Miaka kadhaa iliyopita Simba ilifungwa na Enyimba magoli 3-1 katika Uwanja wa Uhuru. Simba ilizidiwa sana na timu hiyo kutoka Nigeria. Kwenye ufundi pamoja na stamina wachezaji wa Enyimba walikuwa wako imara kuwazidi wachezaji wa Simba.

Baada ya mechi kumalizika, Kocha wa Enyimba akasema Simba ni timu nzuri lakini timu yake ilikuwa bora zaidi. Enyimba wakaondoka zao wakiwa kama washindi waliostahili kushinda kwa kila hali uwanjani.

Hata kabla ya Simba kufungwa na Enyimba, makocha wa timu kutoka nje wamekuwa na tabia ya kistaarabu ya kuwasifia wachezaji wetu baada ya filimbi ya mwisho kupulizwa.

Mwaka 1988, Al Ahly ya Misri ilikuja kucheza na Yanga, mechi ya Ligi ya Mabingwa Afrika, baada ya pambano kumalizika kwa suluhu, kocha wa timu hiyo aliwasifia sana Abubakar Salum na marehemu Celestine ‘Sikinde’ Mbunga.

Yanga walipokwenda Misri wakakumbana na kipigo cha magoli 4-0. Sifa walizomwagiwa mawinga wa Yanga wa wakati ule zilikuwa ni sehemu ya maneno mazuri ambayo makocha wanajua kwamba mashabiki hupenda kuyasikia.

Taifa Stars ilifungwa na Ivory Coast magoli 4-2 pale Uwanja wa Taifa, ikiwa ni mechi ya kutafuta nafasi ya kwenda Kombe la Dunia la mwaka 2014. Kocha mkuu wa Ivory Coast akaimwagia sifa nyingi timu yetu wakati akiongea na waandishi wa habari baada ya pambano kumalizika.

Hata timu yao ilipotua Abidjan, bado akaendelea kusema kwamba wameshinda kwa sababu ya uzoefu wa kina Yaya Toure na si kwa sababu nyingine yoyote ile. Lakini yatazame mafanikio ya Ivory Coast kuanzia wakati ule, wametwaa ubingwa wa Afrika na wanao mtiririko mzuri wa timu za vijana.

Sisi tuliobweteka baada ya kusifiwa, tumezidi kupoteza mwelekeo na tumeshindwa hata kuiendeleza Taifa Stars iliyotupa matumaini. Siku zote makocha wa kigeni hutumia lugha ya kiungwana iliyojaa heshima ya uanamichezo wakati wanaiongelea timu pinzani.

Kocha hajui mwajiri wake mpya ni nani na anatoka katika nchi gani, hivyo hawezi hata siku moja kujiingiza kwenye aina ya uongeaji uliojaa dharau. Kocha mkuu wa Chile atawasifia wachezaji wa Somalia, huku akisema yule aliyevaa jezi namba 10 na yule aliyevaa jezi namba 7 ni wachezaji wenye kufaa kuchezea timu yoyote ile kubwa duniani.

Kocha huyo ataongea kwa heshima hata kama baada ya filimbi ya mwisho matokeo yatasomeka kama ifuatavyo, Chile 8, Somalia 0.

Kocha wa Chile hataweza kuiponda Somalia kwani upo uwezekano katika siku za usoni nchi hiyo ikamuajiri kama mkurugenzi wa ufundi. Makocha wa kigeni kama wangekuwa ni watu wenye kupungukiwa heshima, wangeweza kabisa kuwaponda wachezaji pamoja na makocha wetu.

Makocha wa kigeni wangeweza kuongea lugha ya kutukatisha tamaa na labda tungeishia kuwanunia kama ishara ya kutoafikiana na kauli zao za dharau. Bahati mbaya ni kwamba tunapoambiwa kuwa wachezaji wetu ni wazuri na sisi tunakubaliana na uongo uliotamkwa kistaarabu.

Tunaingia wazima wazima kwenye mtego wa uongo unaotamkwa kisomi. Tunaanza kuongea lugha ile ile inayotumiwa na makocha wa kigeni. Tunabweteka na madhara ya tabia hiyo ni kushindwa kukitofautisha kiwango chetu halisi cha mwaka jana na mwaka huu.

Wachezaji wetu wangedhihirisha ubora wa kauli za makocha wa kigeni kwa kuziwezesha timu zetu kufika mbali kimataifa kila mwaka. Mchezaji kama Mbwana Samatta ameshacheza mechi nyingi ngumu kuliko mchezaji yeyote yule wa Taifa Stars ya miaka ya hivi karibuni.

Hajakubali kuwa alipofika ndio mwisho wa safari ya mafanikio, kwa hiyo unaweza kumsifia  lakini huwezi kumdanganya kupitia sifa ambazo binafsi ameshazoea kuzisikia.

Sura ya kijana huyo aliyekulia Mbagala imeshakuwa maarufu miongoni mwa wadau wa karibu wa soka la Afrika. Yupo Ubelgiji na ameweza kuwa sehemu ya mipango ya makocha makini ambao wanapokuja Tanzania hutusifia baada ya Taifa Stars, Yanga, Simba na Azam FC, kupokea vipigo.

 Angebakia kuchezea Simba labda hivi sasa angekuwa sehemu ya wale wachezaji wanaosifiwa na makocha wa timu za kigeni kuwa eti wamecheza vizuri na wanavyo vipaji vikubwa.

Tangu tupate uhuru tumeshasifiwa sana na makocha wa kigeni na wakishamaliza kutusifia huwageukia wachezaji wao na kuwapongeza kwa kuweza kucheza kadiri ya maelekezo waliyopewa.

Kocha huwakumbatia wachezaji wake, wakati basi lililowabeba wachezaji likielekea uwanja wa ndege. Sisi tunaosifiwa tunabaki  na mwenendo wetu ule ule usiobadilika.

Tunabakia na hazina ya kumbukumbu nyingi sana za makocha wa kigeni wanaowasifia wachezaji wetu, huku wakishangaa eti ni kwanini mchezaji fulani bado anachezea timu ya Ligi Kuu ya Tanzania.

Makocha wa kigeni hawatumii nguvu nyingi katika kuwasifia wachezaji na timu zetu kwa ujumla. Tatizo linabaki kwetu sisi, kwani sifa zile zinakuwa ndio mwisho wa kutafuta mafanikio zaidi. Tunatakiwa tuwekeze sana kwenye soka, kwa maana ya nchi nzima. La sivyo tutaendelea kumiminiwa sifa nyingi ambazo mara nyingi hazifanani na hali halisi.

Mabenchi ya ufundi ya timu nyingi yamejaa kila aina ya upungufu, ni timu chache tu ambazo kweli zinafanya maandalizi sahihi kwa ajili ya ligi kuu na michuano mikubwa ya ngazi ya Bara la Afrika. Tunafungwa kila mwaka halafu tunasifiwa na makocha wa kigeni.

666 Total Views 2 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!