu wa kila mmoja wetu kuweza kuchukua tahadhari za haraka hususani katika mipaka yetu kuhakikisha ugonjwa huo hauingii hapa nchini kwetu.

Baadhi ya madaktari hao wakiwa katika picha ya pamoja na viongozi wa chama hicho katika mkutano unaoendelea jijini Arusha.

Aidha amewataka wananchi kuhakikisha wanafuata masharti yanayotolewa na wataalamu namna ya kupambana na ugonjwa huo wa Ebola .

Kwa upande wake Daktari wa afya ya kinywa mkoa wa Arusha,Dkt. Omar Chande amesema kuwa,ni vizuri chama cha madaktari Tanzania kuendelea kuongeza nguvu zaidi katika kuhamasisha utoaji wa chanjo ya uviko 19 kwenye vituo vya afya ili watu wote wapate muhamko wa chanjo hiyo.

Aidha amewataka wadau mbalimbali kutoa elimu ya kutosha kwa wananchi juu ya kuchukua tahadhari kuhusu ugonjwa huo ili usiweze kuingia huku nchini.

By Jamhuri